ASKARI Polisi wa
Kituo cha Tarime mkoani Mara mwenye namba D. 4662 Koplo Mathew, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za uzembe uliosababisha
kifo kwa risasi cha mwanafunzi wa darasa la kwanza wa shule ya Msingi Rebu,
Deus Jacob (9).
Kifo hicho kilitokea
wakati polisi wakiwa kwenye harakati za kukamata mtuhumiwa, Marwa Bisara, mkazi
wa kitongoji cha Songambele kata ya Sabasaba mjini hapa, aliyekuwa akituhumiwa
kwa shambulio na kudhuru mwili.
Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea
juzi saa 10 jioni katika kitongoji cha Songambele, baada ya Koplo Mathew na
askari wenzake wakiwa na mlalamikaji, wakifuatilia mtuhumiwa na kumkuta na
wenzake katika pagala wakivuta bangi.
Wakati polisi
wakijiandaa kumkamata, mtuhumiwa Bisara alimvamia Koplo Mathew akitaka
kumnyang'anya bunduki na katika purukushani hiyo,
risasi zilifyatuka na moja kumpata Deus kichwani na kumuua papo hapo baada ya
kichwa kufumuka.
Kamanda Kamugisha
alisema chanzo cha mauaji ni mtuhumiwa Bisara kukaidi amri ya kukamatwa. Lakini
mwenzake Julius Maseke (38) mkazi wa mtaa wa Ronsoti alikamatwa akiwa na
misokoto 47 na kilo 3.25 za bangi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati
wowote.
Polisi ilitoa mwito
kwa raia wema kutoa taarifa kwa vyombo husika watakapomwona Bisara na
inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mkuu wa Wilaya ya
Tarime, John Henjewele alionya wanasiasa waache kulitumia tukio hilo kisiasa
kwa kuwa marehemu Deus hakuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.
Alionya hivyo kwa
alichokisema ni baadhi ya wafuasi wa Chadema
kuchocheana kufanya vurugu wakihamasishana kuchukua mwili wa marehemu huyo na
kufanya maandamano kwenda Bomani ziliko ofisi za Mkuu wa Wilaya na Kituo cha
Polisi.
Hata hivyo, maandamano hayo yalizimwa na Polisi kwa kutumia
mabomu ya kutoa machozi na mwili huo uko katika mochari ya hospitali ya wilaya na
unatarajiwa kuzikwa leo
No comments:
Post a Comment