Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

March 25, 2013

KATA YA LUANA WILAYANI LUDEWA YAPATA MATUMAINI YA KUWA NA NISHATI YA UMEME WA MAJI.





Wananchi wa kata ya Luana wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe wanatarajia kunufaika na nishati ya umeme utakaozalishwa katika mto Mlimba katika kijiji cha Mbwila kutokana na mto huo kuwa na maporomoko ya maji yatakayotoshereza kuzalisha umeme huo.

Akikagua chanzo hicho diwani wa kata ya Luana kupitia chama cha Mapinduzi Bw. Thomaso Haule alisema kupitia maporomoko hayo kata yake yenye vijiji vitatu ambavyo ni kijiji cha Luana,Mbwila na Muholo itanufaika kwani wameshajitokeza wadau wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Bw.Haule alisema wananchi wa kata ya Luana wanafulsa mbalimbali ambazo zingeweza kuwainua kiuchumi lakini kutokana na hali halisi ya kata hiyo kutokuwa na nishati ya umeme imekuwa vigumu kuzitumia fulsa hizo ili kujinufaisha.

Alisema bado anaendelea na mazungumzo na wadau mbalimbali wanaoweza kuwekeza katika sekta ya kilimo,umeme na uchimbaji wa chokaa ambavyo vinapatikana katika kata yake ingawa sula la umeme wameshajitokeza watu wa shirika la LCBA ambao wameonesha nia ya kufanya kazi hiyo kwa haraka zaidi
.
Bw. Haule alisema shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu wilayani Ludewa linalojishughurisha na uanzishaji wa umeme vijijini la LCBA limetembelea chanzo hicho na kujionea uwezekano wa kujenga mitambo yao itakayoweza kuzalisha umeme na kusambaza katika vijiji vya kata hiyo na vijiji vya jirani ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuri za usindikaji wa vyakula.

“Tunaweza kupata umeme wenye nguvu kubwa kwa kupitia mito inayotiririsha maji katika kata yetu kwani tayari wadau wameshajitokeza kufanya kazi hiyo,kitu cha msingi ni kuwaelimisha wananchi wanaolima mazao yao katika vyanzo vya maji waache maramoja ili kila mwananchi aweze kunufaika na maji hayo”,alisema Bw.Haule.

Aidha katibu wa shirika la LCBA Bw.Joseph Kayombo alisema maporomoko hayo yanauwezo wa kuzalisha umeme utakaoweza kuwanufaisha wananchi wa kata ya Luana na kata jirani lakini bado haijajulikana umeme utakaozalishwa hapo ni kiasi gani.

Bw.Kayombo alisema wanatarajia kuwaleta wataalamu wa kuyapima maji hayo na kujua ni umeme kiasi gani utazalishwa ikiwa ni pamoja na kupata kibari cha matumizi yam to huo kutoka kwa mamlaka ya bonde la ziwa Nyasa kama walivyoweza kufanya katika kata ya Mundindi.

Alisema wananchi watarajie makubwa kutoka katika shirika lake lakini wanachotakiwa kukifanya wananchi hao ni kutofanya shughuri za kilimo katika vyanzo vya maji sambamba na kutoa ushirikiano katika shirika lake ili kufanikisha mradi huo haraka iwezekanavyo.

Bw.Kayombo alisema awali katika mto huo kuna mwananchi mmoja laiweza kubuni kwa kutengeneza umeme usio wa kitaalamu ambao uliweza kutumika katika kijiji cha Mbwila na kushindwa kuuendeleza kutokana na teknolojia aliyoitumia kuwa chini ya kiwango.

Kupitia shirika la LCBA lenye uzoefu wa kazi hizo za umeme wataweza kuboresha huduma hiyo ambayo itakuwa endelevu na itaweza kusambazwa kwa wananchi wengi zaidi kwa gharama nafuu tofauti na maeneo mengine cha msingi wananchi wanapaswa kutambua mradi huo ni wakwao na si mtu mwingine.

Mwisho.

No comments: