Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

September 12, 2012

WAANDISHI WA HABARI MKOANI NJOMBE WAKACHA KUFANYA KAZI NA JESHI LA POLISI

Na Nickson Mahundi,Njombe.

Waandishi wa habari mkoani Njombe wameungana na wenzao nchini katika kulaani mauaji ya mwandishi mwenzao wa kituo cha runinga cha chanel ten Daudi Mwangosi yaliyotokea Septemba pili katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa muda chama cha waandishi wa habari mkoa wa Njombe Bw. Bazil Makungu alisema wandishi wa habari  mkoani hapa hawaishi katika kisiwa hivyo kitendo cha kinyama kilichomkuta mwandishi mwenzao Daudi Mwangosi aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Iringa hakitafumbiwa macho.
Bw.Makungu alisema unyama huo unaweza kumkuta mwandishi yeyeote nchini wakati akitekeleza majukumu yake iwapo hakutakuwa na umoja na kuungana na waandishi nchini kulaani mauaji hayo kwa nguvu zote.

“Waandishi wa habari mkoa wa Njombe tunaungana na wenzetu nchini kulaani mauaji ya mwandishi mwenzetu Daudi Mwangosi, na kuanzia leo ni marufuku kwa mwandishi wa habari mkoani hapa kufanya kazi na jeshi la polisi bila tamko kutoka UTPC, iwapo atatokea mwandishi akafanya nao kazi tutajua huyu si mwenzetu na hataki ushirikiano na umoja wetu,’’ alisema Makungu.

Aidha aliitaka serikali kutoa tamko juu ya mauaji hayo ya kinyama ambayo alisema kwa kawaida hayavumiliki katika taifa hili na ni kitu cha kushangaza ulimwengu kwa nchi kama Tanzania kutumia nguvu kiasi hicho kuwaua waandishi wa habari.

Hata hivyo baadhi ya waandishi wa habari mkoani hapa wameshangazwa na kitendo cha mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Said Mwema kutomsimamisha kazi Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Iringa Michael Kamuhanda ili kupisha tume ya uchunguzi ya mauaji hayo.

“Tunamshangaa sana IGP Said Mwema kwa kushindwa kuchukua uamuzi mgumu juu kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda ambaye ameshindwa kusimamia usalama wa raia na mali zao na badalayake kuwaua raia wasio kuwa na hatia,” alisema  Bw.Makungu.

Itakumbukuwa kuwa Daudi Mwangosi mpaka mauti yanamkuta alikuwa Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani Iringa (Iringa Press Club) IPC.

No comments: