Viongozi wa Vyama pinzani wilayani Ludewa wamesusia kuingia katika kikao cha baraza la madiwani jana kutokana na kikao hicho kuchelewa muda wa kuanza kama maelekezo waliyoyapata kutoka kwa kaimu mkurugenzi wa Halmashauri.
Akiongea na mwandishi wa mtandao huu mwenyekiti wa vyama pinzani vya siasa Bw.Lazaro Mwinuka alisema wamefikia maamuzi ya kususia kikao hicho kutokana na barua walizopewa kuonesha kikao hicho kingeanza saa tatu kamili asubuhi lakini bila maelezo ya msingi walijikuta wakiwa wao tu ukumbini.
Bw.Lazaro alisema kutokana na madiwani wa chama cha Mapinduzi kutomaliza uchaguzi wa makamu mwenyekiti wa halmashauri ndani ya chama chao ndio sababu ya kuchelewa kufanyika kikao hicho ambacho kililazimika kuanza saa nane mchana ikiwa viongozi hao wa upinzani wametawanyika.
Aidha kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Bw.Lazaro Mapunda akitolea ufafanuzi suala hilo alikubali kuwa na mapungufu ya kuchelewa kikao hicho kutokana na uchaguzi wa makamu mwenyekiti wa halmashauri ambapo kila chama kilitakiwa kuleta jina moja ili kufanyika uchaguzi kwa pamoja.
Bw.Mapunda alisema kikao hicho cha uchaguzi kilipaswa kuanza saa tatu asubuhi lakini kutokana na sababu zisizozuilika kukao hicho kilichelewa na kuanza saa nane mchana na kilichofanyika ni kutowataarifu mapema viongozi hao.
Katika kikao hicho Bi.Monika Mchilo ambaye ambae ni Diwani wa kata ya Ludewa alikuwa mgombea pekee kutoka Chama Cha Mapinduzi(CCM) akichuana na John Kiowi wa chama cha TLP ambaye ni Diwani wa Kata ya Lupingu.
Hata hivyo Bi.Monika alishinda uchaguzi huo na kutangazwa kuwa makamu mwenyekiti wa Halmashauri akimshinda mpinzani wake Bw.Kiowi kwa kura 29 kwa 3 ambapo wapigakura walikua 33 na kura moja iliharibika.
Bw.Lazaro mwinuka ameendelea kusisitiza kuwa vyama vingine vya siasa wilayani Ludewa havithaminiki kama maeneo mengine hivyo kuwataka viongozi wa halmashauri kuacha tabia hiyo kwani iko siku vyama hivyo vitashika dora.
No comments:
Post a Comment