Mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Juma Solomon Madaha akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mbwila
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Bw.Willium Waziri akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mbwila
Meneja wa kanda ya nyanda za juu Kusini Bw.Emmanuel Mwikwabe akiwa katika kampeni ya CHF
Mganga mkuu wa wilaya ya Ludewa Dkt.Msengi Mwendo akiwajibika
Mratibu wa CHF wilaya ya Ludewa Bw.Petrol Mahanza akiongea na wananchi
Wananchi wakisikiliza jinsi ya kujiunga na CHF
Mkuu wa
wilaya ya Ludewa katika mkoa wa Njombe Bw.Juma Solomon Madaha amewataka
wananchi wilayani hapa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii(CHF)ili kuweza
kutibiwa kwa bei nafuu kwa mwaka mzima kwani magonjwa hayapigi hodi
yanapoingia.
Bw.Madaha
aliyasema hayo jana katika vijiji vya Kiwe kata ya Mawengi na Mbwila kata ya
Luana wakati wa kampeni ya uhamasishaji kwa wananchi unaofanywa na viongozi wa
CHF kanda ya nyanda za juu kusini kwa kushirikiana na wilaya ya Ludewa juu ya
umuhimu wa kujiunga na mfuko huo ambao ni msaada mkubwa katika jamii.
Alisema
mfuko huo unaolipiwa kiasi cha shilingi elfu kumi kwa familia ya baba na mama
yenye watoto wanne wasiozidi umri wa miaka 18 kwa muda wa mwaka mmoja wa
kiserikali umekuwa mkombozi mkubwa kwa jamii kwa kutumia gharama ndogo za
matibabu pale mwanafamilia anapougua.
Bw.Madaha
alisema licha ya kuwa Tanzania kuna tatizo kubwa na ukosefu wa Dawa lakini kwa
kupitia CHF Serikali inawajibika kuchangia pale ambao wananchi wameshachangia
ili kupata dawa ambazo zitaweza kuwanufaisha wachangiaji tofauti na wale
wanaopata huduma ya papo kwa papo.
“Nasisitisha
jambo hili kwa kuwa naelewa umuhimu wake kwani kwa familia yenye watu sita
inatibiwa kwa kiasi cha shilingi elfu kumi kwa mwaka mzima hapo ukipiga hesabu
inakuwa kila mmoja ni kama shilingi 1500 tu hivi kuna huduma ya Afya ya papo
kwa papo unaweza kuipata kwa gharama hiyo nchini?”,aliuliza Bw.Madaha.
Alisema kama
kila familia itachangia mfuko huo basi tatizo la ukosefu wa dawa nchini litakwisha
kabisa hasa zahanati za vijijini kwani mpango wa Serikali ni kuwachangia mara
mbili wale ambao tayari wameonesha kuchangia katika huduma za mfuko wa afya ya
jamii.
Mratibu wa
mfuko huo wilayani Ludewa Bw.Petrol Mahanza alisema mwamko wa jamii katika
kuchangia mfuko huo bado hauridhishi kutokana na elimu ndogo waliyonayo kuhusu
jambo hilo hivyo kupitia kampeni hiyo ambayo itafanyika kwa muda wa siku 10
inaweza kusaidia kuwahimiza wanajamii kujiunga nao.
Bw.Mahanza
alisema bado familia ambazo zilichangia mwaka uliopita na hazikuugua zinahoji
matumizi ya fedha zao jambo ambalo sio sahii kwani michango hiyo ni ya mwaka
mmoja mmoja na kila mwaka familia inatakiwa kuchangia upya.
Aidha meneja
wa kanda ya nyanda za juu kusini Bw.Emmanuel Mwikwabe alisema Serikali
inampango mzuri wa huduma za Afya kwa wananchi wake hivyo kila familia inapaswa
kuchangia ili kunufaika na mpango huo ambao hutolewa nyongeza ya fedha ili
kuwaunga mkono kwa wale waliochangia.
Bw.Mwikwake
alisema katika mpango huo wa mfuko wa afya ya jamii licha ya mchangiaji
kupatiwa dawa pia pesa aliyochangia inatumika pale anapohitaji vipimo na hata
rufaa kutoka katika zahanati mpaka hospitari ya wilaya bado familia itatumia
kiasi hicho cha shilingi elfu kumi.
Alisema
mpango huo ulianzishwa hapa nchini mwaka 2001 na kufanya vizuri katika baadhi
ya maeneo hivyo wananchi wa mkoa wa Njombe hususani wilaya ya Ludewa wanapaswa
kuchangamkia huduma hiyo ili kutumia gharama nafuu katika suala zima la
matibabu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment