Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), inatarajia kukutana Desemba 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam, imefahamika.
Taarifa
iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Msemaji wa chama hicho, Seleman
Mwenda, ilisema mkutano huo utatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu (CC),
kitakachofanyika Desemba 11 hadi 12, jijini Dar es Salaam.
Ingawa
hadi sasa ajenda za vikao hivyo hazijajulikana, lakini wachambuzi wa
masuala ya siasa wanasema, kufanyika kwa vikao hivyo kunatajwa kuwa ni
mkakati wa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli kutaka
kuisuka upya CCM.
Baadhi
ya wachambuzi hao wanasema uteuzi wa wajumbe watatu wa sekretarieti ya
chama hicho kuwa mabalozi ni mwendelezo wa mkakati huo kuelekea uchaguzi
mkuu wa ndani wa chama hicho mwakani.
Mbali
na hao mjumbe mwingine wa sekretarieti, Dk Asha -Rose Migiro aliteuliwa
kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na nafasi yake ndani ya chama
kuchukuliwa na Pindi Chana ambaye naye ameteuliwa kuwa balozi.
Katika
Serikali ya awamu ya nne, Pindi Chana alikuwa Naibu Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto na baadae mwaka huu aliteuliwa kuwa Katibu
wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Mjumbe
wa Kamati Kuu (CC), Dk. Emmanuel Nchimbi, kuteuliwa kuwa balozi
kunathibitisha kuhusu uwapo wa mkakati wa Rais Magufuli kusuka upya
chama hicho kwa kuweka sura mpya.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye pia ni
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa chama hatarajiwi kuwapo katika safu
hiyo mpya, kwani tayari yupo serikalini.
Mwingine
ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Rajabu Luhwavi ambaye
ameteuliwa kuwa balozi anazidi kutoa taswira kuhusu mkakati wa Rais
Magufuli kusuka upya chama hicho.
Katika
hotuba ya Rais Dk. Magufuli baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa chama
hicho alisema miongoni mwa mambo atakayoyatekeleza ni kuimarisha
utendaji kazi wa chama, huku akimnukuu hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere kwa kusema kuwa chama legelege huzaa serikali legelege.
“Nitashirikiana
nanyi kujenga chama madhubuti chenye uwezo wa kuisimamia vizuri
Serikali ili itekeleze ipasavyo majukumu yake, ikiwezekana tutapitia
upya katiba na kanuni zetu ili kukidhi mazingira ya sasa na kuweza
kuwatumikia wananchi ipasavyo.
“Tutahakikisha
pia tunakuwa na safu bora ya uongozi katika ngazi zote kuanzia shina
hadi taifa. Tutaangalia muundo (structure) wa chama chetu katika ngazi
mbalimbali na kuondoa vyeo visivyokuwa na tija katika chama na hasa
wakati huu wa mfumo wa vyama vingi” alisema Dk. Magufuli.
Dk.
Magufuli alihoji kuhusu uhalali wa kuendelea kuwapo vijana wa chipukizi
ndani ya chama hicho pamoja na baadhi ya safu za uongozi ndani ya chama
hicho.
“WanaCCM
ni lazima tujiulize je ni kweli katika zama hizi bado tunahitaji mtoto
wa miaka 8 hadi 15 kuwa chipukizi kwa ajili ya kumtumia kwenye siasa
badala ya kumwacha asome? Kama akiwepo chipukizi wa CCM, chipukizi wa
NCCR au Chadema ama TLP tutakuwa tunajenga nchi ya namna gani?
“Je
bado kuna umuhimu wa kuwa na makamanda wa vijana ambao mara nyingi
wenye kupewa vyeo hivyo ni wale wenye uwezo wa kifedha pekee? Je walezi
kwenye Umoja wa Wanawake (UWT) bado wanahitajika? Je washauri ndani ya
Jumuiya ya Wazazi wanahitajika?" Alihoji Dk. Magufuli.
No comments:
Post a Comment