Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

August 04, 2015

Magufuli Kuchukua Fomu ya Urais Leo Saa Sita Katika Ofisi Za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)


MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli leo anatarajiwa kuchukua fomu ya uteuzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kusaka wadhamini na kisha kuidhinishwa kuwa mgombea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Waziri huyo wa Ujenzi anatarajiwa kuchukua fomu saa sita kamili mchana, na kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, mgombea huyo atafuatana na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan na viongozi waandamizi wa chama hicho tawala. 
 
Nape aliwaambia waandishi wa habari jana katika Ofisi Ndogo ya CCM, Mtaa wa Lumumba Dar es Salaam kuwa Dk Magufuli na msafara wake, wataondoka katika ofisi hizo saa tano asubuhi kwenda Ofisi za NEC zilizoko Mtaa wa Garden katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

“Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli atachukua fomu kesho (leo) saa sita mchana. Msafara wake utaondoka hapa (Ofisi Ndogo) saa tano kamili na ataambatana na mgombea mwenza na viongozi waandamizi akiwamo Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Katibu Mkuu, wajumbe wa Sekretarieti, Kamati za Siasa za Wilaya na Mkoa wa Dar es Salaam,” alieleza Nape.

Aliongeza kuwa msafara huo, utapitia katika barabara za Morogoro, Bibi Titi Mohammed na Ohio, na kurudi kwa njia hizo hadi Ofisi Ndogo Lumumba ambako Dk Magufuli atatoa neno la shukrani kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa chama hicho kikongwe na tawala nchini, na Watanzania kwa ujumla.

“Dk Magufuli akishachukua fomu atarejea hapa Ofisi Ndogo na kutoa neno la shukrani kwa kuzungumza na Watanzania wataokuwapo, wanachama na mashabiki wetu ifikapo saa saba mchana,” alieleza Nape ambaye mwishoni mwa wiki aliongoza katika kura za maoni za ubunge katika Jimbo la Mtama mkoani Lindi.

Dk Magufuli alishinda uteuzi wa kuwa Mgombea Urais wa CCM katika vikao vyake vilivyofanyika mjini Dodoma mapema mwezi uliopita, akiwashinda wenzake 38 ambao walikuwa miongoni mwa 42 waliochukua fomu.

Alikuwa miongoni mwa wagombea watano waliopitishwa na Kamati Kuu na kisha kupigiwa kura na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akiwa na Dk Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali, January Makamba na Bernard Membe, ambapo yeye, Dk Migiro na Balozi Amina walishinda kwenda kupigiwa kura katika Mkutano Mkuu.

Katika Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 11, mwaka huu, Dk Magufuli aliwashinda wanawake hao wawili na kupewa jukumu la kupeperusha bendera ya CCM Oktoba 25, dhidi ya vyama vingine.

No comments: