Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

April 06, 2013

SEKONDARI IKOVO YAKOSA VYOO WANAFUNZI, WALIMU WAJISITIRI POLINI.





WALIMU na Wanafunzi wa shule ya sekondari Ikovo iliyoko kata ya Ludende wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe wako hatarini kupata magonjwa ya mlipuko kutokana na shule hiyo kukosa vyoo na maji zaidi ya miezi sita sasa.

Aidha zaidi ya walimu 13 na  wanafunzi 200 wanalazimika kujisaidia polini kutokana na shule hiyo kutokuwa na vyoo kwa muda mrefu kwa kile kinachodaiwa halmashauri ya wilaya kuitelekeza shule kwa muda mrefu na kupelekea shule hiyo kukumbwa na tatizo kubwa la kutokuwa na vyoo kwa wanafunzi.

Akizungumza na gazeti hili afisa Mkaguzi wa shule wilayani Ludewa Florian Mvanginyi alikiri kufanya ukaguzi shuleni hapo na kusema kimsingi shule ya sekondari Ikovo kwa sasa haina sifa ya kuendelea kutoa huduma kwa sababu ni chafu haifai na pia mazingira ya shule hatakiwi kuishi binadamu.

“” tumetoa maelekezo kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa, uongozi wa shule na Kata ya Ludende ilipo shule hiyo kuwa ofisi ya ukaguzi itafunga shule hiyo ifikapo Aprili 12 mwaka huu kama vyoo vitakuwa havijakamilika kwa sababu kuiacha shule na wanafunzi kuendelea kuwepo shuleni hapo ni hatari sana kwa afya zao.”Alisema Bw. Mvanginyi

Bw.Mvanginyi alisema uhitaji wa vyoo katika shule hiyo ni matundu 12 ya vyoo ambapo kati ya hayo matundu saba ni kwa ajili ya wasichana, matundu matatu kwa ajili ya wanafunzi wa kiume wakati matundu mawili ni kwa ajili ya walimu wa shule hiyo.

Akazitaja changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa maji na nyumba za walimu ambapo shule hiyo ina jumla ya walimu 13 lakini shule ina nyumba 3 kwa hiyo walimu wanalazimika kuishi zaidi ya wawili katika nyumba moja.

Naye Makamu wa Mkuu wa shule hiyo mwalimu Simoni Mwangalo Akizungumza jana  alisema tatizo hilo lilisha wasilishwa katika ngazi ya wilaya lakini hakuna juhudi zozote zilizochukuliwa ili kuwanusuru wanafunzi hao.

Mwalimu Mwangalo alisema kuwa shule hiyo ambayo iliyoanzishwa mwaka 2007 imekumbwa na changamoto nyingi zikiwemo za ukosefu wa matundu ya vyoo,ukosefu wa maji safi na salama na kutokuwa na nyumba za walimu ambapo mpaka sasa shule hiyo ina jumla ya nyumba za walimu tatu ambazo wanaishi walimu 13. 

Hata hivyo wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Ikovo wanaoishi hostel wanalazimika kulala chini kutokana na ukosefu wa vitanda 48 shuleni hapo  jambo linalohatarisha usalama wa  afya za wananfunzi shuleni hapo.

Aidha dada mkuu wa shule hiyo Joverida Tibenda alisema kumekuwa na tatizo kubwa kwa wanafunzi wakike wanaoishi hostel hasa suala la maji kwa wanalazimika kuyatumia maji ya mferejini kwa kunywa.

Alisema kwa wale wanaoyatumia maji hayo wakiwemo walimu kwa matumizi ya kuoga huotwa na vipele vingi kutokana namaji hayo kutokuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Joverida alisema kutokana na mateso hayo kwa wanafunzi wanaoishi hostel baadhi ya wanafunzi wamelazimika kuhama na wengine kuacha masomo kabisa.

 mwisho

No comments: