Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

May 03, 2014

WATUMISHI WAMLAUMU MKURUGENZI WAO MEI MOSI.


.Sherehe ilipelekwa kijijini kwao lakini zawadi zikarudi mjini

                    Na Enhard Mwachiro Lugarawa

WATUMISHI na wafanyakazi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa katika mkoa wa Njombe waliopo vijijini wamemlalamikia mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa kutokutenda haki katika utoaji zawadi kwa wafanyakazi bora katika sherehe za mei mosi mwaka huu.

Hayo yamesemwa na wafanyakazi wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wafanyakazi (mei mosi) iliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Lugarawa tarafa ya Liganga ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Ludewa Juma Madaha.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wafanyakazi hao walisema sherehe hizi kiwilaya zimefanyika kama maigizo kwamba pamoja na changamoto walizonazo za kufanyakazi katika mazingira magumu wanakatishwa tamaa na mwajiri wao kutokana na kutoa zawadi na wafanyakazi bora kwa upendeleo.

‘’’’’ zaidi ya asilimia 80 ya wafanyakazi waliopata zawadi za ufanyakazi bora mwaka huu walitoka nao mjini kuja kufanya maigizo huku Lugarawa lakini mbaya zaidi wengine tumeshuhudia wakipata zawadi hizo kila mwaka kuna nini? Aliuza mwalimu mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe

Wamesema hakuna sababu ya kupeleka sherehe za mei mosi katika maeneo ya vijijini wakati wanaonufaika ni wafanyakazi wa mjini. ‘’’’’ tunamwomba mkurugenzi aache kutudhihaki kama siku nyingine afanye sherehe hizo karibu na watu wake anaopendelea kuwapa zawadi za ufanyakazi bora.’’’’ alilalamika muuguzi mmoja

Aidha katika risala yao kwa mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Ludewa wafanyakazi katika halmashauri hiyo wametaja shinikizo la damu kama chanzo cha vifo kwa watumishi wengi wilayani humo.

Akisoma risala ya wafanyakazi mbele ya mgeni rasmi katibu mkuu wa shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi wilaya ya Ludewa Joseph Mvanga alisema wafanyakazi wamekuwa wakipoteza maisha kwa magonjwa mbalimbali lakini kubwa ikiwa shinikizo la damu kutokana na kudai mafao yao bila mafanikio, kutopandishwa mishahara na vyeo.

Mvanga alisema mwajiri amekuwa na kiburi na kuvaa miwani ya mbao kama vile haoni matatizo ya watumishi wake huku akiziba masikio kwa pamba kama vile hasikii kelele na kilio cha watumishi wake jambo linalopelekea wafanyakazi kufa kwa mawazo na maisha magumu.

Akijibu risala hiyo mkuu wa wilaya ya Ludewa Juma Madaha aliwaondoa hofu watumishi na wafanyakazi katika halmashauri ya wilaya kwa kuwaambia kuwa madai yao yatashughulikiwa.

No comments: