MKUU
wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu amewaagiza makamanda wa
Polisi kote nchini, kuendesha oparesheni kali ya kuwachukulia hatua za
kisheria, waendesha bodaboda wasiotii sheria za usalama barabarani.
Ametaja
makosa yatakayosababisha waendesha bodaboda hao kukamatwa kuwa ni
pamoja na kubeba abiria zaidi ya mmoja, kupita katika taa nyekundu na
kutovaa kofia ngumu.
IGP
Mangu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na maofisa wakuu wa Polisi,
wakiwemo makamanda wa Polisi wa mikoa, vikosi na makao makuu katika
kikao kazi kilichofanyika Dar es Salaam hivi karibuni ambacho
kilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.
Alisema
waendesha bodaboda wamekuwa wakikaidi kufuata sheria za usalama
barabarani, lakini sasa mwisho wao umefika na kuwataka makamanda wa
Polisi wa mikoa kote nchini, kutekeleza maelekezo hayo, ili kuleta
nidhamu kwa bodaboda katika kufuata sheria za usalama barabarani.
IGP
Mangu alisema suala la kufuata sheria za usalama barabarani kwa
bodaboda halina mjadala na kila Kamanda ahakikishe kuwa wote wasiofuata
sheria na kukaidi, wanakamatwa bila kuoneana muhali kwa kuwa wamekuwa
wakisababisha ajali zinazoweza kuzuilika.
“Pamoja
na kuendelea kudhibiti uhalifu wa aina zote, natoa maelekezo kwa kila
mkoa kuhakikisha unaendesha oparesheni kali dhidi ya bodaboda, ili
kupunguza ajali zinazosababishwa na bodaboda.
“Wengi
wao hawataki kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani, tusiwaonee
muhali maana maisha ya watu ni muhimu sana na jambo la msingi ni
kusimamia sheria tu,” alisema IGP Mangu.
Awali
akifungua kikaokazi hicho Waziri Kitwanga alilitaka Jeshi la Polisi
kuendelea na mapambano yake dhidi ya uhalifu na wahalifu, ili usalama wa
raia na mali zao uendelee kuimarika na Watanzania waendelee na shughuli
zao za kujiletea maendeleo bila hofu ya kutendewa uhalifu.
No comments:
Post a Comment