Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

July 11, 2013

WAZIRI MKUU AWAFUNDA WANALUDEWA



 Waziri mkuu akipata maelezo juu ya uandaaji wa kahawa

               waziri mkuu akiwa na mkewe mama Tunu Pinda pamoja na mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe akiwasili wilayani Ludewa

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh; Mizengo Pinda ameawataka wananchi wilayani Ludewa kuchangamkia fulsa katika miradi ya makaa ya mawe ya mchuchuma na chuma cha Liganga ili kunufaika wao kwanza kabla ya watu kutoka nje ya wilaya.

Waziri Pinda aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya mpira wa miguu Ludewa mjini katika mkoa wa Njombe katika ziara yake ya siku mbili wilayani humo alikokwenda kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kutembelea maeneo ya uwekezaji wa makaa ya mawe na chuma.

Alisema miradi hiyo miwili iko katika hatua nzuri kwani tayari wawekezaji wako katika hatua za mwisho na ifikapo mwaka 2014 kwa mujibu wa wawekezaji migodi hiyo itakuwa inaanza katika hatua ya uzalishaji wa chuma na umeme.

Kufuatia kuanza kwa machimbo hayo Pinda ameiagiza Halmashauri ya wilaya ya Ludewa kuwaandaa wananchi kwa kutoa elimu kuhusu kunufaika na fursa zitakazotokana na migodi hiyo mikubwa ambayo inatarajia kuzalisha megawati 600 za umeme na chuma.

”” bila maandalizi mazuri kwa wananchi wa Ludewa kuna hatari ya wao kugeuka kuwa watazamaji katika mali waliyoilinda kwa zaidi ya miaka 50 na hatimaye kuzua migogoro isiyo ya msingi hivyo Serikali lazima ihakikisha wananchi wanaandaliwa ipasavyo.’’’’ alisema waziri mkuu

Naiagiza Halmashauri ya wilaya kuwaandaa wananchi ili kwenda sambamba na miradi ya makaa ya mawe mchuchuma na chuma cha liganga ili waweze kunufaika na fulsa zilizopo kwani bila ya hilo miradi hiyo haitakuwa na faida kwao”,alisema waziri Pinda.
Alisema kazi ya Serikali kwa sasa ni kuhakikisha inajenga barabara ili kuweza kupitisha mitambo inayotakiwa katika migodi hiyo na kwamba tayari shilingi bilioni 7 za awali zimeshatengwa kwaajili ya kazi ya upanuzi wa barabara hiyo.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya lami kutoka Itoni, Ludewa hadi Manda Waziri Pinda alisema tayari Serikali imeshatenga fedha za upembuzi yakinifu hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kwani suala hilo halikwepeki kutokana na umuhimu wa uwepo wa miradi hiyo ya madini.

Katika sekta ya kilimo Pinda alisema jembe la mkono haliwezi kumaliza matatizo ya mkulima kinachotakiwa ni kuangalia uwezekano wa kuwakopesha wakulima matrekta ya bei nafuu ili kuwainua wakulima ikiwezekana hata kwa kuunda vikundi.

Waziri Pinda alisema Serikali anaandaa mazingira mazuri katika kuwawezesha wakulima pembejeo za kilimo kwa muda unaofaa ili waweze kunufaika na kilimo kwani kilimo cha mkono kimepitwa na wakati hivyo kama watatumia zana za kisasa kilimo kitakuwa ukombozi kwa wakulima.

Alisema wilaya ya Ludewa imejaliwa kuwa na Ardhi nzuri yenye rutuba hivyo wananchi waanzishe kilimo cha matunda,alizeti na mazao mengine ambayo ili kuweza kijipatia fedha zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Katika ziara yake wilayani Ludewa waziri Pinda kufanya uzinduzi wa kinu cha kukobolea kahawa katika kijiji cha Mawengi kata ya Mawengi na kuweka jiwe la msingi katika jengo la maabara shule ya sekondari ya chief Kidulile iliyoko kata ya Ludewa.

Aidha kuhusu tatizo la ukosefu wa maji safi na salama waziri Pinda alisema tayari Serikali imeshatenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa kuanzia kwani miundombinu ya awali imechoka hivyo fedha hiyo ni kwaajiri ya kurekebisha miundombinu.

Aliongeza kuwa uhaba wa maji katika mji wa Ludewa unasababishwa na ongezeko la idadi ya wakazi hata hivyo miundombinu ya maji iliyopo ni ya zamani wakati idadi ilikuwa ndogo lakini Serikali kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe wataangalia namna ya kulitatua tatizo hilo.

mwisho






No comments: