Zahamati ya Luvuyo ikiwa tayari imeshasogezewa mradi wa maji
Shule ya msingi Luvuyo nayo imenufaika na mradi huo
Mkurugenzi wa shirika la PADECO Bw.Willbad Mwinuka akifuatilia burudani ya ngoma ya asili katika uzinduzi huo
wafadhi wakizindua tenki la maji katika kijiji cha Luvuyo kata ya Madope wilayani Ludewa
kaimu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Mh.Kongo akiwa na wafadhiri ambao ni Bi.Ines Obieta na Bi.Jimena Frankos
viongozi wa jimbo katoliki la Njombe wakiwa na wafadhiri
Mhandisi Zefania Chaula akiongea na wananchi wa Luvuyo
mmoja wa wafadhiri wa mradi huo Bi.Ines Obieta akizindua bomba la maji Livuyo akiwa na mkurugenzi wa PADECO Bw.Willbad Mwinuka
Diwani wa kata ya Madope Mh.Polycape Mlelwa akiongea na wananchi wa Luvuyo
Kaimu mwenyekiti wa Halmashauri Ludewa Mh.Mathei Kongo akizindua mradi wa maji katika tenki kijiji cha Luvuyo
Shirika
lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu mkoani Njombe ambalo ni shirika la
maendeleo shirikishi la PADECO(participatory Development Concern) limekuwa ni
mkombozi mkubwa katika kuhakikisha jamii ya Ludewa na vijiji vyake inapata maji
safi na salama kwa kujenga miradi ya maji vijijini.
Akisoma
taarifa kwa mgeni rasmi jana ambaye ni kaimu mwenyekiti wa Halmashauri ya
wilaya ya Ludewa katika uzinduzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Luvuyo kata
ya Madope mkurugenzi wa shirika la PADECO Bw.Willbad Mwinuka alisema kuwa
shirika lake lilianza kuutekeleza mradi huo wa maji mwaka 2015 baada ya kubaini
kuwa kunauhaba mkubwa wa maji katika kijiji cha Luvuyo.
Bw.Mwinuka
alisema kuwa licha ya kufanya mradi huo wa maji katika kijiji cha Luvuyo kata
ya Madope pia shirika la PADECO limefanya miradi ya maji katika vijiji vya
Muholo kata ya Luana,Lipangala na Ugera kata ya Mkongobaki pamoja na
Maholong’wa kata ya Ludende ambako mradi unaendelea vizuri hivyo ni wazi
ahirikala lake limekuwa mkombozi mkubwa katika kupunguza kero ya upatikanaji wa
maji safi na salama.
Alisema kuwa
mradi huo ambao umefadhiriwa na shirika la MANOS UNIDAS kupitia jimbo katoriki
la Njombe kwa kiasi cha shilingi milioni 186.2 ambapo Halmashauri ya wilaya ya
Ludewa imechangia kiasi cha shilingi milioni 32.6 taslimu wakati nguvu kazi ni
shilingi 24 milioni wakati shirika la PADECO limechangia kiasi cha shilingi
milioni 4 usimamizi taslimu pia wananchi walichangia pesa taslimu kiasi cha
shilingi milioni 5 pamoja na nguvu kazi katika ujenzi wa mradi.
Bw.Mwinuka
alisema kuwa kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa mtego
wa maji,tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 75000,vituo 36 vya maji,njia
kuu na njia mgawanyo za umbali wa kilomita 19.7 pamoja na chemba za kutolea
uchafu na hewa kwani mradi huo ni mkubwa unaweza kusambazwa hata katika vijiji
jirani.
“Tumefanya
miradi mingi katika wilaya ya Ludewa ya namna hii na imekuwa ni msaada mkubwa kwa
wananchi kwani hapo awali tatizo la uhaba wa maji lilikuwa ni kubwa na
lilisababisha magonjwa ya tumbo na upotevu wa muda kwa akinamama kwa kutafuta
maji umbali wa zaidi ya kilomita 7,mahudhurio hafifu kwa wanafunzi hivyo PADECO
tumekuwa suruhisho kubwa”,alisema Bw.Mwinuka.
Bw.Mwinuka
alisema kuwa upatikanaji wa maji kwa urahisi katika kijiji cha Luvuyo
utarahisisha wananchi kufanya kazi za kimaendeleo kama ujenzi wa nyumba bora
kwani wataweza kutengeneza tofari karibu na makazi yao pia afya zitaboreshwa na
wanafunzi wateweza kuhudhuria masomo yao kwa ufasaha tofauti na awali walitumia
muda mwingi katika utafutaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani.
Akitoa
hotuba mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi huo wa maji kaimu Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Ludewa ambaye pia ni diwani wa kata ya Luilo Mh.Mathei
Kongo alisema kuwa shirikia la PADECO limekuwa mfano wa kuigwa kwani idadi
kubwa ya wananchi wa wilaya ya Ludewa wamenufaika na uwepo wa shirika hilo.
Mh.Kongo
alisema ni mashirika machache yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa yakiwafikia
wananchi moja kwa moja kwani yako mashirika ya mfukoni ambayo hutumia fedha za
wafadhiri kwa kujinufaisha hivyo aina ya
mashirika hayo yanapaswa kujifunza kwa kupitia shirika la PADECO katika
utendaji usio na mashaka kuanzia kwa wafadhiri,Serikalini na hata kwa wananchi
wenyewe.
Alisema
Serikali hasa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa inatambua mchango mkubwa wa
PADECO katika kuhakikisha jamii ya wanaludewa inanufaika na miradi ya maji
inayojengwa na shirika hilo hivyo yapaswa wananchi kuitunza miundombinu ya
mradi huo ili uweze kunufaisha vizazi vilivyopo na vijavyo.
Naye Diwani
wa kata ya Madope Mh.Polycap Mlelwa aliupongeza mradi wa PADECO na ule wa Jimbo
katoliki la Njombe kwa kuisaidia jamii ya Luvuyo kwani bila kutatua tatizo la
upatikanaji wa maji kwa urahisi maisha ya wananchi hao yangeendelea kuwa duni
na kuugua magonjwa ya tumbo kila wakati.
Mh.Mlelwa
alikiri kuwepo kwa tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama katika
kata yake hivyo aliwaomba wafadhiri hao kuendelea kuvisaidia na vijiji vingine
nyenye mahitaji hayo ambayo imekuwa kero kubwa hasa kwa akina mama kuacha
kufanya kazi za kilimo na badala yake kutumia muda mwingi katika kutafuta maji
katika mito iliyoko mbali na makazi ya watu.
Aidha
akishukuru kwa niaba ya wananchi mmoja wa wananchi wa kijiji cha Luvuyo na mdau
wa maendeleo katika kata hiyo Mhandisi Zefania Chaula alisema kuwa ni furaha
iliyoje kwa wananchi wa Luvuyo kukabidhiwa mradi wa maji ambao unafanya kazi
vizuri kwani haikuwa kazi rahisi kufanikisha kazi hiyo ikizingatiwa umbali wa
chanzo cha mradi huo wa maji.
Mhandisi
Chaula alisema kuwa ni miaka mingi tokea nchi hii ipate uhuru wananchi hao
hawajawahi kupata unafuu wa maji kama ilivyo leo kwani pongezi za dhati
ziwaendee wote waliofanikisha mradi huo ambao unafanya kazi vizuri kwani
haikuwa kazi rahisi kufanikisha kazi hiyo ikizingatiwa umbali wa chanzo cha
mradi huo wa maji.
Aliwataka
wananchi kutunza chanzo cha maji hayo kwa kuacha kufanya shughuri za kibinadamu
pembezoni mwa chanzo hicho ili mradi huo uweze kuwa endelevu ili mwisho wa siku
uweze kuvisaidia na vijiji jirani vyenye uhaba wa maji kama ilivyokuwa kijiji
cha Luvuyo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment