Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan
amemtumia salamu za pole na pongezi Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali
Mstaafu Ezekiel Kyunga kwa kazi nzuri na kubwa waliyoifanya ya kuwaokoa
wachimbaji wadogo 15 waliofukiwa na maporomoko ya udongo kwenye Mgodi wa
Dhahabu wa RZU uliopo katika Kijiji cha Nyarugusu, wilaya ya Geita
katika mkoa wa Geita.
Tukio
hilo la kufukiwa wachimbaji hao wadogo 15 wakiwemo Watanzania 14 na
raia Mmoja wa China lilitokea usiku wa Tarehe 26 Januari mwaka 2016.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan
amesema amepokea kwa furaha taarifa za kuokolewa kwa wachimbaji hao
wadogo na amesifu na kupongeza jitihada za kuwaokoa wachimbaji hao
zilizofanywa na Serikali ya Mkoa wa Geita, Jumuiya ya Wachimbaji Wadogo
wa mkoa wa Geita, Wamiliki wa Migodi ya Dhahabu na wananchi kwa ujumla
kwa kutoa vifaa mbalimbali vya uokoaji jitihada ambazo zimepelekea
kuokolewa kwa wachimbaji hao wakiwa hai.
Makamu
wa Rais amesisitiza kuwa “jitihada ,Umoja na Mshikamano ulioonyeshwa na
makundi mbalimbali katika kuwaokoa ndugu zetu waliofukiwa na maporomoko
ya Udongo wakiwa kazini huko Geita ni mfano mzuri na wakuigwa na
wananchi na taasisi nyingine nchini katika kujitolea kwa hali na mali
hasa vifaa vya uokoaji kwa ajili ya kusaidia watu wanaopatwa na majanga
ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kama walivyofanya ndugu zetu wa
mkoa wa Geita nawapongeza Sana”.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wamiliki wa migodi kote
nchini wahakikishe wanafanya kazi zao za uchimbaji wa madini kwa
kuzingatia kanuni,taratibu na sheria kama hatua ya kuepuka madhara
yanayoweza kutokea wakiwa wanafanya shughuli zao za uchimbaji wa madini.
Kupitia
kwako Mkuu wa mkoa wa Geita napenda kutuma salamu za pole kwa ndugu,
jamaa na marafiki kufuatia kutokea kwa tukio hilo na nawaombea kwa
Mwenyezi Mungu wachimbaji hao ambao kwa sasa wanapatiwa matibabu Katika
Hospitali ya Serikali ya mkoa wa GEITA matibabu mema ili waweze kupona
haraka na kurejea kwenye kazi zao za kujitafutia riziki.
Wakati
huo huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia
Suluhu Hassan ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Kudhibiti
Maafa nchini, Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya Mambo ya
Ndani kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa
Geita na kupekelea kuchukuliwa hatua za haraka katika kushughulikia
ajali hiyo.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dar es Salaam
29-Jan-2017
No comments:
Post a Comment