Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

April 22, 2013

TAKUKURU YABAINI RUSHWA IDARA YA MAJI LUDEWA, DC ATOA MIEZI SITA WAJISAFISHE.



Mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Juma Solomon Madaha akifungua warsha ya rushwa katika idara ya maji iliyoandaliwa na taasisi ya TAKUKURU wilaya ya Ludewa
Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Ludewa Bw.Edings Mwakambonja akitoa taarifa ya utafiti wa taasisi hiyo kuhusiana na rushwa katika idara ya maji
Muhandisi wa idara ya maji wilaya ya Ludewa Bw.Munge akifafanua jambo kuhusiana na utendaji wa idara yake
Kaimu muhandisi wa maji wilaya Bw.Theodori Mfuse akifuatilia warsha hiyo
Viongozi mbalimbali wakifuatilia kwa makini maelezo ya maafisa wa TAKUKURU
Afisa wa TAKUKURU Bw.Chihongaki akiwa makini kusikiliza maoni ya wadau katika suala zima la rushwa idara ya maji
kushoto ni mmoja wa mafundi wa idara ya maji Ludewa Bw.Abiudi akifuatilia warsha hiyo.

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe imebaini uozo na vitendo vya rushwa, ukiukwaji wa maadili na uvunjaji sheria  katika idara ya maji wilayani Ludewa kwa kutoa huduma za maji kwa upendeleo kwa manufaa binafsi jambo lililomuudhi mkuu wa wilaya hiyo.

Hayo yamebainika jana katika taarifa ya utafiti wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (takukuru) wilaya ya Ludewa kwa wenyeviti wa vitongoji na wadau mbalimbali, wateja na watumiaji wa maji katika mji wa Ludewa juu ya mianya ya rushwa katika utoaji wa huduma ya maji mjini Ludewa.

Akitoa taarifa kwa mkuu wa wilaya ya Ludewa Juma Madaha katika warsha ya siku moja kwa wenyeviti wa vitongoji na wadau mbalimbali wa maji, Kamanda wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Ludewa Edings Mwakambonja alisema ofisi yake imefanya utafiti wa kina na kubaini mianya ya rushwa katika utoaji wa huduma za maji katika mji wa Ludewa.

Mwakambonja akamwambia mgeni rasmi kuwa utafiti wake umefanywa kwa kuzungumza na wadau zaidi ya 46 kutoka makundi mbalimbali akiwemo mkuu wa wilaya, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Ludewa, mhandisi ma maji wilaya, meneja wa mamlaka ya maji mjini, na diwani wa kata ya Ludewa.

Wengine ni wananchi 30, wenyeviti wa vitongoji 8,afisa kata 1 maafisa vijiji 2 mwenyekiti wa kijiji 1na kwamba matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa hakuna usawa katika ugawaji maji katika vitongoji vilivyopo kinyume na sheria ya raslimali maji na 11/2009 kifungu namba 4 isemayo kuhamasisha upatikanaji sawa wa maji na dhana kuwa maji ni muhimu kwa maisha ya binadamu na kwamba maji safi ya kunywa ni haki ya kila mtu.

’’’’’ matokeo ya utafiti ni kwamba watumishi wamekuwa wakiomba hongo kwa wananchi wanapofanyakazi katika maeneo yao, idara ya maji kutoa bili za maji kwa wateja wake hata kama hawakupata maji kwa mujibu wa bili, kuwepo kwa miundombinu mibovu ya maji,kuwepo kwa upendeleona kutojulikana mafundi walioko kwenye zone.’’’’’’ Akataarifu mwakambonja.

Hata hivyo mwakambonja alimjulisha mkuu wa wilaya kuwa utafiti wake unaonesha kuwa mamlaka ya maji haina bodi tangu mwaka 2008 jambo linalosababisha utawala hafifu katika kusimamia huduma ya maji,maji yanayotumika na wananchi siyo safi wala salama kwa sababu yanatoka moja kwenye chanzo bila kutibiwa.

Naye Mkuu wa wilaya ya Ludewa Juma Madaha ambaye alikuwa mgeni rasmi katika warsha ameitaka idara ya maji Ludewa kuacha tabia ya kuomba na kupokea rushwa kwa wananchi wanaotumia huduma hiyo muhimu vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

 Madaha alisema wananchi wanailalamikia idara ya maji kwa kuomba rushwa ili kutoa upendeleo wa ugawaji huduma hiyo muhimu jambo ambalo ni kinyume na sheria na madili ya kazi.

Aidha amewataka watumishi katika idara hiyo kujisafisha haraka kwa kutoa haki sawa katika ugawaji na utoaji  wa huduma ya maji mjini Ludewa kwa kufuata misingi ya utawala bora.

‘’’’’’ natoa muda wa miezi sita kwa idara ya maji kitengo cha mamlaka ya maji mjini kuacha mara moja kujihusisha na vitendo vya rushwa na badala yake kufanyakazi kwa mujibu wa maadili na sheria za nchi sanjari na kurekebisha miundombinu na kufanyiakazi taarifa ya takukuru na wenyeviti wa vitongoji"alisema Bw.Madaha.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wilayani Ludewa inafanya tafiti katika idara mbalimbali za umma ili kujiridhisha na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahili kwa sababu ni haki yao ya msingi. 

  mwisho
Na Bazil Makungu,Ludewa

No comments: