Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

February 08, 2016

Hali tete NIDA Ufisadi Wa Mabilioni waibuka....Yadaiwa Kitambulisho Kimoja Kimegharimu Sh 89,800

 

Wingu  zito limetanda ndani ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuhusu matumizi ya  Sh bilioni 179.6 ambako kila kitambulisho  cha taifa kimegharimu Sh 89,800 zikiwamo gharama za utawala


Hayo yamebainika  siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kushangazwa na watendaji wa mamlaka hiyo ikizingatiwa vitambulisho vilivyokwisha kutengenezwa hadi sasa havifiki   milioni mbili na havina saini.

“Utaona ugumu wa kuongoza, nchi inatawaliwa na madudu ya kila aina.  Wapo watu wanacheza na fedha wanavyotaka wakati wapo watu masikini sana  wengine wanataka bodi zao wakakae Ulaya.

“Hapo ndipo tulipofikia, wengine wanalipwa mshahara wa Sh milioni 35 kwa mwezi…naomba mniombee kabla ya kunihukumu, toeni hukumu kwa haki kwa hawa wanaotaka kuifikisha nchi pabaya, toeni hukumu zao haraka,” alisema.

Rais Dk. Magufuli, licha ya kushangazwa na hali hiyo, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipewa Sh bilioni 70 lakini iliweza kutengeneza vitambulisho   23,253,982 ambavyo vilikuwa na saini ya kila mpiga kura na kila kimoja kimegharimu Sh 3,010.

Kutokana na hali hiyo, tofauti ya gharama kati ya kitambulisho kimoja cha NIDA na cha NEC ni Sh 86,790.

Pamoja na hayo, hivi sasa Watanzania wanasuburi   ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Juma Assad, kuhusu  matumizi ya fedha hizo za NIDA.

Januari 26 mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu.

Maimu alisimamishwa kazi pamoja na maofisa wengine wanne, kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali.

Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.

Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alisema taarifa zilizomfikia Rais zinaonyesha kuwa NIDA hadi wakati huo ilikuwa imetumia Sh bilioni 179.6, kiasi ambacho ni kikubwa.

Alisema Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi kujua jinsi fedha hizo zilivyotumika, maana amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.

Licha ya kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, afanye ukaguzi maalumu wa hesabu za NIDA  ukiwamo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa, pia aliitaka Takukuru ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.

Credit: Mtanzania

No comments: