Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

January 23, 2018

MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA LUDEWA ATEMBEA KWA MIGUU KILOMETA KUMI ILI KUWAUNGANISHA WANANCHI WA KIYOGO NA KIPINGU.

 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Mh.Edward Haule akikagua eneo ambalo uanzishwaji wa barabara ya kuviunganisha vijiji vya Kiyogo na Kipingu itapita.
 Mh.Haule akielekezwa na mwananchi eneo ambalo barabara itapita .
 Mh.Haule akiwa katika picha ya pamoja na mwenyekiti wa waandishi wa habari mkoa wa Njombe Bw.Nickson Mahundi aliye shika kikombe,Bw.Malamba katibu Tarafa ya Masasi na mwenyekiti wa kijiji cha Kiyogo Bw.Milinga.
 Mh.Haule akiwa na viongozi na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kiyogo.

 Haya ndio maji yanayotumiwa na wananchi wa kijiji cha Kiyogo wilayani Ludewa katika matumizi ya nyumbani.
 Hili ndilo daraja linaloviunganisha vijiji vya Kingole na Kiyogo kata ya Masasi
 Mh.Haule na masafara wake wakijiandaa na safari ya kukifikia kijiji cha Kipingu
 Daraja la mto Ruhuhu linalojengwa ili kuunganisha mkoa wa Njombe na Ruvuma kupitia wilaya ya Ludewa na Nyasa.
 Mh.Haule akiwa na katibu tarafa Bw.Malamba eneo la kijiji cha Kipingu baada ya kutembea umbari mrefu kutoka kijiji cha Kiyogo.
  Daraja la mto Ruhuhu linalojengwa ili kuunganisha mkoa wa Njombe na Ruvuma kupitia wilaya ya Ludewa na Nyasa.
Mh.Haule akiwaanga viongozi na wananchi wa Kiyogo mpakani mwa vijiji hivyo.



Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ibumi Mh.Edward Haule ameanza mpango wa kuviunganisha vijiji viwili katika miundombinu ya barabara ili kurahisisha wananchi wa vijiji hivyo kutembeleana kwa urahisi katika kufanya biashara.

Akizungumza na viongozi wa vijiji hivyo wakati wa kukagua maendeleo ambayo barabara ya kuunganisha kijiji cha Kiyogo na Kipingu Mh.Haule alisema kuwa kutokana na umuhimu wa barabara hiyo imemlazimu kutembea kwa miguu ili kujionea ugumu wa kuunganisha vijiji hivyo uko wapi.

Mh.Haule alisema kuwa wananchi wa kijiji cha Kiyogo wamekuwa wakiishi kama wako kisiwani kutokana na ukweli kwamba mahitaji yao huyapata mkoa wa jirani ambao ni Ruvuma hivyo uanzishwaji wa barabara hiyo itawasidia pia msimu wa mvua kufuata matibabu katika Hospitari kubwa ya Lituhi iliyoko wilaya ya Nyasa.

Alisema mto Ruhuhu ambao wananchi hao huuvuka na kwenda kupata mahitaji Ruvuma umekuwa na Mamba wengi pamoja na Viboko hivyo ni hatari kwa maisha yao lakini kwa kupitia kijiji cha Kipingu watakuwa na uwezo wa kuvuka katika daraja ambalo linajengwa na Serikali ili kuunganisha wilaya ya Ludewa na ile ya Nyasa.

Mh.Haule alisema kuwa kutokana na uzoefu wake katika uanzishaji wa barabara za vijiji barabara ya kuunganisha kijiji cha Kiyogo na Kipingu itakamilika mapema kwani kinachotakiwa wananchi wa vijiji hivyo kujitolea kuchimba kamailivyofanywa na vijiji vingine wilayani hapa ili baadae Serikali itie mkono wake.

“nimetembea kwa miguu ili kuona maeneo ambayo barabara itapita na sio mara yangu ya kwanza kutembea porini kuandaa maeneo ambayo barabara itapita,nimefanya hivi katika vijiji vingi ninachokiomba wananchi wajitokeze tuweze kuanza kuchimba na baadae hata tukiomba Serikalini ionekane kuna nguvu za wananchi zilifanya kazi”,alisema Mh.Haule.

Mh. Haule aliwasifu baadhi ya wananchi walioungana na msafara wake katika kukagua barabara hiyo aidha aliwataka wanachi hao kuwaeleza wenzao  namna ya barabara hiyo itakavopita na umuhimu wa  nguvu za wananchi katika uanzishwaji  wa barabara hiyo.

Akitoa taarifa ya wananchi mbele ya  mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa mweyekiti wakijiji cha Kiyogo Bw. Gerhath Milinga alisema kuwa wananchi wake wanashauku kubwa ya uanzishwaji wa barabara hiyo kwani ni ukombozi wa mambo mengi ambayo yalikuwa ni kikwazo kwa maendeleo yao.

Bw.Milinga alisema kuwa kijiji hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ambapo wananchi wanalazimika kuyatumia maji yaliyochafuliwa na wachimbaji wa madini hali ambayo inahatarisha usalama wa afya zao.

Alisema kuwa kufunguliwa kwa barabara hiyo kutawawezesha wananchi wakijiji chake kusafiri kwa kutumia bodaboda na kuweza kuvuka daraja la Kipingu ili kufuata huduma za afya mkoa wa Ruvuma kwani zahanati waliyo nayo ina mhudumu mmoja tu hali inayosababisha apatapo likizo Zahanati hiyo hufungwa.

Bw.Milinga alimuomba mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa kuzifanyia kazi changamoto za kijiji hicho ambazo zimekuwa ni kero kwa muda mrefu bila utatuzi hali inayowafanya wananchi kuichukia Serikali yao.

MWISHO.

No comments: