Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

September 30, 2013

AFUGA MBWA MIA MOJA KUSAIDIA UCHUNGAJI NGO'OMBE

 
KATIKA hali isiyo kuwa ya kawaida Mfugaji ambaye pia ni mchimbaji wa dhahabu katika kijiji cha Mlima Njiwa Wilayani Chunya Mkoani hapa Elias Mwembe amefuga Mbwa zaidi ya mia kwa ajili ya kuchunga Ng'ombe zake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kijijini hapo mfugaji huyo amesema kuwa lengo la kufuga Mbwa hao ni kupunguza kazi za binadamu katika kuchunga mifugo na badala yake kutumia Mbwa hao muda wote wa uchungaji mifugo.

Mwembe alisema huu ni wakati wa jamii kutambua kuwa hakuna sababu ya mwanadamu kuendelea kutumia muda wake katika kuchunga mifugo na kuacha kufanya shughuli za kimaendeleo badala yake kujikita zaidi kwenye poli jambo ambalo alisema sio la msingi.

Akifafanua namna Mbwa hao wanavyofanya kazi ya uchungaji Mwembe alisema kuwa kila ifikapo muda wa saa tatu asubuhi anawapatia chakula cha kutosha na kisha kuiongoza mifugo hiyo akiambatana na Mbwa wake eneo ambalo mifugo inakopaswa kupata malisho na kuiacha huko ikiwa mikononi mwa Mbwa hao.

Alisema kuwa mifugo hiyo hukaa huko huko ikiwa inapata malicho hadi majira ya saa kumi na moja (11:00) jioni na hatimaye kurejeshwa tena na mbwa hao hadi nyumbani kwake kijiji cha Mlima Njiwa.

Aidha alisema jambo la kufurahisha ni kwamba toka aanze kuwatumia Mbwa hao katika chunga mifugo ambayo ni pamoja na Ng’ombe, na Mbuzi, vyote vikiwa zaidi ya elfu moja hajawahi kupata taarifa za kuwepo kwa uharibifu wa vyakula vya wakulima.

“Nashukuru mungu kutokana na namna wanyama hawa wanavyonisaidia kuchunga Ng’ombe na Mbuzi kwani ndivyo vimenifanya niendelee kufanya kazi nyingine za kimaisha kama vile uchimbaji wa dhahabu ambao nilianza nao muda mlefu” alisema Mwembe.

 “Zamani nilikuwa Napata shida sana na kwamba hata watoto wangu walikuwa wanapata shida kutokana na kuhakikisha mifugo inapata malisho lakini wakati huo walikuwa wanakosa masuala mengine muhimu kama vile elimu na kadhalika kutokana na kujikita zaidi kwenye uchungaji wa mifugo lakini sasa kila mmoja watu yuko bize na mwasuala ya kimaendeleo na shule” aliongeza Mwembe.

Aidha mfanyabiashara huyo alisisitiza kuwa katika kipindi hiki, jamii inapaswa kuheshimu mawazo ya watu wengine aidha kwa kuyafanyia kazi na kuacha kuendeleza majungu na fitina zisizo na msingi kwa jamii.

Mwisho.
 Na Ibrahim Yassin,Chunya

No comments: