Ofisi ya Bunge imesema Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe hajanyang’anywa gari.
Taarifa
iliyotolewa na Bunge jana Alhamisi imesema kilichotokea ni kwamba,
gari hilo limerudishwa nchini ili dereva afuate utaratibu wa kupata
kibali cha kusafiri nje ya nchi.
Mbowe
yuko Nairobi nchini Kenya ambako Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu anaendelea na matibabu baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa
risasi Septemba 7 akiwa nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.
Bunge
limesema ni kweli gari lenye namba ya usajili STL 4587 aina ya Toyota
Prado limetengwa maalumu kwa ajili ya kumuhudumia Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni katika kutekeleza majukumu yake ya kikazi na
binafsi nchini.
“Kiongozi
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliomba gari ikamhudumie mjini
Nairobi nchini Kenya na Ofisi ya Bunge iliridhia ombi hilo na kuomba
taratibu zizingatiwe. Hata hivyo, ofisi iligundua kwamba gari ilikwenda
Nairobi na dereva hakupata kibali cha kusafiri nje ya nchi ambacho kila
mtumishi wa umma anayesafiri nje ya nchi lazima apate kibali hicho
kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi,” imesema taarifa ya Bunge.
Bunge
katika taarifa hiyo limesema kwa kuwa utaratibu haukukamilika, dereva
aliambiwa alirejeshe gari hilo nchini na kuliegesha katika Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa wa Arusha hadi utaratibu mwingine utakapokamilika.
“Dereva
yupo Dodoma anakamilisha taratibu ili ofisi iweze kumuombea kibali
Ikulu ndipo anaweza kurejea nchini Kenya kwa ajili ya kuendelea
kumhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,” imesema
taarifa.
Ofisi
ya Bunge imesema inasikitishwa kutokana na utaratibu unaotumiwa na
Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa kuzungumzia
masuala yanayohusu ofisi hiyo kupitia kwa msemaji wa chama kama
inavyoonekana kwenye mitandao ya kijamii akitoa malalamiko kwa niaba ya
ofisi hiyo.
“Ni
vyema ikaeleweka kwamba Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ni kama ofisi nyingine zinazohudumiwa na Sekretarieti ya Bunge
ambayo inapaswa kufuata kanuni na taratibu za uendeshaji wa Ofisi na ni
kosa kwa mtumishi kwenda kinyume na masharti ya Utumishi wa Umma,”
taarifa hiyo imesema.
Imeelezwa
katika taarifa kuwa ni dhamira ya Ofisi ya Bunge kuendelea kumhudumia
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kufuata misingi na
kanuni za utumishi wa umma na zile za Bunge bila kuchanganya na siasa.
“Ofisi
ya Bunge inauhakikishia umma kuwa taratibu zikishakamilika Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ataendelea kuhudumiwa popote
atakapokuwa,” imesema taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment