Serikali imesema itaanza ujenzi wa minara ya simu katika maeneo
ya Wilaya ya Ludewa yasiyofikiwa na huduma za mawasiliano ya simu kwa
mwaka huu wa fedha 2013/14.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana
na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga wakati
akijibu swali la Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM).
Katika swali lake, Filikunjombe alitaka kujua mpango wa Serikali
kujenga minara ya simu eneo la mwambao wa Ziwa Nyasa na Milimani.
Filikunjombe alisema wananchi wanalazimika kupanda juu ya miti kupata
mawasiliano.
Waziri Kitwanga alisema ujenzi wa minara hiyo
utagharimiwa kupitia fedha za Benki ya Dunia (WB), zabuni ya kwanza
itatangazwa Mei mwaka huu.
Alivitaja vijiji ambavyo havina
mawasiliano kuwa ni Chanjale, Lumbila, Nkanda, vijiji vya Kata ya
Madilu, Lupingu, Ntumbati, Nindi, vijiji vya Kata za Kilondo, Makonde na
Madope.
“Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF)
inaendelea na jitihada zake kuhakikisha maeneo yote nchini hususan
vijijini yanapata huduma za mawasiliano ya simu,” alisema Kitwanga.
Naibu waziri huyo alisema lengo ni kuhakikisha maeneo yasiyofikiwa na
watoa huduma yanafikiwa kwa kutumia mbinu mbalimbali, ikiwamo ruzuku
inayotolewa na UCAF kushawishi kampuni za simu kupeleka mawasiliano
maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment