Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

August 24, 2013

MBOWE ASEMA TANZANIA KWANZA VYAMA BAADAE KATIKA MCHAKATO WA KATIBA MPYA




MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mh.Freeman Mbowe amewataka watanzania hususani wananchi wa wilaya ya Ludewa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele na kuacha ushabiki wa vyama vya siasa katika mchakato mzima wa uundwaji wa katiba mpya ya nchi ambayo itatumika na vizazi vijavyo vya nchi hii.

Hayo yalizungumzwa jana katika hotuba yake alipokuwa wilayani Ludewa mkoa wa Njombe katika moja ya mikutano ya katiba ya chama hicho ambapo aliwataka watanzania hususani wananchi wa wilaya ya Ludewa kujali zaidi maslahi ya Taifa kuliko kufuata ushabiki wa vyama vya siasa.

Mh.Mbowe alisema Tanzania iliumbwa kabla ya vyama vya siasa hivyo kama watanzania watashiriki kwa pamoja kuiunda katiba mpya yenye tija kwa kizazi cha sasa na cha baadae basi kizazi cha baadae kitasifu kazi hii ambayo hata Mwenyezi Mungu ataibariki.

Alisema suala la Serikali tatu halipingiki kwani Tume ya Warioba imeliona hilo hivyo anashangazwa na baadhi ya wanasiasa wanaopinga jambo hilo la kheri kwani matokeo ya kuzaliwa nchi ya Tanzania yalitokana na muungano wa nchi mbili ambazo ni Tanganyika na Zanzibar sasa inakuwaje Tanganyika haionekani na Zanzibar inaonekana.

Mh.Mbowe alikitupia lawama chana tawala CCM kwa kusambaza walaka kwa wanachama wa cha hicho kuwa wasikubari mfumo wa Serikali kutokana na kuhofia kuvunjika kwa muungano kwani Zanzibar wakati inaanzisha mamlaka yake na kuwa na Rais wake hawakuliona hilo na kama waliliona iweze upande wa Tanganyika wawe na hofu.

Ndugu zangu watanzania hususani wanaludewa katiba tunayoihangaikia sasa itakuwa ni ya watanzania wa kizazi cha sasa na cha baadae hivyo ni bora kuweka ushabiki wa vyama pembeni na kulitanguliza taifa mbele,inashangaza kuona baadhi ya wanasiasa wanapinga mambo ya msingi kwa lengo la kuingiza maslahi yao katika katiba mpya”,alisema Mh.Mbowe.

Nae Mbunge wa singida Mh.Tundu Lissu alisema ifikie wakati wananchi waelimishwe kuhusiana na mchakato mzima wa katiba na si kupandikizwa woga na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa katika uhuru wa kutoa maoni kwani mpaka sasa wananchi walio wengi wanatoa maoni yasiyo yao.

Mh.Lissu alisema anasikitika kuona viongozi wa chama cha Mapinduzi kuipinga rasimu ya katiba mpya iliyo andaliwa na Tume ya Mzee Warioba wakati katika tume hiyo wamejaa wanaCCM wenzao ambao waliwaamini na kuwapa kazi ya kuandaa mchakato huo na kwa busara za wazee walioko katika tume hiyo waliona mbali na kuiandaa rasimu nzuri lakini CCM wanaipinga.

Alisema haiwezekani Nchi moja ikawa na maamiri jeshi wawili yaani Rais wa Tanzania na Rais wa Zanziba harafu ikaitwa nchi moja,alisisitiza kuwepo na Serikali tatu pia wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wachaguliwe na wananchi ili waweze kuwajibishwa wanapokiuka utaratibu.

Kuhusu madaraka ya rais Mh.Lissu alisema ni lazima yapunguzwe kutokana na rais kuwa na madaraka makubwa ya kuteua kila mtu na ndio maana kumekuwa na utendaji mbovu kwa baadhi ya sekta kutokana na viongozi wengi kupewa madaraka kama zawadi.

Aidha alisisitiza suala la upatikanaji wa maji safi na salama liingizwe kwenye katiba kwani haiwezekani wananchi wanaoishi katika nchi yenye maji mengi wakakosa maji wakati kunamito mingi inayotiririsha maji lakini wananchi wanaoishi maeneo hayo hawana huduma hiyo.

Mh.Lissu aliwataka wananchi wilayani Ludewa kuacha uoga katika kuchangia maoni yao namna katiba wanayoitaka kwani walaka inaosabazwa na chama cha mapinduzi (CCM) uko kwa maslahi ya viongozi wa chama hicho na si kwa watanzania halisi.

MWISHO


No comments: