Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

May 18, 2013

WANANCHI WA KIJIJI CHA ILELA KATA YA RUHUHU WILAYANI LUDEWA WAWATIMUA MTENDAJI NA MWENYEKITI WA KIJIJI



Wananchi wa kijiji cha Ilele kata ya Ruhuhu wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe wamewasimamisha kazi mwenyekiti wa kijiji hicho pamoja na mtendaji kwa kile kinachodaiwa kushindwa kusimamia maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa Afisa mtendaji wa kata ya Ruhuhu Bw.Ashery Lufingo alisema maamuzi hayo ya wananchi yamefikia kutokana na viongozi hao wawili kushindwa kusimamia shughuri za maendeleo katika kijiji hicho.

Bw.Lufingo alisema Mey 5 mwaka huu katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na viongozi hao kwa lengo la kusoma mapato na matumizi ya kijiji hicho na baada ya kusoma taarifa ya kijiji wananchi hao waliipinga vikali taarifa hiyo na kuwatimua.

Akiwataja viongozi hao waliofukuzwa kazi na wananchi Bw.Lufingo alisema mwenyekiti wa kijiji anafahamika kwa jina la John Tendeka na mtendaji wa kijiji hicho anatambulika kwa jina la Esau Haule.

Tumepokea malalamiko kutoka kwa wananchi lakini wao ndio wenye uamuzi na mwenyekiti wao na kuhusiana na mtendaji nimeshapeleka taarifa katika ngazi husika na tuko katika kuchagua viongozi wa muda ili kijiji kiweze kuendelea na majukumu yake”,alisema Bw.Lufingo.

Alisema wananchi hao wamekasilishwa baada ya kuona baina ya viongozi hao kati ya mwenyekiti na mtendaji hawapatani na ndio sababu kuu ya kijiji hicho kufifia kimaendeleo kwa muda mrefu na hakuna suruhu ya viongozi hao wawili inayopatikana.

Aidha Diwani wa kata ya Ruhuhu Bw.Edwin Haule Spika alifafanua kuwa sababu ya viongozi hao kukataliwa na wananchi ni kushindwa kusimamia shughuri za maendeleo zikiwemo ufyatuaji wa tofari za ujenzi wa zahanati.
Bw.Spika alisema wananchi walijitolea nguvu zao katika ufyatuaji wa tofari hizo lakini chakushangaza zimeshindwa kuhifadhiwa vizuri na kufikia baadhi ya tofari kuharibiwa vibaya na mvua.

Alisema taarifa zimeshafika katika ngazi husika hivyo kinachofuata ni uchaguzi wa viongozi wa muda ili kijiji hicho kiweze kufanya kazi za maendeleo kama awali.

Aidha aliyekuwa mtendaji wa kijiji hicho Bw.Esau Haule alipohojiwa na waandishi wa habari alikili kuwepo kwa tukio la wao kukataliwa na wananchi lakini aliwalaumu wananchi kwa kushindwa kutekeleza kazi walizo kubaliana.

Bw.Haule alisema moja ya kazi walizokubaliana ni ukataji wa nyasi na kuyaezeka matanuli ya matofari hayo ili yasiharibiwe na mvua lakini wananchi hao walikaidi agizo hilo na kuikataa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji.

Alisema wao wameyapokea maamuzi hayo ya wananchi kwa mshtuko kwani hawakutegemea kutokana na utendaji wao wa kazi licha ya kutoa maagizo kwa wananchi ili kuleta ufanisi wa kijiji hicho katika maendeleo na kupingwa vikali.

Mwisho

No comments: