Madiwani wa halmashauri ya wilaya Ludewa wakiwa katika kikao
Afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Ludewa Bw.Wiliam Malima akijibu hoja
Baadhi ya wakuu wa Idara mbalimbali wakifuatilia kikao cha baraza la madiwani
Baraza la Madiwani katika
Halmashauri ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe limemtaka mkurugenzi
wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuwafuatilia wachimbaji wadogo na
wakubwa wa madini wilayani huo ili waweze kulipia ushuru kwa kazi
wanazozifanya.
Akizungumza katika kikao
cha baraza hilo jana mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa
Mh.Matei Kongo alisema kumekuwa na wachimbaji wengi wenye maeneo ya
madini wilayani humo wakifanya kazi zao lakini hakuna wanachokilipa
kwa Halmashauri.
Mh.Kongo alimtaka
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuwafuatilia wote wenye vitalu vya
madini wilayani humo bila kujali ni wachimbaji wakubwa au wadogo wa
ndani ya nchi au wanje ya nchi ili waweze kulipia kodi katika
halmashauri.
Alisema taarifa zinaonesha
kwa mwaka 2012 ni kampuni moja tu ya M.M.I LTD ndiyo iliweza kulipa
kiasi cha shilingi laki nne lakini kumekuwa na wamiliki zaidi ya 54
wa vitaru vya madini wasiotambua uwepo wa ofisi za halmashauri
kwaajili ya kulipia ushuru huo.
“Tunashangazwa na
kitendo cha wamiliki hawa wa vitaru kutolipa ushuru katika wilaya
yetu wakati wanatumia barabara zetu huko vijijini na zinapokuwa mbovu
ni Halmashauri pekee ndiyo inayowajibika kuzikarabati,hivyo
tunakuagiza mkurugenzi kuwafuatilia wachimbaji hawa na kuwadai ushuru
mara moja”,alisema Mh.Kongo.
Aidha mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo Bw.Wiliam Waziri aliahidi kuwafuatilia wawekezaji
hao katika ofisi zao ili kuweza kuzungumza nao namna ya ulipaji
ushuru huo ambapo kwa miaka mingi wamekuwa wakwepa kuilipa
Halmashauri hiyo.
Bw.Waziri alisema ofisi
yake ilikuwa katika mchakato huo na kufuatia maagizo hayo ya Baraza
la madiwani basi wamiliki wa vitaru hivyo watafuatiliwa na kuweza
kupata maelezo ni kwanini hukwepa kulipa ushuru kutokana na kazi
wanazozifanya wilayani hapo.
MKUU wa wilaya ya Ludewa
Bw.Juma Solomon Madaha aliwataka madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya
Ludewa kushirikiana kikamilifu na watendaji wa halmashauri hiyo ili
kuhakikisha ushuru huo unaisaidia halmashauri katika kukamilisha
miradi ya maendeleo
Alisema kuwa hakuna haja
ya madiwani kusubiri vikao vya baraza ili kuwakosoa watendaji na
badala yake ni kutoa ushirikiano kwa watendaji hao ili kuhakikisha
miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati uliopangwa ili kuifanya
wilaya hiyo kuwa na maendeleo haraka.
Bw.Madaha alisema njia
sahihi ya kuisaidia halmashauri hiyo kujiendesha ni lazima kubuni
vyanzo vya mapato ya ndani na si vinginevyo kwani kwa kubuni njia za
kuongeza mapato ya halmashauri kunaweza kusaidia kutatua matatizo
madogomadogo yanayojitokeza.
“kimsingi kuna vyanzo
vingi vya mapato wilayani hapa lakini hatuvitendei kazi kama vyanzo
hivyo vitafuatiliwa hasa wawekezaji wa migodi wakubwa na wachimbaji
wadogo wanapaswa kulipa ushuru katika Halmashauri yetu kwa kazi
wanazozifanya”,alisema Bw.Madaha.
Alisema kutokana na
shughuri za uchimbaji zinazofanywa na wachimbaji wadogo na makampuni
makubwa ni dhahiri wanatakiwa kuilipa halmashauri kodi kwani
wanatumia barabara zinazojengwa na Halmashauri hivyo si vyema kukwepa
kulipa ushuru.
Bw.Madaha aliwataka
madiwani na watendaji kushirikiana kimakilifu kwani hata yeye atakuwa
mstari wa mbele ili kuhakikisha Halmashauri inainuka kimapato zaidi
tofauti na wilaya nyingine.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment