Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

November 10, 2014

WANANCHI WA MAENEO YA MIGODI WILAYANI LUDEWA WAFURAHIA ZOEZI LA KULIPWA FIDIA YA MAENEO YAO MAPEMA.


makaa ya mawe Nkomangómbe


chuma cha Liganga

   chuma cha Liganga

Akiongea na mwandishi wa gazeti la majira jana ofisini kwake diwani wa kata ya Nkomang’ombe wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe Mh.Ananias Haule alisema kuwa wananchi wa kata yake ambao ndiko mgodi wa makaa ya mawe utatekelezwa  wamekuwa na furaha kubwa ya kulipwa fidia za maeneo yao mapema ili waanze kuandaa makazi mapya.


Mh.Haule alisema awali wananchi  wa maeneo ya Nkomang’ombe  kwenye  makaa ya mawe na wale wa Liganga ambako chuma kinapatikana hawakuwa na imani na Serikali kama itaweza kuwabana wawekezaji ili waweze kulipa fidia mapema lakini sasa imekuwa furaha kwao baada ya kuzipata taarifa hizi


Alisema kutokana na mpango huu wa kuanza kulipwa fidia zao wananchi wameanza kuwa na uhakika juu ya uanzishwaji wa migodi hiyo kwani ni miaka mingi kumekuwa na ahadi bila utekelezaji hali ambayo ilikuwa ikiwakatisha tama na kuona kama zilikuwa siasa tu zisizo na utekelezaji.


Mh.Haule alisema taarifa za awali alizozipata katika ofisi yake ni kuwa wananchi wa maeneo hayo watapewa elimu ndipo uthaminishaji wa maeneo yao kuhusiasa na malipo utafanyika lakini wapo wengine ambao tayari wameshaanza kutafuata maeneo mengine ya kuhamia kabla ya kulipwa fidia.


“Wananchi wamekuwa wakiilaumu Serikali kwa kuchelewesha mpango huu wa uanzishwaji wa migodi ya mchuchuma na Liganga kwa kua kuwanawatu wamezaliwa na mpaka wamezeeka na wakafa walikuwa wakisikia migodi hii mikubwa itaanzisha lakini zilibaki kuwa porojo ila kwa kuanza kuwalipa fidia  wenye maeneo yao ni ishara nzuri ya utekelezaji”,alisema Haule.


Alisema licha ya Mh.rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kutoa tamko la kuwajengea nyumba wananchi hao ili waendelee na kijiji chao eneo jingine pia zimejitokeza changamoto kwa baadhi wa wananchi kutaka kulipwa fedha zao zote bila kuwajengea nyumba lakini kwa kushirikiana na wataalamu elimu itatolewa ili waone umuhimu wa kujengewa nyumba na si kulipwa fedha tu.


Alisema hatari ya kupuuza akizo la Rais ni kwamba baada ya kulipwa fedha kuna baadhi ya wanaume wanaweza kuwatelekeza wake zao pasipo makazi na kuhamia vijiji vingine na kuoa huko wakati familia zao zitabaki katika maisha ya kutangatanga hivyo ni muhimu wananchi watambue kujengewa nyumba ni bora zaidi kuliko kulipwa fedha.


Aidha afisa ardhi mteule wa wilaya ya Ludewa Bw.Joseph Kamonga alisema wawekezaji watashirikiana na wataalamu kutoka Serikalini katika kutoa mafunzo ya awali kabla ya kufanyika uthaminishaji hivyo wananchi wanatakiwa kujiandaa kwa elimu hiyo.


Bw.Kamonga alisema kitakachofanyika ni malipo ya fedha kutokana na eneo la mwananchi na kujengewa nyumba hivyo viongozi wa vijiji husika wanatakiwa kukaa na wananchi wao ili kuanza kuwaelimisha kwani kuna baadhi ya watu wakishapata fedha hufanya matumizi mabaya na kuziacha familia katika umasikini uliokithiri.


Mwisho.



No comments: