CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kupitia operesheni sangala kimebomoa Ngome ya Mbunge wa Rupa Victor
Mwambalaswa kwa kunyakuwa wanachama zaidi ya 9000 huku walio wengi wakiwa ni
wafuasi wa chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari
jana Wilayani humo Mkufunzi wa chama hicho kanda nyanda za juu kusini Christopher
Mwamsiku alisema kuwa katika operesheni ambayo wameifanya kwa wiki tatu hadi
kufikia jumatani ya wiki iliyopita tayari wamekusanya wanachama wapya 8000
kutoka jimboni kwa mbunge Mwambalaswa.
Mwamsiku alisema kuwa katika
operesheni hiyo wamezunguka katika vijiji vya na kujikusanyia wanachama wapya
kwenye mabano ni Kijiji cha Mpela kata ya Kambikatoto (68), Kambi katoto (108),
Bitimanyanga (260) kata ya Mafyeko (400), Isangambi (300), Matwiga (600),
Mtanila (140), Igangwe (200), na Luwalanje (150).
Aliongeza kuwa vijiji vingine ni
pamoja na Makongolosi (2000), Mwaoga (60) Matundasi (1200), Itewe (28) Mamba
(140) Upendo (300) Mamba A (130) na kubainisha kuwa taarifa zingine zilikuwa
bado hazijakamilika ili waweze kuzitoa kwa vyombo vya Habari.
Akizungumzia sababu za wananchi hao
kuhamia kwenye chama hicho Mwamsiku alisema kuwa hiyo inatokana na wananchi
kuchoshwa na manyanyaso wanayofanyiwa na serikali iliyopo madarakati hasa jamii
ya wafugaji ambao ndio wamekuwa chambo cha mapato kwa Halmashauri ya Chunya.
Alisema wananchi wengi wametua
shutuma zao kwa viongozi wa vijiji ambao wengi wao ni wanachama wa CCM ambao
wamekuwa wakiwatoza shilingi 200,000 za kitanzania ili waweze kuhamia vijiji
vingine wakitokea Mikoa ya Shinyanga, Tabora na maeneo ya Igunga.
Aliongeza kuwa jamii ya wafugaji
wameonekana kama vile sio watanzania tena bali ni kama wakimbizi na ndio maana
walipo waeleza haki zao waliweza kuitikia wito wakujiunga na chama ambacho
kinapigania haki za wananchi.
Alitoa mfano kuwa wabunge wa CCM
wamekuwepo katika jimbo la Rupa kwa miaka nenda rudi lakini wameshindwa
kuwajengea watoto shule ya sekondari katika kata ya Kambi katoto haina
hata shule moja ya sekondari huku ikiwa na shule ya msingi moja tu jambo ambalo
linasababisha watoto kutembea umbali wa kilomita zaidi ya 15.
Alisema kuwa kutokana na umbali huo
wananchi wamekuwa wakikata tama kuwapeleka watoto shuleni jambo ambalo
linasababisha kujikita zaidi kwenye ufagaji badala ya kujiendeleza na elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa msafara wa
operesheni hiyo Peter Edward alisema kuwa jimbo hilo limekuwa na idadi kubwa ya
watoto kutokana kuwepo shule chache hivyo kusababisha watoto wengi kujiingiza
kwenye machimbo ya dhahabu na kisha kuzaliana ovyo.
Edward alisema kuwa uongozi wa
Wilaya hiyo pamoja na Mbunge wao hawana huruma na makabira ya Wasukuma na
Wamang’ati ambao ndio wahanga kutokana na kuwatumia kama ndio vitega uchumi vya
halmashauri kutokana na kumiliki mifugo mingi hivyo kuiingizia Halmashauri pesa
nyingi.
Kiongozi
huyo wa msafara aliwataka viongozi hao kuwaheshimu wafugaji kwa kuwapa
haki zate stahiki kwa kuwa na wao ni sehemu ya wananchi wa Tanzania na
si kama wanavyofanyiwa kana kwamba wao hawana haki katika nchi yao.
MWISHO.
Na Ibrahim Yassin, Chunya
No comments:
Post a Comment