WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amepokea msaada wa sh. milioni 50 kutoka Shirika
la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kusaidia ujenzi wa shule ya
sekondari Lindi iliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu.
NSSF
imetoa msaada huo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake iliyoitoa Julai
17, 2016 katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya
shule ya hiyo iliyoendeshwa na Waziri Mkuu .
Katika
ajali hiyo, shule ya sekondari Lindi iliathirika kwa asilimia 34 ambapo
vyumba tisa vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la
maabara ya kemia na fizikia yaliungua na kusababishia hasara ya sh.
milioni 682.78.
Akipokea
msaada huo leo (Jumanne, Agosti 30, 2016) Waziri Mkuu ameushukuru
uongozi wa shirika hilo na kuwaomba wadau wengine waliotoa ahadi
wazitekeleze ili waweze kukamilizsha ujenzi wa majengo hayo.
“Naamini
fedha hizi zitakwenda kufanya kazi ambayo NSSF wameikusudia. Na leo hii
naikabidhi kwa Meya wa Manispaa ya Lindi pamoja na Mkurugenzi wake ili
waende kuzifanyia kazi,” amesema.
Baada
ya kukabidhiwa hundi hiyo na Waziri Mkuu, Meya wa Manispaa ya Lindi,
Mohamed Lihumbo amelishukuru shirika hilo kwa kutimiza ahadi waliyoitoa
siku ya harambee na kwamba fedha hizo hazitapotea kwa sababu zinaenda
kutumika katika malengo yaliyokusudiwa.
Meya
huyo amesema baada ya kukamilisha ujenzi wa shule hiyo wataanda hafla
na kuwaita wadau wote waliotoa michango yao kwa ajili ya ujenzi huo ili
wakaone matumizi ya michango waliyoitoa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof. Godius Kahyarara amesema
msaada huo ni sehemu ya mpango wa shirika hilo wa kusaidia jamii katika
mambo mbalimbali kwa mujibu wa sera iliyowekwa na shirika hilo.
“NSSF
imekuwa kinara kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kutoa misaada
mbalimbali ya kijamii ambapo imejiwekea sera ya kusaidia katika sekta za
elimu, afya na huduma nyingine muhimu za kijamii,” amesema.
Prof.
Kahyarara amesema misaada hiyo haiathiri michango ya wanachama wa mfuko
huo na mafao yatolewayo kwani hutokana na faida inayopatikana kwa
uwekezaji makini wa mfuko huo.
Habari na Ofisi ya Waziri Mkuu
No comments:
Post a Comment