ALIYEKUFA NA MGANGA WA JADI WAKIWA SHIMONI AZIKWA HUKO HUKO
KIKOSI cha uokoaji kimeshindwa kuupata mwili wa Zuberi Kaima (45)
ambaye yeye pamoja na mganga wa jadi, Sophiani Khamis (60) walisadikiwa
kufa kwa kukosa hewa kwenye shimo walilokuwa wakichimba dhahabu.
Kaimu Kamanda wa kikosi cha Uokoaji, Augustino Magere alisema juzi
kuwa juhudi za kuutoa mwili wa marehemu huyo hazikufanikiwa kutokana na
kuwepo ufinyu wa nafasi ndani ya shimo hilo hivyo kushindwa kumfikia.
Alisema pia kutokuwepo kwa hewa ya kutosha iliyosababisha vifo vya
watu hao na hivyo kuhofia kusababisha madhara mengine yasiyotarajiwa kwa
waopoaji.
Hata hivyo mwili wa marehemu mganga wa jadi, Sophian Hamisi
aliyeoteshwa kuwepo kwa dhahabu katika eneo la Kangaye ‘A’ na
kusababisha maafa hayo kwa kukosa hewa umezikwa juzi mchana kwenye
makaburi ya Kangaye ‘ A’ wilaya ya Ilemela.
Naye Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Amina Masenza juzi alifika katika
eneo la tukio ambako mwili wa marehemu Zuberi ulishindikana kuopolewa na
kuwataka wanafamilia wafanye maridhiano ya maziko na kitakachokubalika
kifanyike.
Jeshi la Polisi mkoani hapa limethibitisha maziko hayo ambayo
yamefanyika kwenye miamba ya shimo hilo baada ya kukosekana nafasi ya
kuuopoa mwili huo na pia kuogopa kusababisha madhara mengine kwa askari
waliojaribu kuopoa mwili uliobakia shimoni.
Eneo hilo la Kangaye ‘A’ linalosadikika kuwa na dhahabu lilizuiliwa kuchimbwa baada ya kubainika kwamba linahatarisha maisha.
No comments:
Post a Comment