WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa amevitaka vyombo vya
dola na wafanyabiashara wakubwa nchini, kujenga mahusiano bora kati yao na
wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) ili kuondoa tabaka la matajiri na
masikini linaloweza kuathiri uchumi wa taifa.
Lowassa aliyasema
hayo jana wakati akizungumza na machinga wa eneo la Makoroboi jijini Mwanza,
ambao pamoja na mambo mengine aliwachangia sh milioni 20 kwa ajili ya kutunisha
mfuko wao.
Mwanasiasa huyo
ambaye pia ni mbunge wa Monduli, aliinyoshea kidole Serikali ya chama chake cha
Mapinduzi (CCM) na kuitaka ihakikishe inatekeleza kwa vitendo ilani yake
inayosisitiza wananchi kuwezeshwa kiuchumi ili kuondoa matabaka.
Huku akishangiliwa na
wafanyabiashara hao, Lowassa ambaye aliongozana na baadhi ya makada wa CCM
kutoka ndani na nje ya Mwanza, alisema kila mwananchi wa Tanzania lazima ale,
ingawa kwa namna tofauti.
Alisema kuwa ili
amani iwepo nchini, lazima Jeshi la Polisi na wafanyabiashara wakubwa
wawathamini wafanyabiashara wadogo.
“Tunataka tuwasaidie hawa vijana wetu, maana ni nguzo kubwa sana katika
maendeleo ya taifa. Ilani ya CCM inasema lazima watu wawezeshwe kiuchumi.
“Kwa maana hiyo katika nchi yetu kila mtu lazima ale. Na kula
kwenyewe tunatofautiana, huyu anakula mkate na huyu anakula hiki. Na ili amani
iwepo lazima RPC au OCD na wafanyabiashara wawathamini machinga,” alisema Lowassa.
Pia alitahadharisha
kuwa endapo wafanyabiashara hao wadogo watadharauliwa katika nchi, lazima
watakula sahani moja na matajiri.
Alitumia pia fursa
hiyo kukanusha tuhuma dhidi yake kwamba amejilimbikizia mali.
“Wapo baadhi ya watu wanasema hela ninazotoa hizi ni zangu. Mimi
sina fedha, ninazotoa ninapewa na marafiki zangu. Mimi si tajiri wa fedha, ila
ni tajiri wa marafiki na ushawishi ninao,” alitamba.
Katika hatua
nyingine, Lowassa alikataa kuulizwa maswali na wamachinga hao akisema ameandaa
kamati itakayoratibu harambee ya kuwachangia kwa lengo la kupata sh bilioni
moja.
“Kwa maandalizi ya harambee nitakayorudi tena kuifanya, na ili mjue
kwamba nipo makini natoa hundi ya sh milioni 10 na milioni 10 nyingine nitaitoa
leo hii,” alisema
Lowassa ambaye baadaye aliondoka kwa kutembea kwa miguu hadi Mwanza Hotel.
Chanzo - Tanzania
Daima
No comments:
Post a Comment