Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

November 10, 2014

WANANCHI WA KIJIJI CHA NKWIMBILI WILAYANI LUDEWA WAANZA KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI SAFI NA SALAMA

Wananchi wa kijiji cha Nkwimbili kata ya Lupingu Wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe wameanza kunufaika na mradi wa maji safi na salama ambao umejengwa kwa ufadhiri wa fedha za TASAF ikiwa bado haujakamilika ili kusambaza maji hayo katika kijiji kizima.


Akiongea kijijini hapo kaimu afisa mtendaji wa kata ya Lupingu Bw.Joseph Nkwera alisema mradi huo utatumia kiasi cha shiringi 240 milioni mpaka utakapo kamilika hivyo ni matarajio makubwa kuwa hakutakuwa na shida  ya maji kama ilivyokuwa awali kwani wananchi hao walikuwa wakitembea umbali mrefu kuyafuata maji hayo.


Bw.Nkwera alisema kutokana na ushiriki mzuri wa wananchi wa kijiji cha Nkwimbili katika mradi huo wataalamu waliweza kufanya kazi nzuri na kwa haraka hivyo kama wananchi wataendelea na moyo huo wa kujitolea basi hata mwaka 2015 hautafika mradi utazinduliwa.


Alisema kutokana na shida kubwa aliyowapata  wananchi hao katika suala la maji safi na salama kwa muda mrefu ndio sababu iliyowafanya kujitokeza kwa wingi katika maendeleo ya kuchimba mitaro na uvutaji wa mabomba hali ambayo iliwashangaza wataalumu ikiwa ni tofauti na vijiji vingine ambavyo waliwahi kufanya kazi.


“wananchi wamekuwa na furaha kubwa ya kupata huduma ya maji safi na salama tofauti na ilivyokuwa awali licha ya kuwa kijiji hiki hakuna miundombinu ya barabara ya gari linaloweza kuleta  vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya maji lakini waliweza kuvibeba na kuvifikisha maeneo husika bila ya malipo hali ambayo ilionesha kwa wataalamu kuwa ni kweli wananchi hawa walikuwa na shida ya maji”,alisema Bw.Nkwera.


Bw.Nkwera alivitaka vijiji vingine kuiga tabia ya wananchi wa Nkwimbili kwa kufanya kazi kwa moyo ili kujiletea maendeleo yao bila kuisubiri Serikali au wanasiasa kutika maendeleo kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuishawishi Serikali na wafadhiri kuongeza miradi mingine ya kimaendeleo.


Naye kaimu muhandisi wa maji wilaya ya Ludewa,Muhandisi Marichela Maisha alisema mradi huo unaotekelezwa katika kijiji cha Nkwimbili kata ya Lupingu pia unatekelezwa katika kata ya Makonde wilayani hapa hivyo wananchi wanapaswa kuiga mfano wa wananchi wa Nkwimbili kwani wamekuwa chachu ya maendeleo katika vijiji vingine.


Muhandishi Maisha alisema kuwa kijiji cha Nkwimbili ni kijiji ambacho hakina barabara na kutoka Lupingu ni zaidi ya kilomita 15 lakini wananchi wake wamekuwa wakiwasaidia wataalamu kubeba vifaa vyote vya ujenzi bila ya malipo yoyote kitu ambacho sio rahisi katika vijiji vingine.


Aliwataka wananchi hao kuendeleza utamaduni huo ambao wanao wa kufanya kazi za kujiletea maendeleo kwa nguvu zao kwani kwa kufanya hivyo kijiji hivyo kitakuwa mbele katika maendeleo tofauti na vijiji ambavyo wananchi wake ni wavivu na hawana moyo wa kujitolea.


Mwisho.



No comments: