Prof. Lipumba apigwa mabomu, akamatwa
Wafuasi kibao CUF mbaroni, Ni katika kukumbuka wenzao waliouawa Zanzibar 2001.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba akiwa
chini ya ulinzi , eneo la Mtoni Mtongani jijini Dar es Salaam baada ya
Polisi kusitisha maandamano ya chama chake jana. (Picha: Salome
Kitomari)
Nguvu hiyo ya Polisi ilitumika wakati wa kuzuia msafara wa
Mwenyekiti huyo kuelekea eneo la Zakhem, Mbagala, kulikokuwa
kumeandaliwa na mkutano wa hadhara, kutoa taarifa kwa wafuasi waliokuwa
wamekusanyika, kuwa mkutano na maandamano yamezuiliwa na Polisi.
Mkutano huo ambao ungetanguliwa na maadamano kutoka ofisi za wilaya
ya Temeke kwenda Zakhem kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 14 ya mauaji
ya wafuasi wake zaidi ya 30 waliouawa Januari 27, 2001 na Jeshi la
Polisi Zanzibar wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa
rais wa Zanzibar wa mwaka 2000.
Kutokana na purukushani hizo za jana, polisi wenye silaha na
virungu walitembeza kichapo kikali kwa wafuasi waliokahidi amri ya
polisi kuwa taka watawanyike, huku wakiwashusha waliokuwa kwenye magari.
Baada ya kipigo cha dakika 30, polisi wakiongozwa na S .Zacharia,
ambaye mara kwa mara alizungumza na Prof. Lipumba na viongozi wengine
kutawanyika bila mafanikio, walimteremsha kwenye gari na kumpakiza
kwenye gari ya polisi.
Katika kamatakamata hiyo wafuasi zaidi ya 15 walitembezewa kichapo
na kuswekwa kwenye gari tatu za polisi, huku katika gari lililombeba
Prof. Lipumba akiwa na wafuasi wengine wawili.
Kabla ya purukushani hizo, Mwenyekiti wa Lipumba akiwa kwenye
msafara wa magari matatu waliotoka katika ofisi za Makao Makuu yaliyoko
Bunguruni hadi ofisi ya Wilaya ya Temeke na kuzungumza na wanachama
waliofurika kwenye ofisi hizo tayari kwa maandamano waliyokuwa
wametangaziwa.
Baada ya kuwasili katika ofisi hizo, aliwaeleza wafuasi wake kuwa
maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kutokea ofisini humo (
Temeke) hadi Zakhem Mbagala, yamezuiwa na polisi, hivyo ni vema
yasifanyike na kwamba atakwenda kutoa taarifa kwa wananchi waliokuwa
nyoka eneo la Zakhem.
Baada ya kutoa taarifa hizo, wafuasi hao walionekana kutoridhika na
kuanza kupiga kelele huku wakidai wako tayari kufa, lakini waandamane.
Mwenyekiti huyo alipata wakati mgumu kuwatuliza wafuasi hao ambao
walipinga kauli ya kutoandamana na kudai hata kama kiongozi huyo
atakwenda kwa gari watatembea kwa miguu au kupanda daladala kumfuta
kwenye mkutano.
Alisema katika barua ya polisi iliyopelekwa ofisi za CUF, Januari
26, mwaka huu, saa 12:30 jioni, ilitoa sababu tatu za kuzuia maandamano
hayo.
Prof. Lipumba alisoma barua hiyo kuwa ilieeleza Kaimu Kamishna wa
Kanda Maalum wa Polisi, akieleza baada ya kutafakari kwa kina wamezuia
maandamano hayo kwa madai kuwa siyo halali.
Alinukuu barua hiyo kuwa maandamano ya Januari 27, mwaka 2001,
hayakuwa halali, hivyo maandamano ya kumbukumbu ya mauaji ya wafuasi wa
chama hicho Zanzibar nayo siyo halali na hivyo hawatakiwi kuyafanya.
Aliendelea kumnukuu kuwa sababu nyingine zilizotolewa na polisi ni
kuwa taarifa za kiitelejensia zinaonyesha kuwa kutakuwa na vurugu,
kuvunjika kwa amani na watu kujeruhiwa, hivyo hakuna sababu za wafuasi
hao kuandamana wala kufanya mkutano.
Prof. Lipumba alisema sababu nyingine waliyotoa ni tishio la
vitendo vya kigaidi, hivyo maisha ya waandamanaji yatakuwa hatarini kwa
kuwa kuna uwezekano wa tukio la kigaidi kutokea.
Muda wote ambao kiongozi huyo akiongea na wafuasi hao, Polisi
wakiwa kwenye magari walionekana wakipiga doria za hapa na pale, hali
iliyowafanya wafuasi hao mara kwa mara kufuatilia kilichokuwa
kikiendelea.
Akizungumza baada ya kusoma barua hiyo, alisema Polisi inaona ni
halali watu kufa, lakini ni haramu kufanya maandamano kwa ajili ya
kumbukumbu ya kifo cha watu hao.
“Leo tungewaandikia barua kuwa tunaandamana kuunga mkono ufisadi na
wizi ndani ya serikali wangetuunga mkono, na Chama Cha Mapinduzi
kikitaka kuandamana kingepewa na mara kwa mara wanaandamana bila
kubugudhiwa," alisema.
Mwenyekiti huyo alisema vyama vya siasa vinatumia sheria namba tano
ya vyama vya siasa kuomba kibali cha polisi kufanya mkutano wa hadhara
na maandamano, lakini polisi wanatumia sheria namba 43 sura ya 322,
kuzuia maandamano na mikutano ya vyama vya upinzania kwa sababu zao.
Alisema Tanzania inakabiliwa na matatizo mengi kubwa ikiwa ni
kukosekana kwa utawala bora na demokrasia na kwamba maandamano ya
Januari 27, mwaka 2001, yalilenga kushinikiza uwepo wa Katiba mpya,
utawala bora na demokrasia, lakini wafuasi waliuawa.
"Leo tunawajibu kwa wenzetu 60 ambao waliokufa wakati wakipigana
haki, haki haipatikani katika sinia la ubwabwa bali inapiganiwa, woga ni
adui wa haki, tuondoe woga tusonge mbele hii ni nchi yetu sote, polisi
wanaona ninaongea nanyi hapa wanapita na magari yao kuwatisha," alisema.
Alisema baada ya kupata barua hiyo na kutafakari malengo makuu ya
chama hicho, wameona wasiandamane, lakini kwa kuwa katika eneo la Zakhem
kuna wananchi waliokuwa nyoka ni vyema akapenda kuwapa taarifa na
wananchi wa eneo hilo (Temeke), waendelee na shughuli nyingine.
Alisema polisi wamefanya makusudi kwa kuwa taarifa za maandamano na
mkutano huo walikuwa nazo tangu Januari 22, mwaka huu, lakini kwa
makusudi wakijibu barua na kuiwasilisha ofisini muda ambao ofisi
zimefungwa na wanachama walishapewa taarifa.
Baada ya kumaliza kuzungumza na wafuasi hao, Mwenyekiti huyo na
wafuasi wengine walioingia kwenye magari, na baada ya kutembea mita
chache kando na hospitali ya wilaya ya Temeke, walikuta polisi wenye
magari madogo na gari kubwa la maji ya kuwasha wakiwa wamefunga
barabara.
Baada ya hali hiyo kiongozi huyo na wafuasi wengine waliteremka na
afande S. Zacharia ambaye alijitambulisha kama Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa
wa Temeke, alisema hawana taarifa za maandamano wala mkutano, hivyo
wanamtaka arudi alikotoka.
Prof. Lipumba aliwaeleza kuwa wana barua iliyowakataza kufanya
maandamano na mkutano, lakini kwa kuwa eneo la Zakhem kuna wafuasi
waliokusanyika anakwenda kuwapa taarifa, jambo ambalo lilipingwa vikali
na polisi waliokuwapo.
Hata hivyo, jitihada za viongozi wa CUF kuzungumza na viongozi hao
wa polisi zilishindikana kutokana na viongozi wa Polisi kudai kuwa
hawana taarifa na kumtaka Mwenyekiti huyo kutopelekwa eneo la Zakhem.
Baada ya mabishano ya dakika 20, msafara wa Prof. Lipumba
uliendelea na walipofika kwenye mzunguko wa Mtongani, magari ya polisi
yalifunga barabara.
Lipumba na wenzake waliteremka na kuongea na polisi hao bila
mafanikio na baadaye alionekana kachero mmoja wa polisi akiwa amevalia
kiraia, akiwataka kutawanyika na kuwaeleza kuwa hawaruhusiwi kuendelea
na safari.
Baada ya kauli hiyo, alijitokeza ofisa wa polisi ambaye alitangaza
tahadhari ya kutaka watu kutawanyika na askari kuamriwa kuanza kurusha
risasi na mabomu hewani huku maji ya kuwasha yakimwagwa.
Purukushani hiyo iliambatana na kichapo kwa wafuasi waliokuwa ndani
ya magari manne ya CUF, likiwamo gari la waandishi wa habari na Prof.
Lipumba, kufunguliwa milango na waliokuwa ndani kuanza kushushiwa kipigo
kikali.
Polisi walionekana wakiwashambulia wafuasi hao kwa dakika 30 na
kuwasweka kwenye magari ya polisi na kuondoka nao, akiwamo Prof.
Lipumba.
Wananchi waliokuwa eneo hilo walitawanyika huku wengine wakifunga
biashara zao na kukimbia ovyo, ikiwa ni pamoja na kutafuta maji ya
kunawa kutokana na mabomu ya machozi yaliyokuwa yanarushwa.
Akizungumza na NIPASHE, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar
es Salaam, Simon Sirro, alisema wamekamatwa kwa,sababu walifanya
maandamano bila kupata kibali cha polisi.
“Waliomba kibali, lakini walinyimwa kwa sababu za kiusalama, wao
wametumia nguvu kufanya maandamano yasiyo rasmi,” alisema Sirro.
Alisema watu 32 akiwamo Prof. Lipumba walitiwa mbaroni na kwamba
wanaume ni 30 na wanawake wawili na kuongeza kuwa walikuwa wakiendelea
kuhojiwa jana jioni katika Kituo Kikuu cha Polisi.
SOURCE:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment