Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

March 10, 2014

ACHOMWA MOTO NA MAMA YAKE KWA KOSA LA KUSHIKA UJAUZITO

Bi Evodia Mgaya ambaye ni mama mzazi aliyemmwagia binti yake maji ya moto

Huyu ndiye Emma Ndelwa aliyemwagiwa maji ya moto na mama yake hapa akiwa katika hospitari ya wilaya ya Ludewa

Mkazi mmoja wa kitongoji cha Ngalawale kata ya Ludewa wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe Bi.Evodia Mgaya(48)anashikiliwa na jeshi la polisi wilayani humo kwa kosa la kumwagia maji ya moto na kumuunguza binti yake kwa kosa la kushika ujauzito.

Akifanya mahojiano binti huyo aliyechomwa moto anayetambulika kwa jina la Emma Ndelwa(19)alisema mkasa huo umempata machi 7mwaka huu majira ya saa 2 usiku ambapo mamayake mzazi alipommwagia maji hayo ya moto na kumsababishia kuungua maeneo ya usoni,kifuani na mgongoni.

Emma alisema chanzo kikubwa ni ujauzito ambao mpaka sasa unaumri wa miezi mitano licha ya kuwa yeye si mwanafunzi lakini amekuwa akipata manyanyaso kutoka kwa mama yake kila wakati ikiwa ni matusi na kupangiwa kazi ngumu za shamba bila ya huruma.

Alisema yeye ni mtoto wa 3 katika familia yenye watoto 10 siku hiyo alipangiwa kazi ya kupalilia mahindi na akimaliza akafyeke shamba kwaajili ya kulima maharage lakini akiwa na wadogo zake baada ya kumaliza kupalilia walijisikia kuchoka hivyo akaona amsaidie mamayake kugema uranzi na siku inayofuata amalizie kufyeka.

Anasimulia baada ya kutoka kugema uranzi aliwaogesha wadogo zake ndipo mama yake mzazi alipofika kutoka katika kilabu cha pombe za kienyeji na kuanza kuwatukana watoto wote na baadae kumwaga mboga iliyokuwa iko jikoni akaanza kummwagia maji ya baridi akaona haitoshi akachukua maji ya moto na kumwagia usoni.

“Alinikuta nimeshaogesha watoto napika nimekaa jikoni nikiwa napika mboga na nimetenga maji motoni kwaajili ya kuoga,akaanza nitukana mimi na wadogo zangu,baadae akamwaga mboga na akatoa maji ya kuoga jikoni akayapeleka nje yakiwa yanachemka,hapo alikua akinimwakia maji ya baridi akaona haitoshi akatoka nje ya jiko na kuchukua maji yale yamoto na kuniunguza nayo,”alisema Emma.

Emma alisema baada ya kumwagiwa maji hayo ya moto ghafla alijisikia maumivu makali ndipo alipoamua kuvua nguo zote na kukimbia kwenda kujificha katika shamba la mahindi akiwa na wadogo zake wakaamua kulala huko ili kuyanusuru maisha yao.

Anasema baada ya kufanyika tukio hilo siku ya pili mama huyo alimuomba msamaha kwa kusema alikuwa na hasira na kumtaka asiende kutibiwa hospitalini na badala yake alianza kumtibu kwa kutumia sukari na dawa za miti shamba,lakini hali ilikuwa mbaya ndipo wasamalia wema walipotoa taarifa katika uongozi wa kijiji.

Emma anaushukuru Uongozi wa kijiji cha Ludewa Kijijini kwa kufanya jitihada za kumchukua na kumfikisha katika kituo cha polisi wilayani Ludewa na hatimaye kuwahisha hospitali kwa matibabu zaidi.

Aidha kaimu mganga mkuu wa hospitari ya wilaya ya Ludewa Dkt.Leuben alithibitisha kumpokea mgonjwa huyo aliyeugunzwa kwa maji ya moto na anaendelea kupata matibabu ikiwa hali yake inaendelea vizuri.

Dkt. Alisema mgonjwa huyo alifikishwa hospitarini hapo jana majira ya saa 12 jioni akitokea katika kitongoji cha Ngalawale kata ya Ludewa mjini akiwa ni mjamzito wa umri wa miezi mitano lakini mpaka sasa anaendelea vizuri tofauti na alivyoletwa hospitarini hapo.

Mwisho.

No comments: