Rais John Magufuli amemwaga
burungutu la fedha kusaidia Waislamu ambao watakwenda kuhiji Agosti
mwaka huu.
“Najua kuna Waislamu watakwenda kuhiji nadhani Agosti,
naomba kama inaruhusiwa na mimi nichangie kitu kidogo kadri ya uwezo
wangu, nimejipigapiga na mimi nikaona nichangie kitu kidogo, kana
inaruhusiwa naomba Mufti uje nikukabidhi,” alisema Magufuli alipokuwa
akizungumza katika Baraza la Eid el Fitri jijini Dar es Salaam jana.
Baada ya kutamka maneno hayo, alishika begi dogo kama briefcase akampa
msaidizi wake ambaye alilifungua na kuchomoa burunguti la noti na
kumkabidhi Mufti, Sheikh Mkuu Zubeiry Ally.
Hata hivyo haikufahamika
kiasi cha fedha hizo. Kabla ya kutoa fedha hizo, awali akimkaribisha
Rais Magufuli kuhutubia, Mufti Zubeiry aliwataka Waislamu kutumia
Bakwata katika safari za hija zitakazogharimu Dola 3,800 kwa mtu mmoja.
Awali Magufuli alikuwa ameahidi kitita cha Sh2 milioni kwa kijana
aliyesoma dua katika sherehe hizo pamoja na kiasi kingine kama hicho kwa
kundi la Kaswida lililotumbuiza.
Katika hotuba yake, Dk Magufuli alisema Serikali yake ipo katika mchakato wa kurejesha
heshima yake ingawa kuna watu wachache watakaoguswa kwa kuisababishia
hasara Serikali.
Rais Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi katika baraza hilo
la Eid el Firti alisema Tanzania ni nchi tajiri lakini baadhi ya watu
wamesababisha watu waendelee kuwa masikini.
“Tanzania hii ni tajiri
sana, kila kitu kipo. Juzi mpaka wamegundua Helium tani za kutosha. Kila
madini yapo hapa. Lakini kwa nini tuko masikini? Kwa nini watu wana
shida? Ndiyo maana tumeamua kwa niaba yenu turudishe heshima yetu.
tulete mabadiliko ya kweli na katika kufanya hayo wapo watu
watakaoguswa, lakini ni wachache sana kuliko wale waliokuwa wanaguswa
kwa kuibiwa, ni wachache waliokuwa wanadhulumiwa,” alisema Rais
Magufuli.
Alisema kwa miezi saba tangu alipochaguliwa kuingia madarakani
Serikali yake imetekeleza mambo kadhaa ikiwa pamoja na kutoa elimu bure
kwa shule za msingi na sekondari, kurudisha nidhamu ya watumishi wa
umma, kudhibiti matumizi mabaya ndani ya Serikali, kuongeza mapato na
mengineyo.
“Pamoja na hatua hizo ni dhahiri kuwa bado tuna safari ndefu
katika kutimiza yale tuliyokusudia na tuliyowaahidi Watanzania. Naomba
niwahakikishie kwamba dhamira ya kuwahudumia kwa nguvu zetu zote pamoja
na vipaji vyote bado tunayo. Tuna sababu ya msingi na tuna imani kuwa
Mungu yupo kuhakikisha kuwa tunaipeleka nchi yeti mbele...” alisema
Rais Magufuli huku akiwataka waumini hao kuiombea Serikali.
Aliwataka
viongozi wa dini ya Kiislamu kuwahimiza waumini wao kushiriki katika
shughuli za maendeleo hususani katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano ambao utekelezaji wake umeanza mwezi huu.
“Tusipofanya kazi
hatutapata pesa. Ndiyo maana wale waliozoea kupata fedha za bure
wameanza kusema fedha zimeisha mifukoni. Hela haiji bila kufanya kazi,”
alisema.
Kuhusu mali za Waislamu zilizodhulumiwa, Rais Magufuli
alisema atawasaidia kuzirejesha.
Alimpongeza Mufti wa Baraza la Waislamu
Tanzania (Bakwata), Zubeiry akisema alikuwa mstari wa mbele katika
kurejesha mali hizo kabla hata hajapewa cheo hicho.
“Nakumbuka wakati
nikiwa Waziri wa Ardhi, kabla hujawa Mufti, pamoja na viongozi wa Bakwata na
wengine, ulifika ofisini kwangu ukieleza jinsi mali za Waislamu
zilivyokuwa zinadhulumiwa.
"Ninafamu pamekuwa na hiyo tabia ya baadhi ya
viongozi wenye mali kuwatumia viongozi wa Bakwata na dini nyingine
katika kuwarubuni na kuingia ubia, mali hizo baadaye huwa zinapotea
kabisa,” alisema na kuongeza:
“Tujitahidi kwa nguvu zote kusimamia
mali hizi, zisije kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani. Tunapenda
wawekezaji lakini wanachokiahidi hawatekelezi, haiwezekani.
"Haiwezekani
na wala haikubaliki kwa watu kwa ujanja wao na wakati mwingine kwa
kutumia wanasheria wao kukalia mali za Waislamu. Mali za Waislamu lazima
zirudi na za Wakristo zirudi ili amani iwepo.”
Baraza hilo
lilihudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu Ali Hassan
Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Katibu wa Bakwata
Sheikh Suleiman Lolila na mabalozi wa nchi mbalimbali na waumini wa dini
hiyo.
No comments:
Post a Comment