Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

May 04, 2013

ACRA KUFUTA WASIOJUA KUSOMA, KUANDIKA NA KUHESABU LUDEWA.




SHIRIKA lisilo la kiserikali la kitaliano la ACRA linalofanya kazi wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe limefanikiwa kuwapeleka mafunzo ya muda mfupi walimu 52 kutoka katika shule za msingi na za awali 13 zilizopo katika kata za Mlangali, Mawengi Milo ili kwendana na wakati

Akizungumza jana katika warsha ya siku moja kwa maafisa elimu sekondari na msingi  wakiwemo wadau mbalimbali wa elimu meneja wa shirika hilo Beppe Buscaglia alisema madhumuni ya warsha ni kukutana na wadau wa elimu na kujadili kwa pamoja juu ya  mustakabali wa elimu na changamoto zake.

Beppe alisema shirika lake limefanya mambo mengi wilayani Ludewa ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa madarasa na nyumba za walimu kutokana na shule nyingine kuwa na vyumba vya madarasa ambavyo ama ni vibovu au vimechakaa.

Buscaglia akaongeza kuwa matokeo na mafanikio ya shirika la acra kuwagharimia mafunzo walimu kupitia chuo cha uwalimu cha Kreruu cha mjini Iringa kumeleta ufanisi mkubwa kwa walimu hao ikiwa ni pamoja na ongezeko la ufaulu na mahudhurio mazuri kwa wanafunzi.

Naye Robert Hyera afisa elimu msingi wilaya ya Ludewa aliyealikwa kama mgeni rasmi, akifungua warsha hiyo alikiri kuwepo kwa wimbi la walimu waliokaa zaidi ya miaka kumi  tangu kuhitimu vyuoni ambao hadi sasa hawajawahi kupata mafunzo wala semina yoyote jambo ambalo limekuwa likididimiza elimu kwa sababu walimu hawaendi na wakati.

 “”” walimu wanahitaji kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kwenda na wakati tena sambamba na mitaala lakini pamoja na kuyakabili mabadiliko yanayokea kila siku katikasekta ya elimu nchini.’’’’’ Alishauri Hyera

Aidha Bw Hyera alilisifu na kulipongeza shirika la acra kwa kugundua mapungufu hayo ambayo kimsingi kutokumwendeleza mwalimu ni kumdidimiza mwanafunzi kielimu na kwamba kama serikali itaiga mfumo huo basi itakuwa imeondoa na kufuta kabisa kuwepo kwa watoto wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu. 

“’’’’ tumekuwa na matatizo katika idara ya elimu kutokana na bajeti finyu ambayo imepelekea kudorora kwa elimu kwani walimu walio wengi hawapati mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha ujuzi na taaluma zao jambo ambalo linasababisha matokeo mabovu kwa wanafunzi”,akaongeza Bw.Hyera.

Katika mradi huo walimu wawili wa madarasa ya awali kutoa Ulayasi na Mlangali ambao wanajitolewa pasipo kuajiriwa serikalini walipata mafunzo ya miezi mitatu katika chuo cha ualimu Kreluu walipata mafunzo ya miezi mitatu na kuona mabadiliko makubwa.

Kwa upande wao walimu Tulamvona Mturo wa shule ya msingi mlangali na  Imelda Cassian Mtweve mwalimu wa shule ya awali ulayasi ambaye analipwa na jamii alisema mafunzohayo yamemsaidia na kumwongezea maarifa sana.

‘’’’’ kabla ya kupata mafunzo alikuwa akiingia darasani na kuanza kufundisha moja kwa moja bila ya kuwapa wanafunzi muda wa kucheza. Lakini kupitia mafunzo niliyoyapata nimeweza kuelewa saikolojia ya watoto na imekuwa rahisi kulimudu darasa kutokana na kuzitambua tabia tofauti za wanafunzi anaowafundisha.

 “Natumia zana za kufundishia na kujifunzia pia nafurahia ufundishaji wangu wa sasa kuliko zamani kwani awali sikujua jinsi ya kumudu na kupanga ufundishaji wangu,nilitumia jitihada nyingi kufundisha lakini wanaojiunga darasa la kwanza takribani nusu yao walikuwa hawajui kusoma na kuandika”,alisema mwalimu Mtweve

Alisema wanafunzi walikuwa wanachoka mapema kutokana kutokujua mpangilio wa ufundishaji hali ambayo ilipelekea wanafunzi karibia nusu ya darasa kutokujua kusoma na kuandika pindi waingiapo darasa la kwanza.

Nae Afisa maendeleo ya jamii wa shirika la ACRA Bi.Neema Lazaro alisema licha ya ujenzi na mafunzo yanayotolewa na shirika lake pia wanatoa vitabu vya masomo ya hisabati na kiingereza katika shule za msingi za kata ya Milo,Mlangali na Mawengi.

Bi.Neema alisema pia baadhi ya madarasa ya awali katika kata hizo wametoa vifaa vya kuchezea watoto na kuchora michoro katika kuta za madarasa hayo ambapo picha hizo husaidia watoto kutambua vitu mbalimbali.

Mwisho.

No comments: