Mkuu wa mkoa Said Meck Sadick akiwa na Rais
Kikwete na Kamanda wa polisi kanda maalum Dar es salaam Suleiman Kova
Jengo lililoporomoka
Watu 40 wahofiwa kufukiwa baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka Dar
Watu zaidi
ya 40 wanahofiwa kufukiwa na kifusi baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa
linajengwa kuporomoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam jana asubuhi.
Kuporomoka kwa ghorofa hilo
lililokuwa katika Mtaa wa Indira Gandhi, kulizua huzuni, taharuki na simanzi
kwa ndugu na jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini
kimetokea.
Shughuli mbalimbali katikati ya jiji
hilo zilisimama kwa siku nzima baada ya jengo hilo kuanguka na kusababisha vifo
vya watu watano, 13 kuokolewa huku zaidi ya watu 40 wakisadikiwa kufukiwa na
kifusi cha udongo wa jengo hilo.
Jengo hilo lililokuwa likijengwa
mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na
Kampuni ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi
wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe
wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Pamoja na vifo na wengine
kujeruhiwa, magari takribani manne yalifunikwa na kifusi cha jengo hilo na
kupondwa pondwa na kuwa kama chapati.
Katibu wa Msikiti wa huo wa Shia
Ithnasheri, Mushtaq Damji alisema: “Leo tulikuwa na kitu kama jumuiya kwa jamii
ya wahindu, tulipanga kusherehekea lakini yote yakafutika.
“Baada ya swala ya alfajiri, watu
walikuwa wanazungumza hapa na pale na baada ya kupambazuka, watoto walikuwa
wanacheza mpira, walikuwa 9. Sasa, bahati nzuri watoto saba wakakimbia na
watoto wawili wakawa wamekwama,” alisema Damji.
Naye Mlinzi wa Msikiti huo, Athuman
Nassor alisema: “Mimi nafanya kazi ya ulinzi hapa msikitini, lakini nilikuwa
ninashangaa kiasi cha saruji kilichokuwa kikitumika kukorogea zege, kweli
walikuwa wanazidisha mchanga.
“Niliwahi kuwaambia hata hawa
vibarua, kuwa hii inayofanyika mbona siyo…,” alisema mlinzi huyo. Alisema; jana
ilikuwa siku ya kumwaga zege ghorofa ya 16 na kulikuwa na vibarua wapatao 50
ambao kila mmoja alikuwa na ndoo yake tayari kuanza kazi kabla ya ghorofa hilo
kuporomoka.
Mlinzi huyo alisema kuwa wakati
tukio hilo linatokea alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio na kusema kuwa bila
shaka baadhi ya kinamama lishe ni miongoni mwa waliofukiwa.
No comments:
Post a Comment