Mbunge
wa Kilombero, Peter Lijualikali na viongozi watatu wa Chadema wilayani
Malinyi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya kusanyiko lisilo
halali.
Mbunge
huyo amekamatwa jana Alhamisi saa 12:40 jioni akitoka kwenye kikao cha
ndani cha chama hicho kilichofanyika katika Kijiji cha Makerere
wilayani Malinyi.
Akizungumzia
kukamatwa kwa viongozi hao, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati,
Alfonce Mbassa alisema baada ya kumaliza kikao, mbunge huyo na viongozi
wengine walipanda kwenye magari ili kuondoka lakini ghafla lilitokea
gari la polisi na askari walimuamuru Lijualikali ashuke.
"Tulishuka
wote kujua tatizo ni nini lakini askari walimhoji Lijualikali kwa nini
amekwenda kufanya siasa Malinyi wakati yeye ni mbunge wa Kilombero,"
alisema Mbassa.
Alisema
walijaribu kuwaelewesha polisi kwamba kilikuwa ni kikao cha ndani
lakini askari walisisitiza kuwa lilikuwa kusanyiko lisilo halali.
Aliwataja
waliokamatwa pamoja na mbunge huyo kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema
Malinyi, Emmanuel Lukindo; Katibu wake, Sadi Lyampawe na Katibu wa
Uenezi wa wilaya, Lucas Lyambalimu.
"Lakini tulivyowabana polisi wametuambia wameelekezwa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika kuwakamata," alisema Mbassa.
Alipotakiwa
kuzungumzia tuhuma hizo, mkuu wa wilaya Kasika amesema ni kweli
ameagiza polisi kumkamata mbunge huyo kwa kuwa anafanya siasa nje ya
jimbo lake.
"Ndiyo,
nimetoa maelekezo akamatwe maana hakuna mbunge anayeruhusiwa kufanya
siasa nje ya jimbo lake na tunaendelea kumshikilia kwa mahojiano,"
alisema Kasika.
No comments:
Post a Comment