Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

July 23, 2013

FILIKUNJOMBE ATOA PIKIPIKI 34 KWA MADIWANI LUDEWA


Katibu wa Mbunge Bw.Gowele akitoa maelekezo kwa madiwani hao
Katibu wa Mbunge Bw.Gowele akimkabidhi pikipiki diwani wa kata ya Ibumi Mh.Edward Haule









WAKATI serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ikitafakari na kutafuta namna ya kuwakopesha madiwani usafiri kama ilivyo kwa wabunge, mbunge wa Jimbo la Ludewa katika Mkoa wa Njombe Deo Filikunjombe ametoa jumla ya pikipiki mpya 34 kwa madiwani wote wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa bila kujali itikadi zao kisiasa ili kuwarahisishia kutoa huduma kwa wananchi jimboni mwake.

Filikunjombe ametoa pikipiki hizo kwa madiwani 25 wa majimbo miongoni mwao wawili ni kutoka vyama vya chadema na Nccr mageuzi na madiwani 9 wa viti maalum pamoja na mipira mitano mitano kwa kila diwani ili kuboresha michezo kwa kila kata pamoja na kuwafanya vijana kupenda michezo badala ya kujihusisha na ngono.

Akikabidhi pikipiki kwa madiwani hao mtendaji na katibu wa mbunge wa Ludewa Stanley Gowele alisema mbunge ametekeleza ahadi yake aliyowaahidi madiwani wake miaka miwili iliyopita kama njia ya kuwafikia wananchi kirahisi.

“” pikipiki hizi najua zitaongeza ajira kwa vijana, zitaingizia halmashauri mapato na mbali ya kuwarahisishia madiwani kufanyakazi zao pia zitawaingizia vipato wao wenyewe kwa kutokana na serikali kuruhusu bodaboda kubeba abilia.”” alisema Gowele

Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti madiwani hao walisema saa ya ukombozi ni sasa kwani jiografia mbaya ya wilaya ya Ludewa iliyojaa milima imekuwa ikiwapa wakati mgumu wa kuyafikia maeneo yao ya uwakilishi lakini kwa sasa pikipiki zitawarahisishia kufanyakazi zao.

Kwa upande wake diwani mkongwe kutoka kata ya Ibumi Edward Haule alisema kutekelezwa kwa ahadi ya mbunge kuwaletea madiwani usafiri wa pikipiki kutarahisha utendaji wa kazi na kuwafikia wananchi kwa wakati hasa ukilinganisha na jiografia ngumu ya miundombinu ya barabara wilayani Ludewa.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika Agost 2012 wilaya ya Ludewa inajumla ya wakazi 128,155 kati yao wanaume ni 60,477 na wanawake 67,678 wastani wa ongezeko la watu kwa mwaka ni 1.6% hadi kufikia 2012 na sasa wilaya ya Ludewa inakadiriwa kuwa na watu 152, 285 kati yao wanawake 79,318 na wanaume ni 72,968 ambapo kiutawala wilaya ya Ludewa imegawanyika katika tarafa 5 kata 25 vijiji vilivyoandikishwa 77 na vitongoji 340.

Wilaya ya Ludewa ina eneo la kilomita za mraba 8,397 kati ya hizo kilomita za mraba 73.54 ni hifadhi ya misitu, kilomita za mraba 2,072 ni maji na milima na kilomita 6,251.46 zinafaa kwa makazi ya watu na kilimo.

mwisho

No comments: