Katibu
Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad anatarajiwa
kuzuru mikoa ya Kusini mwa Tanzania katika kipindi ambacho bado kuna
sintofahamu kuhusu nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho.
Mwanasiasa
huyo ambaye ataongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya chama
hicho, Julius Mtatiro pamoja na Wajumbe wa Baraza Kuu watazuru Mtwara na
Lindi ikiwa ni miezi michache baada ya Mwenyekiti wa chama hicho
anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Profesa Ibrahim
Lipumba kuzuru eneo hilo la kusini.
Akizungumzia
ziara hiyo, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa
chama hicho, Mbarala Maharagande alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni
kukagua shughuli za chama na kupokea maoni ya pamoja ya namna ya
kuboresha utendaji wa chama hicho kwa ngazi za chini.
Maalim
Seif anatua katika eneo hilo wakati ambapo kukiwa na mvutano baada ya
baraza la madiwani kufanya jaribio lililoshindikana la kumng’oa Meya wa
Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, Geofrey Mwanchisye.
Jaribio
hilo liligonga mwamba baada ya Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Sifaeli
Kulanga kueleza kuwa hoja zao hazina msingi kwani tuhuma zao kuhusika
na matumizi mabaya ya fedha za umma yanakinzana na ripoti ya kamati
maalum iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Kesi
kuhusu Uenyekiti wa chama hicho inaendelea Mahakamani ambapo Baraza Kuu
la chama hicho linapinga barua ya Msajili inayomtambua Lipumba kama
Mwenyekiti wa chama hicho wakati ambapo Baraza hilo lilikuwa limetangaza
kumfuta uanachama.
No comments:
Post a Comment