BARAZA
la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limeendeleza
msimamo wake wa kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, uliopangwa kufanyika
Julai 23, mwaka huu mjini Dodoma.
Katika kuhakikisha linatimiza azma yake hiyo, baraza hilo limesema
wanachama wake wapatao 4,000 wamejiandaa kushiriki kwenye shughuli hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuhojiwa
kwenye Kituo Kikuu cha Polisi, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole
Sosopi, alisema kuna vijana watakaotoka sehemu mbalimbali ili kuzuia
mkutano wa CCM.
Sosopi alisema Bavicha watakwenda Dodoma kuzuia
Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kile walichodai kusaidia Jeshi la Polisi
kutekeleza amri yake ya kuzuia mikutano ya kisiasa hadi 2020.
Alisema
pia kuna watu wamejitolea kutoa magari kwa ajili ya kuwabeba vijana hao
ili kuwafikisha Dodoma kuunga mkono agizo la polisi.
Sosopi pia
aliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua viongozi wa Umoja wa Vijana
wa CCM (UVCCM) kutokana na kauli zao za vitisho walizozitoa dhidi ya
Bavicha hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 4, mwaka huu, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamad Shaka, aliionya Bavicha wasiende Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kuwa
watatumia kila mbinu kuwazuia ili kulinda heshima ya chama chao.
Sosopi alisema wao hawataki matatizo wala vurugu bali wanachofanya ni kutii agizo la polisi kwa unyenyekevu.
"Mkuki
kwa nguruwe kwa binadamu mchungu kwani Rais alipopiga marufuku mikutano
ya kisiasa hadi 2020, CCM walichekelea wakiamini kuwa Chadema
tumekomolewa lakini iweje sasa Jeshi la Polisi likubali kuruhusu mkutano
wao wakati Chadema hata mikutano ya ndani tunazuiliwa?
"Hatutanii
hata kidogo na wala CCM wasidhani kuwa hatutakwenda Dodoma lakini
tunaliomba Jeshi la Polisi litende haki juu ya kauli za uchochezi kwani
nilitegemea viongozi wa UVCCM wangekamatwa na jeshi hilo lakini
tunaokamatwa ni sisi tu," alisema Ole Sosopi.
Akizungumzia suala
la kuhojiwa na polisi jana, Ole Sosopi alisema alikuwa kituoni hapo
kuhojiwa kwa kosa analodaiwa kufanya Juni 18, mwaka huu la kutoa kauli
za uchochezi.
Sosopi alikamatwa mara ya kwanza Juni 26, mwaka huu mkoani Iringa na kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam na
kuhojiwa kwa kosa hilo katika shughuli ya mahafali ya wanachama wa Chadema waliomaliza vyuo vikuu.
Sosopi alisema baada ya kuhojiwa jana na polisi, anatakiwa kuripoti tena kituoni hapo Julai 18, mwaka huu.
Akizungumzia
suala la Sosopi, mwanasheria wake, Frederick Kihwelo alisema Sosopi
aliripoti kituoni hapo kwani anakabiliwa na tuhuma ya kutoa lugha ya
uchochezi.
Alidai lengo la mteja wake ni kuhakikisha polisi
wanatenda haki bila upendeleo kwani kazi yao kubwa ni kulinda usalama wa
raia na mali zao
Alisema baada ya kuhojiwa na polisi jana,
atatakiwa kufika tena kituoni hapo Julai 18, mwaka huu wakati huu
upelelezi unafanyika na ushahidi kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaki
ya Jinai (DPP) ili aamue kama kuna kesi ya kujibu au la.
No comments:
Post a Comment