Chama cha Wananchi (CUF), kimesema taarifa zinazosambazwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kwamba Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad anataka kuhama chama hicho ni za kupuuzwa kwa kuwa hazina ukweli.
Naibu
Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema hayo jana
baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kuwa Maalim anataka kuondoka ndani ya chama hicho cha upinzani.
Alisema
tangu kuibuka kwa mgogoro ndani ya CUF na Mwenyekiti wao, Profesa
Ibrahim Lipumba imekuwapo mikakati ya kuwakatisha tamaa jambo ambalo
halitafanikiwa.
Mazrui
alisema wanaopanga mikakati wamehangaika kila njia na wameonekana
kukwama, hivyo kuibuka na mkakati wa kumzushia Katibu Mkuu kuhama chama.
“Hivi
unafikiria Katibu Mkuu anaweza kuhama chama katika mazingira rahisi
kiasi hicho? Hiki chama amekipigania vya kutosha wataondoka wao,” alisema.
Naibu
Katibu Mkuu huyo aliwataka wana CUF kuendelea kutoa ushirikiano kwa
Katibu Mkuu wao na kupuuza kauli za watu ambao wamepoteza mwelekeo
kisiasa.
Alisema
CUF si chama kinachotegemea mtu mmoja, na pia hakiko tayari kumpoteza
Maalim kwa vibwagizo vya vibaraka wa chama tawala, ambao hawataki
kupigania mabadiliko nchini.
Aidha,
kuhusu chama kuwa kimya kuhusu madai yao ya ushindi katika uchaguzi wa
Oktoba 25 mwaka jana, alisema bado wanaendelea na mchakato huo na
watatoa taarifa hivi karibuni kuhusu hatua waliyofikia.
Mazrui
alisema kila kitu kinakwenda vizuri na kutaka wana CUF kuwa na subira
katika kipindi hiki, kwani mambo mazuri hayahitaji haraka.
Alisema
ushirikiano wanaopata kutoka jumuiya ya kimataifa ni mzuri hali ambayo
inawapa matumaini ya kuhakikisha kuwa haki inapatikana.
“Suala
la madai ya ushindi wa uchaguzi linakwenda vizuri, na naamini hatima
yake itapatikana kwa busara, ni vema wana CUF kuwa na subira,” alisema.
Jana
katika baadhi ya magazeti ziliandikwa habari zikimhusisha Maalim na
kuhama CUF na kutajwa kutarajia kuhamia vyama vya ADA-TADEA, AFP au
ACT-Wazalendo, ambapo viongozi wa vyama hivyo walikanusha taarifa hizo.
Hali kadhalika Katibu Mkuu huyo alihusishwa na kutaka kujiunga na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
No comments:
Post a Comment