Rais Kikwete azindua mfumo wa BRELA wa kusajili biashara kwa njia ya mtandao.
Rais Jakaya Kikwete, jana amezindua mfumo wa usajili wa kampuni kwa njia ya mtandao utakao ondoa urasimu, rushwa na usumbufu kwa wananchi wanaotaka huduma hiyo. Awali watu walilazimika kusafiri hadi Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).
Kabla
ya kuzinduliwa kwa mfumo huo, Ikulu jijini Dar es Salaam, Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyusi, alisema kazi ya mtandao huo ni
kusajili, kulipia na baadaye kupewa cheti cha usajili ndani ya muda
mfupi.
Uzinduzi
huo ulifanyika wakati wa mkutano wa tisa wa serikali na taasisi
binafsi, ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), chini ya
uenyekiti wa Rais Kikwete, ukiwa na lengo la kupokea utekelezaji kutoka
kwa wizara, taasisi na wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali
yaliyojadiliwa katika mkutano wa nane mwezi Septemba, mwaka huu.
"Mfumo
huu utaondoa rushwa kwa kuwa mwenyekutaka kusajili kampuni hatakuwa na
haja ya kuonana na mtumishi moja kwa moja, ili kusajili ni lazima uingie
kwenye tovuti ya Brela,"alisema.
Kanyusi
alisema mfumo huo umetengenezwa na vijana wa kitanzania kwa kutumia
mapato ya ndani na kuzitaka taasisi nyingine nchini kuiga kwa kutegemea
fedha za nje kutekeleza majukumu yao na kwamba kwa rasilimali za ndani,
taifa linaweza kupiga hatua na kuendekeza misaada au mikopo ya nje ni
kurudi nyuma.
Baada
ya kuzindua mfumo huo, Rais Kikwete alisema umerahisisha maisha ya
Watanzania ambao walilazimika kusafiri hadi Brela kushughulikia usajili.
Katibu Mkuu wa TNBC, Raymond Mbilinyi, alisema kuna mafanikio makubwa ambayo yatarahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini.
Aliyataja
kuwa ni kitengo cha kushughulikia uwekezaji wa wazawa (local content
unity), ambacho kimekubaliwa kiwe chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Baraza
la Taifa la Uwezeshaji.
Alisema
eneo jingine ni urasimu katika kufanya biashara, ambazo ni uwepo wa
sheria nyingi zinazokinzana na kwamba moja ya majukumu yaliyoelekezwa
kwa wizara ni kuangalia jinsi ya kuainisha sheria ili iwe rahisi kwa
mfanyabiashara kujua ni ipi itamsadia kufanya biashara.
"Cha
muhimu zaidi pamoja na dunia inavyoenda tunahitaji kuwa na mfumo rahisi
wa kumuwezesha mfanyabiashara popote duniani kupata taarifa za biashara
inavyofanyika na kupata leseni kwa urahisi, tunakwenda kidijitali
badala ya kuwa na utaratibu wa kuandika karatasi, Wizara ya Viwanda na
Biashara inatengeneza mfumo wa kurahisisha wafanyabiashara ndani na nje
kupata taarifa na leseni kwa urahisi zaidi,"alisema.
Alisema
kuweka mfumo mmoja wa taasisi zinazomuhudumia mfanyabiashara kutoa
huduma katika eneo moja na badala ya kumpa usumbufu wa kwenda katika
kila taasisi.
"Kuna
Osha,TRA, Brela na taasisi nyingine nyingi, hizo zote zinaweka
mazingira magumu, tuje na mfumo ambao wafanyabiashara wanaweza kujipima
katika maeneo yanayohitajika,” alisema.
Katibu
Mkuu Kiongozi na Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya TNBC, Balozi
Ombeni Sefue, alisema mkutano huo pia umeangalia namna ya kukuza utalii
nchini kwa kuboresha mazingira, ikiwamo kuangalia utathimini wa msimu
kwa kupunguza kodi kipindi ambacho siyo msimu wa utalii na kuiweka
katika Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Alisema
mazingira ya biashara yanarahisishwa kwa kuhakikisha serikali inaweka
mfumo mmoja wa kumhudumia mfanyabiashara kuliko kuwa na taasisi nyingi
na kumlazimu mfanyabiashara kuzitembelea zote.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja, alisema mazingira
ya kufanya biashara Tanzania ni magumu kutokana na jinsi ya kupata
leseni, namba ya usajili na usajili wa kampuni na jina la biashara.
Alisema
serikali inatakiwa kupunguza au kuweka katika mfumo mmoja taasisi
zinazomuhudumia mfanyabiashara kwa kuwa zote zipo chini ya serikali.
Mkutano
huo umewakutanisha mawaziri, makatibu wakuu, Shirikisho la wenye
viwanda nchini (CTI) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
No comments:
Post a Comment