Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

June 05, 2015

PADRI KANISA KATOLIKI NA WANAFUNZI SITA WAFARIKI DUNIA BAADA YA GARI WALILOKUWA WAKISAFIRIA KUTEKETEA KWA MOTO




Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.



BAADHI ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya Kigonsera Catechists Secondary School (KCS) iliyopo katika kata ya Kigonsera, akiwemo na Padri wa Parokia ya Kigonsera kanisa katoliki jimbo la Mbinga, mkoani Ruvuma wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria, kutumbukia kwenye korongo na kuteketea kwa moto.



Wanafunzi sita na Padri Hyasint Kawonga ndiyo waliopoteza maisha katika ajali hiyo, wakati wakitoka shambani kuvuna mahindi yaliyokuwa yamelimwa kwa ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni hapo.



Padri Kawonga ndiye Mkurugenzi wa shule hiyo, ambapo gari lenye namba za usajili T 306 AYM aina ya Land rover ndilo walilopata nalo ajali, baada ya gari hilo kushindwa kupanda mlima wakati wanatoka huko shambani.



Tukio hilo lilitokea katika eneo la Minazi kata ya Kigonsera wilayani humo, Juni 4 mwaka huu majira ya jioni ambapo baada ya kushindwa kupanda mlima katika eneo hilo, lilirudi nyuma na kutumbukia kwenye korongo kisha kuwaka moto huku ndani ya gari wakiwa wanafunzi na padri huyo.




Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo kilitokana pia gari hilo kupakia watu kupita kiasi na kwamba wanafunzi 24 walikuwa ndani ya gari hilo, huku wengine wakiwa wananing’inia nje ya bodi la gari wakati linatembea, wamenusurika kupoteza maisha.



Vilevile alisema kuwa baadhi yao hali zao ni nzuri, walikuwa wakipatiwa matibabu kwenye kituo cha afya Kigonsera na wameruhusiwa kurudi nyumbani.



Wanafunzi saba kati ya hao hali zao ni mbaya, ambapo wamekimbizwa Hospitali ya wilaya ya Mbinga kwa ajili ya matibabu zaidi na kwamba maiti zimehifadhiwa katika kituo hicho cha afya, ambacho humilikiwa na jimbo la Mbinga.



Majeruhi wanaopatiwa matibabu katika hospitali hiyo ni Regobert Mahay (16), Edgar Maseko (15) Luiza Mapunda (14), Alpha Kifaru (15), Nelly Nchimbi (16), Theodora Wolfa (16) na kwamba  Josephat Komba (16) amekimbizwa katika Hospitali ya misheni Litembo iliyopo wilayani humo, kwa matibabu zaidi kutokana na kuungua moto vibaya.



Msikhela alisema maiti saba zilichukuliwa kutoka kwenye korongo hilo, ambalo linakadiriwa kuwa na urefu wa mita tano, ambako gari lilitumbukia na kuteketea kwa moto.



Aliitaja maiti moja ambayo imetambuliuwa kuwa ni Padri huyo na nyingine ambazo ni za wanafunzi jitihada za kutambua majina yao zinaendelea kufanyika kutokana na kuungua moto vibaya, hivyo kusababisha kushindwa kuzibaini kwa haraka.



“Gari hili lilikuwa likiendeshwa na Padri Hyasint Kawonga wa kanisa katoliki Parokia ya Kigonsera, ambaye pia ni Mkurugenzi wa shule hiyo ya KCS naye amepoteza maisha katika ajali hii”, alisema Msikhela.



Hata hivyo taarifa zilizotufikia hivi punde, kesho kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Ruvuma ikiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu itakwenda katika eneo la tukio hilo ambako ajali hiyo imetokea.

No comments: