Lowassa, amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akisema hana mpango wa kushindwa.
Lowassa aliwasili katika Makao Makuu
ya CCM mjini Dodoma jana saa 10:20 jioni akiambatana na mkewe, Regina
huku akisindikizwa na wabunge mbalimbali pamoja na wanachama wa CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari
pamoja na wanachama waliokuwapo katika Ukumbi wa Makao Makuu ya CCM mara baada
ya kuchukua fomu, Lowassa alisema hawezi kuzungumzia upande wa kushindwa katika
safari yake.
“Swali rahisi sana, sina mpango wa
kushindwa,” alisema Lowassa alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa
habari kama atashindwa katika kinyang’anyoro hicho.
Alipoulizwa kuhusu hali ya nchi kuwa
na watu wanaoshambuliwa, Lowassa alisema atajenga Serikali itakayojali utu na
uhuru wa vyombo vya habari.
“Kwanza nimpe pole yule
mwandishi aliyeteswa. Sikubaliani na mambo ya kuingilia uhuru wa watu
kuteswa. Serikali yangu itaheshimu uhuru wa vyombo vya habari,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na wanachama wa CCM
waliokuwa wamefurika ndani na nje ya ukumbi huo.
Alipoulizwa kwanini anahusishwa na
vitendo vya ufisadi, Lowassa aliyekuwa akijibu maswali kwa ufupi, alisema kama
kuna mtu ana ushahidi na tuhuma hizo amtaje jina.
“Kama hawakunitaja hawakunihusisha…
Mtu anayejiamini aseme, na anitaje. Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi
viongozi kwa rekodi za matusi ila tutawapima kwa matendo yao,” alisema.
Kada huyo wa CCM alivitaka vyombo
vya habari kutoshabikia tuhuma zisizo na ushahidi, huku akisisitiza kuwa kila
mtu apimwe kwa rekodi yake.
Kuhusu uteuzi wa mawaziri, Lowassa
hakutaka kulizungumzia akisema bado hajavuka daraja.
“Nitavuka daraja nitakapolifikia,”
alisema.
Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa,
alisema ni sera ya CCM iliyotekelezwa baada ya kutokea mgogoro kati ya vyama
vya CCM na CUF.
“Angalieni kule Marekani, vyama vya
Democrat na Republican, vinashindana kwa kura chache sana. Hata sisi
tunapishana kwa kura chache, mimi nadhani kama hatupishani sana hivyo hilo
ndilo suluhisho,” alisema.
Awali Lowassa aliwashukuru wana CCM
waliofurika katika ukumbi huo akisema anajua kero za chama hicho na atakapokuwa
rais atazishughulikia.
“Nawashukuru kwa kunileta nyumbani,
nimeitumikia CCM kwa muda mrefu. Nilieleza Dodoma na Arusha nia yangu. Naelewa
matatizo wanayopata watumishi wa CCM, nayaelewa. Mishahara midogo,
hawakopesheki, hawana fedha za likizo na hawana uchumi mzuri. Wakati wengine
wanajengewa nyumba na mikopo wenyewe hawapati,” alisema Lowassa.
Hata hivyo, alimsifu Rais Jakaya
Kikwete kwa kuimarisha uchumi ndani ya chama hicho, lakini akasema akiwa rais
atafanya zaidi.
“Tunaweza kufanya zaidi, tusiwe
ombaomba. Nilipokuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini tumejenga jengo la
ghorofa 22 Dar es Salaam. Tuna viwanja na maeneo mengi. Nikichaguliwa kuwa rais
na mwenyekiti nitaangalia hilo…Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba,” alisema.
Baada ya mkutano huo, Lowassa
alikwenda kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Dodoma kupata udhamini wa chama hicho
ambapo Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pancras Ndejembi alikuwa
miongoni mwa wanachama waliomdhamini, akiwamo mlemavu wa miguu, Idd Omari.
Baadhi ya vigogo waliokuwa ukumbini
ni pamoja na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, Mbunge wa
Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na
Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah.
Akizungumza na wakazi wa Wilaya ya
Dodoma Mjini baada ya kuchukua fomu, Lowassa alisema vigelele na makofi
anavyopigiwa sasa haviwezi kumpeleka Ikulu isipokuwa wananchi wanapaswa
kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura ili iwe njia rahisi ya yeye kuwa
mkuu wa nchi.
“Naomba watu wajiandikishe,
hakikisheni watoto wenu, wajomba na hata washikaji zetu wanajiandikisha katika
Daftari la Wapigakura na nitarudi tena kwenu kuomba kura,” alisema.
Huku akishangiliwa na mamia ya
wakazi wa Dodoma, Lowassa aliwaambia amekwenda kuomba wadhamini na si kuomba
kura, kwani amebanwa na sheria na utaratibu wa chama chao.
Alisema ameguswa na mapokezi
waliyompa na kuwashukuru wadhamini wake kwa kumwamini na kusisitiza kuwa
atarudi tena kuomba kura.
“Leo siombi kura, naweka akiba ya
maneno hata wakihesabu nina kampeni potelea mbali, lakini nilipokuwa waziri
mkuu nilianza kuijenga Ikulu mnayoiona mpaka leo haijakamilika, nitakuja
kuikamilisha, maana yake nini, nahamia Ikulu Dodoma,” alisema mbunge huyo wa Monduli huku akishangiliwa na mamia
ya wananchi hao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment