WANAUME WANAOPIGWA NA WAKE ZAO WATAKIWA KUJITOKEZA
Ni nadra kusikia mwanamume akilalamika kuwa amepigwa na mke au
mwenza wake. Suala hilo ni adimu zaidi katika nchi za Afrika hasa zilizo
Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zimefunikwa na blanketi la mfumo
dume.
Kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni woga, aibu
na kasumba ya mfumo dume, wanaume wanaonyanyaswa wamekuwa wakificha aibu
hiyo na kuendelea kubaki katika unyanyasaji huo.
Kutokana na ongezeko la matukio ya wanaume
kunyanyaswa na wake au wenza, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania,
(Tawla) kimetoa wito kwa wanaume kujitokeza ili kupata msaada wa
kisheria pindi wanaponyanyaswa.
Mwenyekiti wa asasi zisizo za kiserikali za katiba
na jinsia, (Zec) zinazoratibiwa na Tawla, Victoria Mandari anasema
matukio hayo ni mengi lakini wanaume wamekuwa wakiyafanya kuwa siri
pengine kwa kuona aibu.
“Wanaume watafute chama kitakachowasaidia kutetea
haki zao na kutengeneza hata sheria ambazo zitawasaidia kupata haki
zao,” anasema. Anasema sheria zinasema kuwa asiwepo mwanandoa
anayemnyanyasa mwenzake kijinsia, hivyo basi hata wanaume nao hawatakiwi
kunyanyaswa.
“Tatizo ni kuwa wanaume hawajitokezi wanaponyanyaswa, waseme ili wasaidiwe,” anasema.
Matukio ya wanaume kunyanyaswa na wake zao
yameendelea kutokea huku wanaume wakidai kuwa unyanyasaji huo
unachochewa na wingi wa vyama, asasi, na mashirika yanayotetea haki za
wanawake pekee.
Mwaka jana, Naibu Kamishna wa Polisi, Adolphina
Chialo alisema wanaume wengi sasa wanakwenda kushtaki katika madawati ya
kijinsia ya polisi pale wanaponyanyaswa.
Inaelezwa kuwa hata wanawake wanaowanyima unyumba waume zao bila sababu maalumu nao wanafanya unyanyasaji wa kijinsia.
Kamishna Chialo anasema wapo wanaume wanaofika vituo vya polisi wakiwa na majeraha baada ya kupigwa na wake zao.
Katiba Inayopendekezwa
Pamoja na unyanyasaji kwa wanaume, wanasheria hao
walizungumzia Katiba Inayopendekezwa na kusema kuwa licha ya kupingwa na
taasisi nyingi za kijinsia na kisheria nchini, kwa upande wao
imezingatia masuala ya jinsia ambayo awali, hayakutambuliwa katika
Katiba ya sasa.
Mandari anasema maoni yaliyotolewa na chama hicho katika Katiba Mpya yalifanyiwa kazi.
“Tumeona mambo mengi ambayo tuliyasema wakati wa
kukusanya maoni kwa mfano, Katiba Inayopendekezwa sasa inatambua kabisa
masuala ya ndoa, umri sahihi wa ndoa na umiliki wa mali,” anasema.
Anasema Katiba ya mwaka 1977 iliruhusu ndoa kwa
msichana wa miaka 14 suala analosema liliwanyima mabinti haki ya kusoma
na kuchochea unyanyasaji wa kijinsia.
“Ile sheria haikuwa nzuri kabisa, hebu fikiria
mtoto mdogo anaingia katika ndoa wakati hata maumbile yake bado ni
madogo, hata kura hawezi kupiga lakini anakuwa mke wa mtu,” anasema
Anasema zaidi jinsi Katiba Inayopendekezwa
ilivyoyafanyia kazi maoni yao yaliyohusu haki za wanawake na kusema kwa
sasa kuna marekebisho ya sheria ya kimila ambayo katiba ya zamani
haikumtambua mtoto wa kike kama mrithi wa mali isiyohamishika jambo
ambalo kwa sasa halipo.
Aidha, anasema sheria nyingi zilizokuwapo katika
katiba ya zamani zilionekana kukinzana. Kwa mfano, sheria hizo
hazikufafanua mtoto ni nani na ana haki gani na kwa upande mwingine
zikiruhusu mtoto kufunga ndoa.
“Tulitumia fursa hii vyema kwa sababu tulijua
kabisa katiba ni moyo na ikitengenezwa basi kuibadili huwa ni kazi
vigumu lakini tunashukuru maoni yetu yalifanyiwa kazi,” anasema
Katika kuhakikisha wanatoa maoni bora ya katiba,
Tawla walitembelea nchi za Afrika Mashariki ili kujifunza jinsi ambavyo
nchi hizo ziliunda katiba yenye manufaa hasa kwa upande wa haki za
kijinsia.
“Tulijifunza kwa kina kabla ya kutoa maoni yetu,
hatukutembea Afrika Mashariki tu, bali tulifika hata Afrika Kusini nia
ilikuwa ni kuhakikisha mwanamke anatambulika na anakuwa na fursa katika
katiba hii,” anasema.
Mwanasheria, Cecilia Assey anawaasa wanawake
kuacha woga pindi wanapokumbana na unyanyasaji kutoka kwa waume, wenza
au wanajamii kwani sheria zipo.
“Hapa tunapata elimu kuhusu katiba na masuala ya
jinsia lakini baada ya mafunzo haya tutaendelea na kazi ya kuwasaidia
wanawake wanaokumbana na changamoto katika jamii,” anasema.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment