Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

September 09, 2012

WANANCHI KANDOKANDO YA ZIWA NYASA WAHOFIA MAISHA YAO


Wananchi wilaya ya Ludewa mkoani Njombe hasa waishio katika kata za pembezoni mwa ziwa Nyasa wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa ya maisha yao kufuatia mgogoro ulioko baina ya nchi mbili za Tanzania na Malawi.

Wakitoa malalamiko yao katika kikao cha baraza la Madiwani lililofanyika jana wadiwani wa kata saba zilizoko mwambao mwa Ziwa Nyasa walisema wananchi wao wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli za kimaendeleo wakihofia usalama wa maisha yao.

Madiwani hao waliilalamikia kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kwa kushindwa kuishawishi Serikali kuu kuweka kambi ya Jeshi la wananchi wa Tanzania katika kata moja ya zile za mwambao wa ziwa Nyasa ili wananchi waweze kuamini kama wako mikono salama ya Serikali yao.

"Tumekua tukiishi kwa hofu kwani kila boti inayoingia usiku katika kata ya Manda wanachi hukimbia na kuja kulala kwa mimi Diwani kutokana na vitisho vya ndege za malawi zilizotua katika ufukwe wetu na hivi karibuni kuna boti ilikuja usiku ikiwa na wazungu wawili na raia mmoja wa Malawi. Wananchi walikimbilia kwangu. Tunaamini kukiwa na kambi ya Jeshi karibu wananchi wataishi kwa kujiamini",alisema Diwani Kizota.

Nae Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Ludewa ambaye pia ni katibu Tawala Bw.John Mahali alisema wananchi wasiwe na wasiwasi kwani Serikali inawalinda wananchi wake kwa karibu hivyo viongozi wa ngazi za juu wanaendelea na mazungumzo na nchi a Malawi.

Bw.Mahali alisema wasione kama Serikali iko kimya bali suala la amani kati ya nchi hizo mbili linazungumzika kama alivyotamka Amiri jeshi mkuu ambaye ni Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzani Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa tusiwe na wasiwasi wowote.

Hata hivyo mbunge wa jimbo la Ludewa Mh. Deo Filikunjombe aliitaka kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ni vyema ingepita katika kata hizo ili iweze kuzungumza na wananchi na kuwahakikishia usalama wao ili waweze kuendelea na kazi za uzalishaji mali kuliko kukaa kimya kwa kuhofia usalama wao.

Bw.Filikunjombe aliwataka madiwani hao kuwaelimisha wananchi kupitia mikutano mbalimbali ili wananchi waweze kutulia na suala la kujenga kambi ya jeshi katika kata hizo, hilo suala ni la kitaifa hivyo Serikali italiangalia kiundani zaidi ili kufanikisha usalama wa watanzania waishio Nyasa.

No comments: