Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

May 04, 2013

WAFANYABIASHARA LUDEWA WAITOLEA MACHO HALMASHAURI.





Wafanyabiarasha Mjini Ludewa katika mkoa wa Njombe wameitaka Halmashauri ya wilaya hiyo kufanyakazi kwa uwazi, ukweli na kutenda haki kwa mujibu wa sheria katika kuandaa mikataba katika vibanda vya biashara vilivyoko stendi kuu na eneo la soko ili kila mtu ashiriki uendeshaji halmashauri kwa kulipa ada na ushuru bila kinyongo.

Kauli hiyo ya wafanyabiashara imekuja kufuatia halmashauri hiyo kupanga kodi na tozo mbalimbali ikiwemo kuandika mikataba ya vibanda hivyo vilivyojengwa na wafanyabisha bila kuwashirikisha.

Awali wafanyabiashara hao waliuziwa maeneo ya biashara na halmashauri ya wilaya kwa masharti kwamba wavijenga kwa gharama zao na ramani zao lakini baadaye halmashauri iliandika mkataba ukielekeza wafanyabiashara kuanza kulipia kodi baada ya miaka mitano bila kuwa shirikisha jambo ambalo lilipingwa vikali 

Sakata hilo lilitokea baada ya wafanyabiashara hao kupewa viwanja maeneo ya soko,kituo kikuu cha mabasi na viwanja vya michezo kwa gharama ya shilingi laki nne na kuamliwa kuvijenga haraka kwa gharama zao.

Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wafanya biashara na wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Afisa ardhi wa wilaya Isaack Makinda alisema viwanja hivyo ni mali ya Serikali hivyo mkataba unaonesha umiliki wa vizimba hivyo ungekoma baada ya miaka mitano.

Makinda alisema licha ya kuwepo kwa mkataba huo lakini katika hali ya kibinadamu Halmashauri ilifanya tathmini na kuona bado wafanya biashara wa maeneo ya soko hawajanufaika na vizimba hivyo hali ambayo iliwafanya wataalamu kuwaongezea muda wa umiliki.

“ni zaidi ya miaka kumi na zaidiimepita tokea mlipoongezewa muda lakini tumeona muda umeshafika wa kufunga mkataba lakini tunachokifanya sio kuwanyang’anya bali mnatakiwa kuomba upya kwani hata muda tuliowaachia ulipaji wa kodi ya mwaka imekuwa ni shida”,alisema Bw.Makinda.

Alisema cha kushangaza zaidi wafanyabiashara wamekuwa wakiuza vizimba hivyo kinyemela bila ya kutoa taarifa katika ofisi za halmashauri ya wilaya jambo ambalo linasababisha migogoro na ukwepaji wa ulipaji ushuru kila mwaka.

Mwanasheria wa ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa Joseph Kamonga alifafanua kuwa watu wengi bado hawaijui sheria ya ardhi hivyo wanatakiwa kuelimishwa ili waweze kutambua sheria ya ardhi katika nchi ya Tanzania.


Bw.Kamonga alisema hakuna raia anayeruhusiwa kumiliki maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa matumizi ya Serikali,hivyo kila mfanya biashara aliyejenga kizimba anapaswa kuupitia mkataba wake ili aweze kujirizisha nini kiliandikwa.

Alisema lengo la halmashauri ni kukusanya mapato katika vizimba hivyo lakini kwa muda mrefu sasa hakuna ushuru wowote unaotolewa na wamiliki wa vizimba hivyo wakati sheria ilikuwa ni kulipia shilingi elfu kumi na tano kwa mwaka hata hiyo hailipwi.

Bw.Kamonga aliwataka wafanyabiashara kufuata mkataba kama ulivyoonesha kuwa ifikapo miaka mitano kila anayemiliki kizimba anatakiwa kuomba katika halmashauri yake ili uamuzi uweze kutolewa kama mlipa ushuru mzuri hakuna matatizo ya kukubaliwa kumiliki kizimba hicho upya.

Aidha mwenyekiti wa wafanya biashara wilayani hapa Bw.Mwasanga alisema licha ya kuongezewa muda wa umiliki wa vizimba hivyo ambavyo wafanya biashara ndio waliovijenga viashara imekuwa ngumu katika baadhi ya maeneo hali ambayo imesababisha hasara kwa waliovijenga.

Bw.Mwasanga aliwalaumu wataalamu kwa tathmini walioifanya na kutaka kuvirejesha vizimba hivyo mikononi mwa halmashauri wakati bado waliotumia gharama zao katika ujenzi hawajanufaika navyo kutokana na uchache wa wakazi wa wilaya hiyo.
 
Alisema jambo la msingi ni kukubaliana na wafanya biashara katika suala la ulipaji ushuru na si kuwanyang’anya kwani wengine ndio wanakamilisha ujenzi sasa nab ado havijaanza kutumika licha ya kupewa viwanja hivyo kwa muda mrefu.

Nae Bw.Aurelian Mhagama mabaye ni mfanya biashara alipinga kauliuli ya wataalamu kusema wafanyabiashara hao waliingia mkataba na halmashauri kwani mkataba ni makubaliano ya pande mbili lakini halmashauri haikufanya hivyo.

Bw.Mhagama alisema wananchi walio wengi hawana uelewa kuhusiana na mkataba hali ambayo inawashangaza wananchi hao kwa kauli ya kutaka kunyang’anywa vizimba na kutakiwa kuomba upya wakati wao ndio wajenzi wa vizimba hivyo.

Alisema kutokana na kauli hiyo wananchi watashindwa kuendelea na vizimba vya kuzunguka uwanja wa mpira kwa kuhofia kunyang’anywa pindi watakapo maliza ujenzi huo na kuanza kuvifanyia kazi katika biashara.

Bw.Mhagama aliwataka wataalamu hao kupanga ushuru kwa mwaka na si kuwaeleza wafanyabiashara kupeleka maombi ya kuvimiliki upya wakati bado havijawapa faida wafanyabiashara hao.

Mwisho.

No comments: