Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

July 12, 2014

TEKNOLOJIA BVR YAWACHEFUA VYAMA VYA UPINZANI




  Kamishna wa tume ya taifa ya uchaguzi jaji John Mkwawa akizungumza na waandishi wa habari wa mkoa wa Njombe kuhusu kupeleka elimu kwa jamii ili wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari ya kudumu la wapiga kura kwa mfumo mpya.
 
VYAMA vya upinzani vimepinga teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR), itakayotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura vikidai mfumo huo umetumika Zanzibar, lakini bado una changamoto nyingi.
 
Hatua hiyo ilijitokeza jijini Dar es Salaam jana, wakati NEC ilipokutana na viongozi wa vyama vyote vya siasa, kikiwemo CCM, ili kupeana taarifa kuhusu maandalizi ya uboreshaji huo utakaoanza Septemba.


Pia, mkutano huo ulikuwa kwa ajili ya NEC kuwaonyesha viongozi hao jinsi mtambo mpya utakavyofanya kazi. Lakini ulipofika wakati wa kuonyeshwa mtambo huo, viongozi wa NEC walidai wako nyuma ya muda.


Uamuzi huo ulionekana kumkera Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), na hivyo kuhoji kwanini waliahidi kuwaonyesha mtambo  halafu waseme wako nyuma na muda.


“Mmetuambia kuwa mtatuonyesha jinsi mtambo huo utakavyofanya kazi, lakini sasa hivi mnasema muda umeenda, hivyo mtatuonyesha ulivyo tu bila ya kuona utendaji wake wa kazi, haina maana yoyote, kama hilo limeshindikana ni bora tuendelee na ratiba zingine,” alisema Lissu na kuungwa mkono na viongozi wengine.


Akizungumza na waandishi wa habari, Lissu alisema kuwa bado anaona kuna tatizo na kwamba kuna maswali mengi ambayo wanajiuliza na hawajapata majibu, hivyo bado hawajaelewa jinsi mfumo huo utakavyoleta mabadiliko na kuondoa changamoto zilizopo.


“Wamesema kitambulisho kitakuwa kina mfano wa kadi ya benki, kama ukikipoteza haupigi kura? Tume inaandikisha wapiga kura wengi sana na utaratibu wa sasa kama una kadi unaenda kujiandikisha na ukijiandikisha kwa sababu una kadi, kumbukumbu zako wanazo.


“Je, kama ulijiandikisha huna kadi, unaenda kujiandikisha kama mpiga kura mpya ambaye kumbukumbu zako haziko kwenye tume au unaenda kujiandikisha kama mpiga kura ambaye kumbukumbu zako ziko kwenye tume, lakini huna ushahidi wa kuwa na kadi?” alihoji.


Aliongeza kuwa kitu muhimu kinachohitajika kwanza ni mabadiliko ya sheria, kwamba tatizo kubwa lililopo mtu hata kama alijiandikisha akapoteza kitambulisho haruhusiwi kupiga kura, hivyo utaratibu huo hauwezi kuondoa tatizo.


“Namna ya kuliondoa ni sheria iseme wazi kwamba kama umejiandikisha, picha yako iko kwenye tume na ipo siku ya uchaguzi kwenye orodha ya kupiga kura, una haki ya kupiga kura kwani watu wanakufahamu na picha yako ipo,” alisema.


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, alisema tume imeeleza kuhusu mashine hiyo, lakini hawajaambiwa kampuni ambayo imehusika na jinsi gani inaweza kusimamia ikiwa na uzoefu gani.


Alisema Zanzibar wanatumia mtambo kama huo, lakini bado kuna matatizo mengi, hivyo tatizo sio mtambo ila ni utendaji.


Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema bado nchi iko nyuma kiteknolojia, kwani mtambo huo unatumiwa na nchi za Afrika tu, na kama ungekuwa na ubora ungetumika pia katika nchi zilizoendelea.


“Bado sijaona kama matatizo yataisha, nenda nchi zote za Ulaya, mfumo ni mmoja tu, wanatumia kitambulisho kwa kila kitu, lakini nchi yetu kila kitu kina mfumo wake,” alisema.


Mapema katika hotuba yake ya ufunguzi, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema mfumo wa BVR ni wa kuchukua au kupima taarifa za mtu kibaiolojia au tabia ya mwanadamu na kuzihifadhi katika kanzi data (Database), kwa ajili ya utambuzi.


Alisema kwa kutumia mfumo huo, wananchi wote wenye sifa za kuwa wapiga kura na wale walio na kadi za mpiga kura, watatakiwa kuandikishwa upya.


“Mtakumbuka kuwa vituo vya uandikishwaji uliopita vimekuwa katika ngazi ya kata, kwa utaratibu huu vituo vya kujiandikisha vimeongezeka kutoka 24,919 hadi kufikia 40,015 ambavyo vimewekwa katika ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa ili kuwezesha kuwa karibu zaidi na wananchi,” alisema.


Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, uchaguzi mkuu wa mwakani kwa mujibu wa Sensa ya 2012, utakuwa na wapiga kura 23,917,467 baada ya kutoa watu watakaokadiriwa watakuwa wamefariki.

No comments: