May 03, 2014
MWEKAHAZINA, MGANGA KORTINI KWA WIZI NA UDANGANYIFU.
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wilayani Ludewa katika Mkoa wa Njombe imewafikisha mahakamani mwekahazina wa Halmashauri ya wilaya hiyo Godfrey Yesse Zimubiha pamoja na Dr Adamson Ndapisi mganga wa Hospitali ya wilaya na mratibu wa mfuko wa bima ya Afya kwa makosa mbali mbali ikiwemo wizi wakiwa watumishi wa umma, udanganyifu na kughushi nyaraka mbalimbali kwa nia ya kumdanganya mwajiri na kujipatia fedha.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Ludewa Fredrick Lukuna, mwendesha mashtaka wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Imani Mzizi alisema washtakiwa walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti ambapo mweka hazina Godfrey Zimubiha alitenda makosa ya wizi na kughushi juni 30 mwaka 2012 akiwa mtumishi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa kama mtunza hazina.
Mzizi aliiambia mahakama kuwa Godfrey Zimubiha anashtakiwa kwa makosa ya kughushi kwa kutengeneza nyaraka za uongo linaloangukia katika kifungu cha 333,335,(a) na 337 sura ya 16 kanuni ya adhabu huku kosa la wizi wa sh 734,000 likiangukia katika kifungu 270 sura ya 16 ya kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kusikilizwa kesi hiyo kwa hatua ya awali kwa sababu upelelezi katika kesi hiyo umekamilika. Nayehakimu wa mahakama hiyo Lukuna akitoa masharti ya dhamana alisema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa lakini akadai wadhamini wawili kwa dhamana ya shilingi m.3 na mali isiyohamishika, mshtakiwa aliachiwa kwa baada ya kutekeleza masharti ya dhamana.
Katika kesi nyingine mwendesha mashtaka Amani Nitume mzizi alimsomea mashtaka ya wizi wa jumla ya sh m. 3 Dr Adamson Ndapisi mganga wa hospitali ya wilaya ya Ludewa na mratibu wa Bima ya afya fedha ambayo anadaiwa kuendesha semina hewa kwa wajumbe hewa huki akitoa orodha ndefu ya wajumbe hewa na saini za kughushi.
Wakitoa ushahidi kwa nyakati tofauti mahakamani hapo Dr Camiro wa hospitali ya mission Lugarawa, Dr Peter Yakobo Msigwa wa hospitali ya mission Milo, Dr Amani Haule afisa tabibu katika hospitali ya wilaya ya Ludewa, Dr Frankson Mwambasanga mganga wa hospitali ya Ludewa, Wolfam Kiowi afisa tabibu zahanati ya Ligumbilo walikiri kumtambua mshtakiwa lakini wakakana kuhudhuria semina iliyodaiwa kuendesha na mshtakiwa.
Mashahidi hao walikana kupokea fedha kwa ajili ya kuhudhuria semina na kukataa kuzitambua saini zilizokuwa mbele ya majina yao.Zimubia amekuwa mtumishi wa sita wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa kufikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali akiongozwa na mwenyekiti wa Halmashsuri hiyo ya wilaya hiyo Matei Kongo, wengine ni pamoja na Afisa mtendji kata ya mlangali Makamba, Dr Adamson Ndapisi wa hospitali ya wilaya ya Ludewa,mwenyekiti wa kijiji cha kipangala Yohana Jankin Pill na Tito Haule afisa mtendaji wa kijiji cha Mavanga.
mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment