Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

March 30, 2013

RAIS KIKWETE AELEZA KUHUZUNISHWA KWAKE NA MAAFA YA KUPOROMOKA KWA JENGO LA GHOROFA 16








                                      Rais Jakaya Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mchana wa jana, Ijumaa, Machi 29, 2013, ametembelea jengo  lililoporomoka na kusababisha vifo vya watu na majeruhi kwenye Mtaaa wa Indira Gandhi/Morogoro mjini Dar es Salaam na amesikitishwa na kuhuzunishwa na maafa yaliyotokana na kuporomoka kwa jengo hilo.

Rais Kikwete anawapa pole nyingi wafiwa, anawapa pole nyingi walioumia na wanaoendelea kupatiwa matibabu baada ya kubanwa katika kifusi, wakiwamo watoto wadogo ambao walikuwa wanacheza chini ya jengo hilo la ghorofa 16 wakati lilipoporomoka asubuhi ya jana huku likiendelea kujengwa.
Rais Kikwete amewapongeza na kuwashukuru wananchi wote walioshiriki na wanaendelea kushiriki katika zoezi la uokoaji pamoja na vyombo na taasisi za umma na Serikali zinazoshiriki katika zoezi na kazi hiyo ya uokoaji.

Amewataka waendelee na jitihada hizo ili kama kuna watu ambao bado wamebanwa kwenye kifusi waweze kuokolewa ili wapatiwe matibabu, na kama watakuwa wamepoteza maisha basi miili yao ipatikane na iweze kupewa mazishi ya heshima yanayostahili mwanadamu.

Wakati alipotembelea eneo la tukio hilo, Rais Kikwete ametoa maelekezo mahsusi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mheshimiwa Saidi Mecky Sadik pamoja na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova.

Rais amewataka kuhakikisha kuwa Mjenzi wa jengo hilo ambaye ndiye anakuwa anajenga jengo hilo, Mhandisi Mshauri aliyekuwa anasimamia ujenzi wa jengo hilo, Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam  ambaye alitoa kibali cha ujenzi na ndiye Mkaguzi wa ujenzi pamoja na mwenye Jengo wanapatikana haraka na kuwajibishwa ipasavyo.

Aidha, Rais Kikwete amezitaka taasisi za kitaaluma zinazohusina na shughuli za ujenzi – Wachoraji Majengo, Wakadiriaji Majengo, Wajenzi, Wakandarasi na Wahandisi nazo zichunguze tukio hilo kwa haraka na kwa karibu, ili zibaini yapi yalikuwa ni matatizo na zichukue hatua kwa mujibu madaraka na mamlaka ya taasisi hizo kwa sababu zinayo madaraka na mamlaka hayo.

Rais pia amesema kuwa wakati umefika kwa taasisi hizo sasa kujihusisha kwa karibu zaidi na matatizo yanayojitokeza katika shughuli za ujenzi kwa sababu kila yanapoporoka majengo inakuwa heshima mbaya kwa taasisi hizo. 

Hivyo ni muhimu kwa taasisi hizo kufanya uchunguzi wa kubaini nini chanzo cha kila tukio kuanzia na lile la jana – kama ilikuwa ni udhaifu katika uchoraji, kama ilikuwa ni udhaifu katika ukandarasi, kama ilikuwa udhaifu na Ushauri ili hatua stahiki zichukuliwe.

No comments: