Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

March 20, 2013

LUDEWA YAKOSA MAJI, MAFUNDI WA IDARA WATAJWA KUHUJUMU MIUNDOMBINU.



                

WANANCHI wa kata ya Ludewa katika Mkoa wa Njombe wameilalamikia idara ya maji kwa kutofanya kazi walioajiriwa na badala yake wameanza kufanya hujuma kwa kuziba mabomba na kuharibu miundombinu kwa nia ya kuwashinikiza wateja kuwalipa fedha nje ya mishahara yao imefahamika.

Wakizungumza na gazeti hili jana walisema tatizo la maji katika kata ya Ludewa ni la muda mrefu  lakini serikali imefumba macho na kuziba masikio utadhani haioni wala haisikii kelele za wananchi kuhusu uhaba wa huduma hii muhimu kwa binadamu.

Cathberti Haule, Benitho Mgimba ni wakazi wa mtaa wa kanisa wao wakaenda mbali zaidi na kusema katika maisha yao hawajawahi kuyaona maji katika maeneo yao kwa hiyo wameshakata tamaa kwa sababu septemba mwaka jana waliahidiwa kupata maji lakini hakuna hata dalili ingawa waliambiwa wachimbe mtaro.

‘’’’ septemba mwaka jana uongozi wa kata ulituagiza tuchimbe mtalo kwa ajili ya kuweka bomba tukafanya hivyo na kupoteza nguvu zetu lakini kumbe ilikuwa danganya toto hadi leo hakuna maji, kuna wakati alikuja diwani na mhandisi mtaani kwetu wakaishia kutoelewana wao na mpaka leo hakuna ufumbuzi twende wapi?’’’’’ aliuliza Benitho kwa masikitiko.

Kufuatia sakata hilo gazeti hili likaonana uso kwa uso na meneja wa mamlaka ya maji mjini Ludewa ofisini kwake Bw Teodori Mfuse lakini baada ya kumweleza tatizo la maji akakataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba alikuwa na kazi nyingi ya kupeleleka ripoti kwa mkurugenzi wake.

‘’’’’ Karibuni lakini kwa sasa sina muda wala nafasi ya kuzungumzia hayo nina shughuli nyingi hapa ofisini mwende kwanza nikipata nafasi nitawapigia simu.’’’’ Alizungumza Bw Mfuse huku akionesha wazi kuwa suala la maji mjini ni kero na limemshinda.

Nao wananchi wa mtaa wa mkondachi katika kijijicha Ludewa(m) wamewalalamikia watumishi wa idara ya maji kwa kufanya hujuma kwenye mabomba na miundombinu yake kwa kuingiza vijiti na magunzi kwenye mabomba na wanapoitwa hutaka kulipwa kwanza fedha ndipo waende kutoa huduma hiyo.

‘’’’’msimu wa jua yaani kiangazi idara ya maji ilikuwa ikitoa taarifa kuwa kutokana na jua kali vyanzo vya maji vimepungua hivyo wananchi watarajie neema ya maji msimu wa mvua lakini hali imekuwa ni tofauti na ripoti yao mbona mvua zinavyesha lakini hakuna maji? Aliuliza mkazi wa Mkondachi kwa masharti ya kutoandikwa jina lake.

Aidha wananchi hao wamelalamikia mamlaka ya maji mjini kutokuwa na usimamizi mzuri katika mgao wa maji hayo kutokana na baadhi ya wananchi wenye nacho kupata maji muda wote na wasionacho kuyakosa kabisa kutokana na urasimu wa baadhi ya mafundi wa mamlaka hiyo.

Hata baadhi ya mitaa ambayo ilikuwa ikipata maji msimu wa kiangazi kama mitaa ya Mkondachi,Majengo mapya na Ibani kwa sasa imeingia katika mkumbo huo wa kukosa maji safi nasalama kama ilivyo mitaa ya kanisa,kimbila na kiyombo.

Wananchi hao waliilalamikia Idara hiyo ya maji kwa kile kinachodaiwa kulipishwa bili za maji kwa kila mwezi pasipo kuipata huduma hiyo licha ya kuwa kuna baadhi ya watu wanaendelea kuipata huduma hiyo bila matatizo yoyote.

Hali hiyo imekuwa ikitokea mara kwa mara na kuwafanya mafundi hao kuendelea kunufaika na mradi huo wa kuitwa kuzibua kwa kutoa vipande vya miti vilivyochomekwa ndani ya mabomba kwa kulipwa posho na mwanacnhi anayeitaka huduma hiyo.

“Tumechoshwa na adha hii ya kutopata maji katika misimu yote ya mwaka,kwani tunashuhudia kinachoendelea kama hujuma kwa baadhi ya mafundi wa idara ya maji kwa wananchi,kumekuwa na baadhi ya mafundi hutuzibia maji ili tunapowaita tutoe kidogodogo”,alisema mwananchi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Akijibu malalamko hayo Kaimu Mhandisi wa maji wilaya ya Ludewa Athanasio Munge alikiri kuwapo kwa taarifa na kero ya baadhi ya watumishi wake kufuatia malalamiko aliyoyapata kutoka katika baadhi ya ofisi na wananchi wakiilalamikia ofisi yake  kuwa na wafanyakazi wasio waadirifu na kwamba amewaita mara nyingi kuwaonya lakini anashangaa kusikia tatizo hili kuendelea.

Monika Mchiro diwani wa kata ya Ludewa kwa upande wake alipotakiwa na gazeti hili juu ya hatua gani amechukua kuondoa tatizo la maji katika kata yake alijibu kuwa amelipokea atalifanyia kazi.

Bw.Munge alisema tatizo la maji katika kata ya Ludewa limeshakuwa kubwa hivyo ofisi yake inatarajia kufanya mabadiliko makubwa ya miundombinu ya maji kutokana na bajeti itakavyo tosheleza .
mwisho




No comments: