Mwandishi Wetu, Dodoma
HALMASHAURI Kuu ya CCM (Nec), imetangaza majina ya wagombea walioteuliwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho, huku ikionyesha kuwa uchaguzi huo utakuwa na mchuano mkali. Katika orodha iliyotolewa jana, baadhi ya makada wake maarufu akiwamo Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono na Salum Londa wametupwa.
Mchuano mkali unaonekana kuwapo
kwenye nafasi ya ujumbe wa Nec Mkoa wa Manyara ambako Waziri Mkuu Mstaafu,
Frederick Sumaye anachuana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu.
Mchuano huo unatarajiwa kuwa mkali
katika nafasi ya uenyekiti kwenye baadhi ya mikoa kutokana na kupitishwa kwa
majina ya makada wake maarufu. Mwanza ni miongoni mwa mikoa hiyo kwani Nec
imepitisha jina la Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo
ambaye atachuana na Clement Mabina anayetetea nafasi hiyo.
Makada hao watapata ushindani
mkali kutoka kwa Zebedayo Athumani, Joseph Yaredi na Mashimba Hussein
Mashimba.
Dar es Salaam nako kunatarajiwa
kuwa na mchuano mkali kwani mwenyekiti wa sasa, John Guninita atachuana na
Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi Makao Makuu ya CCM, Matson Chizzi na kada
mwingine, Ramadhan Madabida. Godfrey Mwalusamba, Harold Adamson na Paul
Laizer wanawania nafasi hiyo mkoani Arusha.
Vita nyingine kali ipo kwenye
Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT), ambako Mwenyekiti wa sasa, Sofia Simba
ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto anachuana na
Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango Malecela na Mbunge wa Viti Maalumu,
Mayrose Majige.
Katika Jumuiya ya Wazazi, Mkono
ambaye alikuwa akiwania nafasi hiyo ametupwa na kuwaacha Abdallah Bulembo,
Martha Mlata na kada wa siku nyingi, John Barongo kuchuana.
Awali, Mkono alikatwa jina lake na
Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya hiyo na kutangaza hali ya hatari akisema
asipopitishwa patachimbika. Jina lake lilirejeshwa na Kamati ya Usalama na
Maadili kabla ya kukatwa tena na Kamati Kuu.
Alipoulizwa jana kuhusu kuondolewa
katika kinyang’anyiro hicho, Mkono alisema: “Nimekubaliana na uamuzi wa chama
na nitaendelea kuwa mwanachama wa CCM. Nimelelewa na kukulia CCM na
nitaendelea kubaki CCM nikiwa mwanachama mtiifu.”
Katika Jumuiya ya Vijana (UVCCM),
mchuano mkali unaonekana kuwa katika nafasi ya makamu mwenyekiti kwani mmoja
wa wagombea waliopitishwa, Paul Makonda anaaminika kuwa na nguvu kubwa kutoka
katika kundi la wabunge na mawaziri wapambanaji wa ufisadi. Makonda anawania
nafasi hiyo pamoja na Mboni Mhita na Ally Hapi.
Nafasi ya Mwenyekiti UVCCM
inawaniwa na Sadifa Juma Khamis, Rashid Simai Msaraka na Lulu Mshamu
Abdallah.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa atachuana na Dk Salash Toure na Nanai Kanina kwenye nafasi ya ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Monduli. Wagombea wa ‘kundi la kifo’ Vigogo kadhaa wamepitishwa kuwania nafasi 10 za Nec, wakiwamo baadhi ya mawaziri na viongozi wa juu wa chama hicho.
Miongoni mwao ni Mbunge wa Bunge
la Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Dk David Mathayo David, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu
na Bunge, William Lukuvi, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January
Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na
Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama.
Wengine ni Katibu wa Fedha na
Uchumi CCM, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano, Stephen
Wassira, Waziri wa Habari, Michezo, Utamaduni na Vijana, Dk Fenela Mukangara
na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela.
Kwa upande wa Zanzibar, nafasi 10
za Nec kupitia kapu zinawaniwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali
Iddi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan.
Katika orodha hiyo wamo, Waziri wa
Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, Waziri wa zamani wa Ofisi ya Makamu wa Rais,
Muungano, Mohamed Seif Khatib, Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Omar
Yussuf Mzee na Naibu Waziri wa Fedha wa zamani, Abdisalami Issa Khatib.
Familia ya Kikwete Katika uteuzi huo wa wagombea, majina matatu ya wagombea kutoka katika familia ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete yamepitishwa.
Waliopitishwa ni pamoja na mkewe
Salma Kikwete ambaye anakuwa mgombea pekee katika nafasi ya ujumbe wa Nec
Lindi Mjini na Ridhiwan Kikwete ambaye pia ni mgombea pekee wa nafasi hiyo
katika Wilaya ya Bagamoyo.
Mbali ya hao, Nec pia imepitisha jina la Mohamed Mrisho Kikwete kuwania nafasi ya uenyekiti wa Wilaya ya Bagamoyo. Vigogo watemwa Nec imewatema vigogo kadhaa, baadhi yao ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Azim Premji na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Vicky Nsilo-Swai ambaye alikuwa anagombea ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Hai na kada wa siku nyingi, Salum Londa.
Pia wamo wabunge, Sarah Msafiri,
Munde Tambwe, Deo Filikunjombe na Victor Mwambalaswa.Wengine waliotemwa ni
Hussein Bashe na hasimu wake mkubwa kisiasa Dk Hamis Kigwangalla, Jamali
Kassim, Anthony Mavunde na Emmanuel Nzungu, ambaye aliomba kugombea Uenyekiti
Wilaya ya Ilemela, Mwanza.
Mgeja chupuchupu Mwenyekiti wa sasa wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja aliponea chupuchupu kutemwa baada ya Nec kurejesha jina lake kwenye orodha ya wagombea lililokuwa limeondolewa na vikao vya awali.Taarifa za kuondolewa jina la Mgeja zilivuja tangu juzi wakati kikao cha Kamati Kuu kilipoketi ikidaiwa ni kutokana na malumbano kati yake na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.
Inadaiwa wakati wa kujadiliwa
Mgeja, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alitoka kwenye kikao na Katibu
wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na kumwachia kiti Makamu Mwenyekiti wa CCM
Bara, Pius Msekwa.
Baada ya mjadala mrefu wa kumtetea Mgeja kwamba hakutendewa haki, Msekwa alifikia uamuzi wa kurejesha jina. “Baadhi ya waliomtetea ninaokumbuka ni Dk Makongoro Mahanga na Peter Serukamba, lakini wakati wa mjadala wa Mgeja, Mwenyekiti (Kikwete) na Nape walikwenda chemba, kiti akaachiwa Msekwa,” kilisema chanzo chetu. Awali, kada mkongwe wa chama hicho, Kingunge Ngombale - Mwiru aliituhumu Kamati Kuu kwamba imevunja kanuni za uchaguzi kwa kuteua majina zaidi ya matatu kwenye nafasi moja.
Hata hivyo, inadaiwa Msekwa
alimsomea kanuni moja baada ya nyingine zinazohusu uteuzi hali iliyoonyesha
kama kumweka darasani na hatimaye ikabainika hakuna kanuni iliyovunjwa.Hoja
hiyo ilitokana na baadhi ya mikoa kwenye nafasi moja kusimamisha wagombea
zaidi ya watatu kama nafasi ya mwenyekiti mkoa wa Mwanza.
Hatua hiyo inadaiwa inalenga
kuondoa matokeo ya kupanga kwa baadhi ya wagombea na kwamba, kwa hali hiyo
mshindi hawezi kupatikana kwa mzunguko wa kwanza.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu
Mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba anadaiwa kushambulia mtandao uliokuwa
umejipanga na kuweka wagombea wao hata kama hawana sifa.“Yule mzee (Makamba)
amewachana-chana vibaya, anasema hapa tunasajili timu, kama majina hayafai
yaondolewe,” kilidokeza chanzo na kuongeza kwamba hoja hiyo iliungwa mkono na
kada mkongwe wa chama hicho, Mzee Peter Kisumo.
|
September 27, 2012
VITA NEC CCM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment