RIWAYA;MAMA YANGU MUUAJI
MTUNZI;Moringe Jonas
MAWASILIANO;jonasymoringe@gmail.com
SEHEMU YA PILI
Ilipoishia,,,,,
Lakini kabla hata ya kumfikia Yule binti mvua kubwa ilianza
kunyesha eneo lile walilokuwa na hata walipojaribu kutoka kuna nguvu ya ajabu
iliwazuia kufanya hivyo.
‘’Haya maajabu mvua gani ituzunguke sisi pekee?’’Alisikika
kijana mwingine akiacha kufanya kazi ya kumchuna Yule nyoka.
SONGA NAYO…..
‘’Jamani huyu nyoka ana maajabu tuna upofu halafu anatuletea
mvua ya namna hii’’Aliongea mmoja wa walev ijana waliokuwa wamepoteza uwezo wa
kuona.
‘’Ila mtaalam alitueleza hatari ya huyu nyoka’’Alisikika
kijana mwingine aliyekuwa akiendelea kuhangaika kuchuna ngozi ya Yule nyoka
licha mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha huku miale ya radi ikionekana katika
giza lililokuwa likiongezeka kadiri muda ulivyosonga mbele.
‘’Arisema
kuwa joka hiri ni Mungu wa makabira ya huko Bunjumbula’’Mwita naye aliongeza
wakati huo alikuwa amefanikiwa kutoka kwenye eneo lile palipokuwa pana mvua na
kumfikia Yule mtoto ambaye baada ya kumgeuza geuza aligundua kuwa alikuwa na
uhai.
Swali
alilojiuliza ni kivipi mtoto Yule alifika pale msituni,na je kuna uhusiano
wowote kati ya Yule nyoka na mtoto na maswali mengine mengi yaliyokosa majibu
sahihi.Baadaye alimwinua na kumpelekea chakula cha akiba walichokuwa nacho na
kuanza kumlisha,Delphine alijitahidi kula huku Mwita akiwa na hamu ya kumuuliza
juu ya sababu ya yeye kuwa pale.
Lakini
hata baada ya kushiba na kupumzika usiku ule hakufanikiwa kuongea naye kwani
hawakuelewana lugha kwani licha ya kuwahi kukisikia Kiswahili lakini Kiswahili
alichokiongea Mwita kilimchanganya na kumtisha hasa mtindo wake wa kumkazia macho
kila alipoongea ulisababisha akose kabisa kumwelewa.
Wakati
hayo yakiendelea wale vijana wengine waliokuwa wametingwa na kumchuna Yule
nyoka walikuwa wakihangaika kutoka kwenye lile eneo bila mafanikio yoyote.Mvua
kali iliyokuwa ikinyesha kuzunguka eneo walilokuwa iliwafanya hata baadhi
kuachana na kazi ya kumchuna Yule nyoka na kuhangaika kutoka pale.
Hata hivyo mmoja wao alizidi kuichuna na kuitengeneza vizuri
ile ngozi ya nyoka ambayo mganga wao aliwaeleza kuwa wakiipeleka basi
wangetengenezewa dawa ya kupata utajiri.
Umasikini ni kitu ambacho kijana Henrick Mbawala kutoka
Mbinga alikichukia kuliko kitu kingine chochote duniani, ambapo harakati zake
za kutafuta maisha zilimkutanisha na kijana Mwita katika machimbo ya dhahabu ya
Masuguru kabla ya kwenda Geita ambako walikutana na wenzao ambao juhudi zao za
kuukwepa umasikini zikiishia kwa Mganga mmoja wa jadi.
Mganga
huyo aliwataka wampelekee ngozi ya tumboni ya nyoka hatari aliyepatikana katika
msitu uliokuwa kati ya Rwanda na Burundi upande wa mashariki.Chuki dhidi ya
umasikini na tamaa za kupata mali ziliwafanya vijana wale kupanga safari kwa
takribani mwezi mmoja kabla na kuelekea Kigoma mwishowe walifika msituni hapo.
Mvua ya ajabu iliyoendelea kunyesha pale ni kama
ilimwongezea nguvu kijana Henrick na kutoijali kabisa kama wenzake
walivyofanya.Alikumbuka maneno ya mganga wake kuwa walitakiwa kuziweka roho zao
rehani ili kufanikisha zoezi lile.
‘’We Mngoni pesa itakuua wewe yaani hiyo mvua huiogopi
kabisa’’Aliongea kijana mwingine kutoka Iringa baada ya kufanikiwa kutoka pale
mvua ilipokuwa ikinyesha , ambaye kila mara alikuwa akitaniana na Henrick na
kujivunia utani wao ambao mara nyingi ulionekana kuwashangaza waliowasikia na
kuwatazama wakifikiri wangeweza hata kupigana.
‘’Kama umekuja kufanya utafiti ugopa mvua utaletewa turubai
la Umoja wa Mataifa, mimi baba yangu ni mcheza Mganda huko Ndumbi anategemea
nimpelekee kaptura yake nyeupe na kilo ya nyama kila jumamosi siwezi kuikwepa
mvua nimekuja kutafuta hukusikuja kutembea.
Mwenzangu wewe wajivunia kwenu mnakula mbwa machungu ya pori
mnaaita sijui mnafu na mzee wako anaogopa kukukaripia usije
kujinyonga’’Alitania Henrick na kuwafanya wenzake wacheke hali iliyomshtua na
kumwogofya Yule binti.
‘’Jamani nimeukumbua ughali macho yeyewe hayaoni’’Alinung’unika
kijana mmoja wa Kisukuma wakati huo Henrick alikuwa ameshamaliza kazi ya
kumchuna Yule nyoka ngozi iliyohitajika lakini kazi ilikuwa kutoka nayo eneo
alilokuwepo.
Alitumia zaidi ya nusu saa huku giza likiwa limeingia
Kurunzi walizokuwa nazo wenzake wakimmulikia hazikumsaidia kuona chochote hadi
alipokanyaga mwiba wa lile joka kwa bahati mbaya na kuanguka chini kama mzigo
akiangukia kiu kilichokuwa kikitoa harufu kali na kumwingia usoni mwake akianza
kubabuka ngozi.
‘’He! Ngozi hii hapa ila huyu mngoni mbona
haonekani?’’Ilisikika sauti iliyojaa utanio bila kujua kilichompata mwenzao ,
Mwita aliichukua ile ngozi na kuanza kuondoka hukua kiwa amemshika mkono Yule
binti ambaye moyo wake ulimtuma kumsaidia na kwenda kumlea na familia yake.
‘’Mungu wangu jamani Henrick Yule anayeyuka ‘’Aliongea Yule
kijana kutoka Iringa akiangalia mwili wa Mtani wake ukiyeyuka kutokana na
nyongo ya Yule nyoka iliyokuwa kali.
‘’Twende wewe urizani aliposema sadaka arimaanisha nini huyo
sadaka hujui Tumemwua Mungu wa watu?’’Sauti ya kutisha ya Mwita iliwafumbua
macho kuwa Henrick alikufa kama sadaka wapate kupata ile ngozi.
Kama msafara wa watumwa, watu watano walikuwa wakipita chini
ya miti mirefu ya msitu ule huku wakiwa na mizigo kichwani na kamba moja
ikiunganisha viuno vyao ili kuwasaidia waliopoteza uoni wao kutokana na sumu ya
nyoka.Walijua uelekeo wao ulikuwa sahihi kuokana na miti waliyoiona mchana huku
Mwita akionekana kama mwenyeji wa ule msitu kwani kila mara alikuwa
akiwakumbusha wenzake kuwa sehemu Fulani walipita mchana wa siku ile.
Baada ya mwendo mrefu miguu ya binti Yule ilianza kulegea na
hatimaye kupoteza nguvu kabisa na kujikuta akikaa chini kama mzigo,kumbukumbu
za vifo vya ndugu zake asubuhi ya siku ile huku yeye kiherehere cha kuangalia
choo kila aamkapo kikimkwepesha na kifo kile zilipita haraka haraka kichwani
mwake naye akifumba macho tayari kwa kuwafuata wazazi wake na ndugu zake kwa
kufa kwani aliamini kuwa kifo kilikuwa kimemfuata kila alipoenda licha ya muda
tuu kuchelewa yeye kufa.
‘’Jamani ngoja nisaidie huu mzigo mie nimbebe huyu
mtoto’’Aliongea Mwita akimtwisha ile ngozi mwenzake na kumnyanyua Yule binti
safari ikianza tena.Huku yote yakiendelea akili ya Yule binti ilishindwa
kuamini kabisa kama wale watu walikuwa wema kwani hakufanikiwa kuwaelewa kama
walikuwa watu wa wapi japo lugha waliyoongea aliifananisha na lugha
iliyoongelewa na watu kutoka nchini Kongo na Tanzania akielewa baadhi ya maneno
ambayo hayakumsaidia kuwaelewa wale watu vyema.
‘’Tutaweka kambi hapa halafu kesho tutaendelea na safari
yetu’’Mwita alitoa amri ambayo ilifuatwa na wote waliifuta na kuwekka mizigo
yao chini.Licha ya kunyeshewa na mvua na kupata baridi waliogopa kuwasha moto
kwani moja ya sharti walilopewa lilikuwa ni kutowasha moto ndani ya msitu kwani
kw akufanya hivyo mambo makubwa yangetokea na kushindwa kufanikisha
kilichowapeleka huko.
Walikula viazi vitamu walivyovibeba wakishushia kwa maji
chakula ambacho binti wliyemwokota ilimuia vigumu kuvila lakini kutokana na
njaa aliyokuwa nayo ilimbidi kujilazimisha kula.Sehemu yakulala iliandaliwa na
wakajipanga na kulala huku Yule mtoto akiwekwa katikati kabisa.
Asubuhi ya siku ya pili iliwakuta lakini walijikuta wapo
pale pale walipopambana na lile joka na kuliua huku ile ngozi ikiwa imerudi
kwenye mwili wa lile joka ambalo lilikuwa liihanaika kujiinua.Mwili wa Henrick
haukuonekana zaidi ya kiatu chake kioja kilichokuwa na kipande cha mguu wake wa
kushoto.
‘’Jamani hali mbay a likipona tumekwisha’’aliongea mmoja wa
wale vijana waliopoteza uwezo wa kuona na kuwafanya wenzao wajue kuwa walipona
macho yao.
‘’Kwa nini we kipofu’’sauti ya matani ilimtoka kijana
mwingine ambaye naye alipatwa na tatizo lie jana yake.
‘’Kipofu wewe mie mzima kabisa naliona joka likijiviriga
vema kutufuata’’Alimjibu na kushika vitu alivyoona vya lazima kukimbia navyo.
‘’Tuondoke hapa si sarama’’Sauti ya kukwaruza ya Mwita
ilisikika akimwinua Yule binti na kuanza kuondoka naye.
‘’Sauti ya kilio kutoka kwa Yule msichana baada ya kuliona
joka lile la ajabu ililifanya lile joka kuanza kuvimba kwa hasira tayari kwa
mapambano wakati huo mbele yake kulikuwa na Mwita na Yule binti pekee ambapo
wale wengine walikuwa wameshafika mbali.
Mwita hakuwa na chakufanya zaidi ya kujaribu bahati yake kwa
kutaka kukimbia na Yule binti lakini kabla hata ya kumaliza mita tatu alijikuta
akibwagwa chini na kujikuta alimwachia Yule mtoto kutokana na sumu iliyotemwa
na lile joka.
‘’Hesuuuu hesuuu hesuuu uleembu’’Sauti iliyopangiliwa
ilisikika na kumfanya Mwita ageuke na kuangalia ilikotokea ,hakuamini
alichokiona na kujikuta akitetemeka.
Lile joka lilitulia na wale watu waliliinamia huku wakiongea
maneno Fulani ambayo bila shaka ilikuwa ni ibada Fulani.Baada ya kama dakika
ishirini kitendo kingine kilifuata ambako ng’ombe wawili waliokuwa wamefungwa
jirani walichinjwa wakati huo Mwita alikuwa ameganda pale chini akishuhudia
yale mambo lakini hakuweza hata kusogeza kidole chake huku Yule mtoto akiwa
kama hana fahamu kutokana na mwonekano wake.
Hatimaye ibada ile iliisha na mmoja kati ya wale watu
alimsogelea Mwita na kumwamuru kwa ishara kuwa aondoke kitu kilichofanywa kwa
haraka sana akimbeba Yule mtoto na kuanza safari ya kurudi Tanzania.Safari
iliyojaa uoga ilichukua zaidi ya masaa sita hadi walipofika kando ya ziwa
Tanganyika ambako kama bahati kwao walikutana na boti iliyokuwa ikijiandaa
kuondoka kuelekea Kigoma na kama bahati alikutana na wale wenzake waliokimbia
kule porini.
‘’Mnyalu yuko wapi?’’Lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa
Mwita mara baada ya kuwachunguza wenzake.
‘’Hatujaonana naye tulidhani mpo wote’’alijibu kijana
mwingine akimwangalia Yule mtoto kwa huruma kwani alionekana amelegea sana.
‘’Mhh kweli tumeshindwa’’sauti nyingine ilisikika kuitoka
kwa kijana mwingine ,wakati huo boti lilikuwa likiondoka.
Safari iliyochukua siku tatu iliishia mbele ya kinyumba Fulani
kisiwani Ukerewe ambacho mwonekano wake kwa mbali ulionekana kuwashtua
waliokuwa wakielekea pale.Watu wengi walionekana kukaa kwa makundi makundi kila
mtu akiwa ana cha kuongea.
‘’Hii ni ajabu nyoka mkubwa vile kutokea majini na kummeza
mtu si hatari hii’’Ilisikika sauti ya mmoja wa watu waliokaa karibu kabisa na
waliposimama akina Mwita.
‘’Tatizo …’’alinong’ona Mwita na kuwafanya wale wenzake
warudi nyuma na kujadiliana kidogo kasha kuanza safari ya kuelekea sehemu
nyingine ambako walilala na hatimaye kuvunja rasmi kundi lao huku kila mtu
akipanga kufanya kitu kingine cha kujikibu maisha yake.Mwita akiwa na Delphine
walianza safari ya kuelekea kwao Mugumu ambako naye aliona ni sehemu sahihi ya
yeye kwenda kuishi baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kutafuta riziki.
Hali ya Delphine kiafya ilidhoofu kutokana na siku zile za
mateso na maumivu makali huku kumbukumbu za vifo vya wazazi wake zikijirudia
kichwani na kumpa maumivu makali,hali iliyompelekea kuumwa sana mara tuu
walivyofika Mugumu.Lakini kama hiyo haitoshi Delphine alikutana na mapokezi
hasi si tuu kutoka kwa wazazi wa Mwita bali hata kwa watoto wenzake ambao
walimwona kama kituko Fulani kutokana na sura yake ya Kinyarwanda ambayo
haikujificha licha ya kuwa na umri mdogo wa miaka mitano tuu.Kwa waliobahatika
kujua alikotokea ,kuna waliomwita jinni,mkimbizi ,mtoto wa nyoka ili mradi tuu
kumnyanyasa.
Hakuwa na jinsi zaidi ya kuvumilia kwani hakujua pa
kukimbilia wala hakumwona wa kumweleza matatizo yaliyomkuta zaidi ya Mwita
ambaye shughuli zake zilimtenganisha sana na Delphine.Alitamani aelewe lugha ya
wenyeji wake walau ampate rafiki wa kumfariji lakini kila aliyemwona alijitenga
naye huku sauti za vicheko vya kebehi vikisikika kutoka kwa kila aliyemwona.
Siku ,wiki miezi hatimaye miaka ikapita huku Delphine
akiilelewa lugha ya wenyeji na kuwa miongoni mwa wanawali wa pale Mugumu
ubaguzi juu yake ukafutika na hakuna aliyekumbuka tena kama ni mtoto wa
kuokotwa porini .Vijana kama ilivyokuwa ada walianza kumsimamisha njiani iwe
alipoenda kisimani ama porini kukusanya kuni yote ni kutaka kujaribu bahati ya
kuonja tunda ya Yule binti wa Kinyarwanda aliyemvutia kila aliyemwona hasa kwa
akicheka kwani mwanya wake ulizidisha uzuri wake ukiachana na uso wke mrefu
ulioonekana kama ni wa kuchorwa machoni pa wengi.
Licha ya kuwa na ujirani na ukaribu na familia ya mwita
ambaye kwa umri aliokuwa nao hakuwa na mtoto wala mke zaidi ya watoto wa kaka
na dada zake waliomwita baba mdogo ama mjomba Delphine alikuwa na urafiki wa
karibu sana na bibi mmoja ambaye licha ya kujulikana kama mkunga pia alikuwa ni
ngariba aliyehusika na ukeketaji wa wasichana wa kabila lile.Ukaribu wao
uliwachanganya wengi na hata kumtisha Mwita lakini mara nyingi alipomuuliza
alimjibu kuwa anajifunza kuwa mkunga na Yule bibi alisisitiza hilo.
Lakini akiwa hajui lolote kuhusu ukeketaji siku moja akiwa
katika kuandaa vifaa vya ukeketaji bila kujua akiamini ni vya ukunga Yule bibi
anamtaka aingie bandani kwani kuna kitu cha muhimu kilipangwa kunfanyika.
‘’Ni nini hicho bibi?’’aliuliza Delphine akionekana
kushangazwa na wingi wa watu waliokujwa wakiongezeka hasa wanawake na wasichana
wa umri wake.
‘’We uende ndani leo nakuachia rasmi kasi yangu ya kusalisha
‘’alijibu Yule bibi na kutangulia ndani.
, huku akiamini kuwa Delphine angemfuata .Tofauti na alivyodhani
Delphine alizunguka nyuma ya kibanda kile akijiamini akipishana na watu kadhaa
kabla ya kuanza kukimbia kuelekea shambani ambako aliamini lazima angemkuta
Mwita na kama alivyotegemea alimkuta akinywa maziwa baada ya kulima kidogo.
‘’Nini wewe mbona unanishtua’’Lilikuwa ni swali la kwanza la
Mwita baada tuu ya kumwona Delphine kwani ujio wake haukuwa wa kawaida.
‘’Sijui ila sipo salama’’alijibu Delphine akiangalia
alikotoka ambako aliona kundi la wanawake wakielekea upande walikokuwa.
‘’Nenda kajifiche pale kichakani ,nimeshaelewa’’Alielekeza
Mwita akijifanya anaendelea kunywa maziwa yake.
‘’We Mwita hujamwona Dela huku?’’aliuliza mama mmoja
akionekana mwenye hasira.
‘’Sijamwona si yupo kwa bibi?’’alijibu kwa swali hali
iliyozidi kuwaudhi wale wanawake.
‘’Tumetoka huko na katukimbia si ulisema unataka kuoa wewe
utamwoa mwanamke ambaye hajasafishwa?’’Swali lingine lilimtoka Yule mama ambaye
alihisi kuwa Mwita alijua aliko Delphine na aliamua kumficha.
‘’Si lazima kuoa mwanamke aliyesafishwa’’Sauti nzito ya
Mwita ilisikika akionekana kukerwa na utaratibu ule huku akisahau kama Delphine
alisikia kile alichokiongea.
‘’Anataka kunioa mimi? Kusafishwa? Kivipi? Mhhh naondoka
‘’aliwaza Delphine pale kichakani na kuamua kunyata akielekea porini zaidi akipita
mashamba kadhaa ambayo yalikuwa ni kama yamesahaulika na wamiliki wao kutokana
na nyasi zilivyokuwa zimesonga mazao.
Aliamua kukimbia kijiji kile kwani licha ya kusaidiwa na
kuokolewa na Yule mtu hakufukiria kuolewa naye ,alimchukulia kama baba yake sasa
kusikia suala la kuolewa naye kulimfanya aamue jambo moja tuu kukimbia na
kutorudi tena Mugumu.
Kukimbia alikimbia tena kukimbia haswa na hata kama
kungekuwa na mashindano angejizolea medali katika kila mbio ziwe fupi au ndefu
lakini swali lilikuja kichwabni mwake angekimbia hadi wapi mpaka lini na
alielekea wapi? Nguvu za kuendelea mbele zilimwishia baada ya kukimbia kama
kilometa ishirini hivi na kujikuta akikaa chini kama mzigo ulioangushwa huku
simulizi za wanyama wakali kutoka mbugani Serengeti zikipita akilini mwake na
kumfanya ainuke na kutaka kuanza safari.Lakini kabala ya kupiga hatua yoyote
kuna sauti ilimshtua na kumfanya aanze kutetemeka huku haja ndogo ikionekana
kulowanisha gauni lake chakavu na ile sauti ikizidi kuongezeka kadri muda ulivyosonga
mbele.
ITAENDELEA
Je, nini hicho?
Mama yaangu muuaji ni yupi?
No comments:
Post a Comment